UKARIBU NI MUHIMU KATI YA WANANDOA WAKRISTO

Suala la ukaribu kati ya wanandoa Wakristo hasa wale waliookoka na kumfanya Kristo Yesu kuwa ni Bwana na Mwokozi wa maisha yao limekuwa ni la kufumbiwa macho ama kupuuzwa. Ukaribu ninaouzungumzia sio tu wa kuwa pamoja wakati wa kulala, kula ama kwenda kanisani bali ni kuhusiana na mambo mbalimbali yanayoonekana madogomadogo lakini yana umuhimu sana katika hali ya kuboresha mahusiano ya wanandoa na familia kwa ujumla.

Wakristo wengi tumekuwa tukiona ndoa za watumishi wakubwa zikikumbwa na misukosuko na kuanza kumtupia lawama za kwanza adui wetu nambari moja ambaye ni shetani atajwaye na biblia kuwa ni baba wa uongo. Lakini ukichunguza ukweli wa mambo unaweza kuona kuwa sisi wenyewe ndiyo chanzo cha hayo matatizo.

Kuna mambo mazuri na ya muhimu ambayo wanandoa wanapaswa kushirikishana na kujuzana lakini wengi wao huona haya na woga kufanya hivyo kwa wenzi wao wa maisha. Mambo hayo si mengine bali ni yanayohusiana na hali za kibaiolojia, hisia, kijamii na mengine yafananayo na haya.

Nikianza kuzungumzia hali ya kibaiolojia, ningependa nigusie suala la mzunguko wa siku za akina mama. Suala hili ni muhimu kwa wanandoa wote wawili kujua mzunguko unavyoenda na kama kutakuwa na mabadiliko yeyote ni muhimu kwa mwanamke kumtaarifu mumewe. Kabla sijatoa faida za kujua mwenendo wa siku hizo nitoe ushuhuda nilioupata kutoka kwa kijana (jina linahifadhiwa) mmoja aliyeishi na mkewe kwa takribani miaka miwili bila kujua hali ya mwenendo wa siku zake.

Alikuwa ananieleza kuwa alikuwa wakati mwingine analazimishwa na mkewe kupata faragha wakati wakiwa wameshashiriki kwa siku zipatazo nne mfululizo na hivyo kuishiwa nguvu na kuhitaji muda wa kupumzika kwa siku hiyo.

Pia, alikuwa ananitanabaishia malalamiko yake kuwa siku nyingine alikuwa anamkuta mke wake katika hali ya tofauti; yaani kukosa furaha na kutohitaji hata kuwa naye karibu na hivyo kumfanya akwazike na kuona maisha ya ndoa siyo paradiso ndogo iliyo duniani kama wanavyoeleza watumishi wa Mungu mabalimbali.Haya ni baadhi tu ya madhara ambayo aliyapata kutokana na kutojua mzunguko wa siku za mkewe.

Mzunguko wa siku ni muhimu kafahamika kwa mwanaume kwasababu kuna siku zinaitwa siku za ‘heat’; hizi ni siku ambazo mwanamke anakuwa anawiwa sana kuwa karibu na mumewe kwa ajili ya faragha (faragha inayoelezwa kwenye 1kor 7). Hivyo Mwanaume akifahamu kuhusu hili atampatia mkewe faragha ya kutosha na hivyo kutokuwa na tatizo la mwanamke kutafuta faragha nje ya ndoa. Kijana huyo inaonekana kuwa alikuwa anatoa faragha ya kutosha kwa mkewe sikuambazo mkewe hakuhitaