SIFA YA KWELI INAYOUPENDA MOYO WA MUNGU

MUNGU aliweka nyingi za taratibu za ibada ya sifa katika Agano la Kale, akachangia sana kwenye kitabu cha Zaburi, ambacho maneno yake watunzi wengi wa nyimbo wanatumia hadi leo hii. Hata hivyo, baada ya karne chache kuwa zimepita Mungu ilibidi awakemee watu wake kupitia Isaya (29:13) kwa kumwabudu kwa midomo wala si kwa mioyo yao; jambo ambalo hata Yesu alilifanya wakati wa huduma yake. Miaka 3000 baada ya Daudi ingefaa Kanisa kuyatilia maanani haya maneno. Injili ya msalaba ilipoanza kuweka mizizi kwenye makanisa ya  ibada ya sifa ilianza kuleta sura halisi ya uhusiano wetu na Yesu Kristo. Watu wa Mungu wakaanza kuelewa ya kwamba sifa ya kweli na safi ni ile iliyoelekezwa kwa Yesu peke yake na ambayo imetoka katika moyo safi. Jambo lingine tofauti na hilo ni kuutumbuiza mwili tu, muziki mzuri unaochezwa na wanamuziki stadi! Daudi hasifiwi kwa kuwa alikuwa mtunzi mzuri wa nyimbo, au kiongozi mzuri wa sifa, bali anafahamika kama mtu ‘aliyeupendeza moyo wa Mungu’! Leo hii, inaonekana ya kwamba watu wengi wanaojihusisha na sifa na kuabudu wanajitahidi kuiga namna Daudi alivyotumia vipaji vyake; hawaelewi ya kwamba wanapaswa kuwa na hali ya moyo aliyokuwa nayo Daudi katika uhusiano wake na Mungu. Lengo ni Kuabudu “Kusifu na kuabudu sio njia ya kutafuta kibali kwa Mungu, au hata mbinu ya kumlazimisha atusikie na kututimizia haja zetu. Kusudi zima la kuabudu ni kumfanya mtu awe huru kuelezea shukrani zake kwa Mungu kwa yote aliyomtendea; kuufurahia uwepo Wake na kuukiri ukuu Wake. Muziki na nyimbo vinapaswa viwe tu njia ya kufanikisha hili lengo – lakini badala yake vimefanyika kuwa ndilo lengo kuu!” anasema Peter McKenzie, Mchungaji, Uingereza. Kama ilivyo katika mambo yaliyo na mchanganyiko wa misisimko, vipaji vya kimwili, kiburi na majivuno, mambo yanavuka mipaka haraka sana. Makanisa mengine leo hii yana fundisho la muziki na kuabudu, huku mengine yakisisitiza ‘ubora wa huduma’ kutoka kwa timu ya uimbaji: mavazi ya kisasa yanayofanana; muziki usiokuwa na dosari yoyote; vyombo vya kisasa vya bei ghali, n.k., mambo ambayo tunaweza kuyaita ‘matendo, sheria, na juhudi za kimwili’. Makanisa mengine yana vitengo vya muziki vyenye uongozi unaojitegemea mbali na uongozi wa kanisa, kwa sababu tu vinaliingizia kanisa fedha…Iwe ni katika nchi za Ulaya ‘zilizoendelea’ au katika Afrika au Asia, suala la kusifu na kuabudu limechukua mwelekeo wa aina yake, na linaonekana halina uhusiano na namna Mungu anavyoliona. Kwa hivyo, ingawa sifa na kuabudu linaonekana kuwa ni suala la ‘ndani’ la Kanisa – yaani, si jambo la kuuonyeshea ulimwengu – lakini moyo unaotoa hiyo ibada, nia sahihi, moyo sahihi, na muziki unaotokana na hayo mambo kwa vyo vyote utauathiri ulimwengu. Wakristo wanafurahia nyimbo za injili kuwepo kwenye ‘chati’ za miziki ya dunia; Jina la Bwana linatukanwa kwa kuchezwa kwenye vilabu vya usiku, ambapo vileo, madawa ya kulevya na uasherati vinaendekezwa; mapigo na midundo ya kidunia, na mavazi ya kidunia na kucheza dansi vinaendana na maneno matakatifu; kwenye baadhi ya makanisa ni vigumu kutofautishaa ibada zake na matamasha ya kidunia, kwani zinaambatana na fataki na vimulimuli; muziki wa Kikristo wa ‘rock’, kizazi kipya, ku-‘rap’, reggae…ni nini kitakachofuata? “Ulimwengu umelivamia kanisa”, anasema Miki Hardy. “Ni muhimu sana viongozi wake waamke na waangalie suala la kusifu na kuabudu kwa mtazamo tofauti, wa ki-Uungu!” Kulingana na Moyo wa Mungu Katika Yohana 4, Yesu anaeleza tutakavyojaliwa kumwabudu Mungu ‘katika Roho na katika kweli’ kupitia wokovu utakaokuja kwetu sisi, Kanisa. ‘Wakati’ aliozungumzia ni wakati wa kifo chake msalabani, ambacho kingefungua njia mpya na tofauti ya kumwabudu Mungu katika uhuru na kwa moyo safi. Kuna gharama iliyolipwa kutuwezesha tumwabudu Muumba wetu kwa jinsi hii! “Hakuongea na mwanamke Msamaria kama kiongozi wa sifa; bali alikuwa akiufunua moyo wa Baba kwa Kanisa lake”, anasema Eugene Nyathi – Mchungaji na Mtunzi wa nyimbo, Zimbabwe. Yesu alitufundisha kumpenda Mungu kwa nafsi yetu yote. Na ni kwa kuyafananisha maisha yetu na kuteswa kwake, kifo chake na kufufuka kwake – injilii ya Msalaba – ndipo tutakapoweza kumwabudu sawasawa na moyo wa Mungu. “Sifa ya kweli ni matokeo ya maisha yaliyotolewa sadaka kwenye barabara ya msalaba”, anasema Roland La Hausse – Mzee wa Kanisa, Mauritius. Kumpendeza Mungu Wanamuziki wengi wanaonekana kuchukulia vipaji walivyopewa na Mungu kama kitu cha kujiletea manufaa na maslahi binafsi na utukufu, huku wakisahau kuwa, kama ilivyo kwa vipawa vingine vilivyotolewa Kanisani, hivi vipaji ni kwa ajili ya kuwahimiza watu wamwabudu Mungu. Ni maisha ya waimbaji yaliyosalimishwa na kutolewa yanayompendeza Mungu na kufungua mlango kwa ajili ya hicho kipawa kuchukua nafasi yake stahili Kanisani. “Nina hakika Bwana hufurahia sauti nzuri…ila ninaamini hufurahia zaidi sauti mbovu inayotoka katika moyo safi!” anasema Vanessa Fitzroy – Muimbaji, Mauritius; ambapo anaongeza Jonathan Hett, mcheza violini kutoka Mauritius: “Nilipojiunga na kikundi cha uimbaji, niligundua haraka sana ya kuwa jambo la muhimu zaidi halikuwa uwezo wangu; bali ni maisha yangu yaliyotolewa madhabahuni, katika hiyo wiki!” Uhusiano Sahihi Ibada ya kweli si ibada ya Jumapili tu. Wakristo wote wameitwa wadhihirishe moyo wa sifa kama kielelezo cha imani yao, unaotokana na shukrani waliyo nayo siku kwa siku. Wakati huo huo, maombi na sifa za kweli zinakuwa ni madhihirisho ya kile tulichobeba mioyoni mwetu; kama hakuna kitu, itabidi tuigize. Zaburi za Daudi ni kielelezo cha uhusiano wake na Mungu. Hakuna eneo la maisha yake lisilokuwa wazi kwa ajili ya kuguswa na Bwana. Anamwelezea Mungu kuwa ni mwamba wake, ngome yake, kimbilio lake, msaada wake, nguvu yake…anayesikiliza, na kusikia, kilio chake na maombi yake. Kutokana na uhusiano wa jinsi hiyo, ni wazi kwamba Daudi angeweza kuandika na kuimba zaburi za jinsi hiyo. 2 Mambo ya Nyakati inasema: “Na wakati ilipoanza sadaka hiyo ya kuteketezwa, ukaanza na huo wimbo wa BWANA...” Clara Grant – muimbaji toka Mauritius, anaelezea kipindi alichopitia cha utupu wa rohoni, na ugumu wa moyo kwa Bwana: “Niliimba kwa sababu nilifahamu maneno, lakini kusifu kwangu kulikuwa kumekufa kabisa. Lakini, mara tu niliposalimisha kila kitu na nikawa tayari kuuchukua msalaba wangu na kumfuata Yesu katika yale mazingira, sifa ilibubujika kutoka katika roho iliyopondeka.” Si kwa Jumapili tu Kwa maana hiyo, sifa si kijisanduku cha maisha ya Mkristo, kinachofunguliwa pamoja na timu ya uimbaji Jumapili asubuhi. Ni udhihirisho wa hali ya juu wa mtu aliyeyasalimisha maisha yake kwa Mungu kwani inahusisha nafsi yake yote… Kwa kadiri Roho anavyotuongoza, sauti zetu zinaimba, mikono yetu inapiga makofi, miguu yetu inacheza… tunapata utoshelevu mwingi katika kukisogelea kiti cha enzi cha Mungu na uwepo wake. Tunamwabudu Mungu wetu si kupitia uimbaji tu, bali kwa kusalimisha kwake karama zetu na vipaji vyetu, muda wetu, pesa zetu, huduma zetu, na maisha yetu kwa ujumla wake wote. Pale Mungu alipowaletea watu wake ukombozi na ushindi katika Agano la Kale, nyakati za kipekee za kusifu na kuabudu zilishuhudiwa, zikidhihirishwa kwa moyo wa furaha, uimbaji na kucheza. Madhihirisho mengine ya sifa na kuabudu yalitokea walipoletwa kwenye toba; na pia kila wakati waliposujudu mbele zake katika kumkumbuka kuwa Yeye ni nani… Mungu Mkuu, Mungu mwenye uwezo na upendo! Kwenye Agano Jipya, kusifu na kuabudu vinapaswa viwe kwa sababu zizo hizo, na kwa kufuata utaratibu huo huo, pamoja na kushukuru kutokana na kwamba Yesu, Mwana wa Mungu, alikuja kuleta wokovu, ukombozi, na ushindi kwa wote wanaomwamini. Lakini haitoshi tu kujumuika katika kumsifu na kumuabudu Bwana, ikiwa mioyo yetu haiko sawa kwake na kwa watu wengine. Tusisahau ya kwamba hakuna jambo tunaloweza kufanya kwa nguvu zetu na kwa uwezo wetu linalokubalika mbele za Mungu. Ni lazima tuhoji, basi, ni kwa nini katika mengi ya makanisa leo hii mkazo umewekwa kwa kile mwanadamu anachoweza kufanya kwa kipaji chake cha uimbaji na ni kiasi gani cha uwezo wake kilichoelekezwa katika kutumbuiza. Dhana ya ‘ubora wa huduma’ pia imeenea, kana kwamba tunaweza tukampendeza Mungu kwa kwaya zetu zenye mavazi mazuri, vyombo, na kadhalika… Yesu huangalia Moyo Jocelyn Sery – Mzee wa Kanisa na mtunzi wa nyimbo kutoka St. Pierre, La Reunion, anasema: “Nilitumia miaka mingi yenye kukatisha tamaa nikijitahidi kutumia kanuni za kibiblia katika sifa, bila kuyafananisha maisha yangu kikamilifu na msalaba wa Kristo. Kabla ya kuja huo ufunuo, na msalaba kuanza kufunua nilichokuwa nacho moyoni mwangu – jinsi mwili wangu ulivyokuwa umeunda mbinu za kuficha uongo ulioyatawala maisha yangu – nilikuwa sielewi kabisa Yesu alichomaanisha aliposema tutamwabudu katika Roho na katika kweli. Nikaona jinsi sheria, au mkono wa mwanadamu, ulivyokuwa umeikanyagia chini neema ya Mungu. Nilimwabudu Mungu kwa kanuni za kibinadamu; lakini, machoni pa Mungu, sifa yangu ilionekana ya uongo. Amosi 5:23-24 na 6:5 inatuonyesha jinsi Mungu asivyoangalia vipaji vyetu vya uimbaji. Ni kwa sababu Yeye husikia mambo ambayo sauti zetu haziyatamki. Yeye huona mambo yote tunayojaribu kuficha…Kwa sababu ushirika wa Mungu si pamoja na miili yetu, bali na mioyo yetu!” Sifa iliyonajisiwa na Ulimwengu Katika makanisa mengi na matamasha, ibada ya sifa imechanganyikana na roho ya dunia kiasi kwamba ni vigumu kutenga ya Mungu na ya dunia. Uongozi wa makanisa umeruhusu kughoshi ili ‘kuwaweka vijana kanisani’. Hata kucheza kuliomo katika mengi ya makanisa si matokeo au matunda ya ushindi, kama Daudi alivyocheza mbele za Bwana wakati wa kulileta sanduku la agano kwenye mji wa Mungu. Leo hii Wakristo hawahitaji ushindi au kumbukumbu ya kile Bwana alichofanya ili waenende kana kwamba wako kwenye vilabu vya usiku… Kucheza, kurukaruka na kuchezesha miili yao kwa kufuata miziki ya kidunia na yenye kusisimua hisia kwa kiwango cha hali ya juu. Mungu na atusaidie! “Wanafanya mambo kanisani ambayo wangetamani kufanya duniani!” anasema Miki Hardy. Malengo ya Kidunia Joelle Atisse – Mtunzi wa nyimbo, Curepipe, Mauritius, anasema: “Nakumbuka juhudi zangu za kutaka kufanya vizuri, nikijua watu wangesifia uimbaji wangu... Ndani mwangu nilikuwa na makusudi na malengo ya kuwa mtu ambaye angependwa na mwenye kufurahisha machoni pa watu wote... Lakini, kadiri nilivyozidi kusikiliza Injili ya Msalaba, haya makusudi yote yakadondoka, moja baada ya lingine; Bwana ananielekezea kioo cha kunionyesha jinsi ninavyokuwa dhaifu wakati siubebi msalaba. Naona waziwazi kwamba roho ya dunia inauteka moyo wa mwanadamu na kumpeleka mbali kwa muziki wa giza unaovutia tu hisia zake. Unaweza ukaathiri au kuambukiza ujumbe wowote mzuri au mbaya kwa njia ya maneno na nyimbo. Nyimbo zenye upako na zilizovuviwa Roho wa Mungu zinapoimbwa, Roho wa Mungu anatembea na anagusa, anaponya, anavunja, anakemea na kuifariji mioyo. Kwa upande mwingine, nyimbo za kidunia zinatoa mwanya kwa Shetani ambapo maisha ya watu yanapata athari mbaya na hatimaye kuharibiwa. Mimi natamani zaidi na zaidi Roho aniongoze. Nimekuja kugundua ya kuwa pamoja na udhaifu wangu na kasoro zangu, Bwana anapendezwa na moyo mnyofu usiotaka kuchanganya, bali unaotaka kujisalimisha kikamilifu kwake.” Kile Yesu alichonena katika Yohana 4 ni ibada yenye uhalisia na ya kweli itokayo katika vina vya mioyo yetu na iliyomwelekea Kristo tu. Hili linadhihirisha jinsi moyo wa kiongozi wa sifa unavyopaswa kuwa msafi, kwa sababu alichobeba ndicho atakacholivuvia Kanisa. Udhihirisho wa Moyo Wangu Eugene Nyathi – Mzee wa Kanisa na mtunzi wa nyimbo, Zimbabwe, anasema: “Kwa sababu hii, sifa haianzi pale tunapoimba wimbo. Uimbaji ni udhihirisho wa moyo wangu kwa Mungu. Mungu huangalia hali ya moyo wangu zaidi ya maneno ninayoimba. Ninawafahamu watu wengi wa Mungu wenye sauti zisizovutia. Hebu fikiri ingekuwa sifa ingepimwa kwa aina ya sauti. Ingekuwa hivyo, basi wengi wasingemwabudu Mungu... hakika si machoni petu! Mwimbaji mwenye sauti mbaya anaweza asivutie sana, lakini huyo mtu anaweza akawa mbele ya kiti cha enzi cha Mungu kwa wakati huo, akitazamana na Mungu uso kwa uso. Ila kwako wewe, kile wanachoimba kinaonekana kutokukubalika kwa kuwa hakina ‘mvuto’. Lakini kumbuka Mungu huangalia mioyo. Ni zaidi ya muziki au nyimbo nzuri, au uimbaji mzuri... ni maisha yako!” Kutokana na shuhuda zote hizi, tunaona ya kuwa moyo sahihi na ufahamu sahihi juu ya uhuru tulio nao katika Kristo ndio msingi wa yote tunayofanya kuhusiana na sifa. Kama mtu mmoja alivyosema: “Muziki si sifa, ila sifa inaweza ikawa muziki!” Kuabudu kwa njia ya Ufunuo Jean-Jacques Fabien, Kiongozi wa sifa na mtunzi wa nyimbo toka Curepipe, Mauritius, anasema: “Ni sharti pia kuwepo na ufunuo wa neema ya Mungu ili tumwabudu katika uhuru na si kwa kanuni. Huu ufunuo unaweza ukadhihirika na kukua tu mioyoni mwetu tunapohubiriwa injili ya Msalaba wa Yesu; msalaba ukiwa ni mahali na muda ambapo mabadiliko yalifanyika katika namna ya kuweza kuufurahia ushirika na maisha yetu naye... si tena katika roho, au kanuni, au sheria yeyote ile ya Agano la Kale, bali katika neema yake. Ninaamini tumeitiwa uhuru wa kuyaishi maisha ya ufunuo wa msalaba na wa neema ya Mungu kusudi tutembee katika ngazi ya juu zaidi ya sifa... sifa ya kweli inayompendeza Mungu. Kwangu mimi, sifa ina uhusiano na maisha yangu katika ujumla wake, na si muziki!”

Comments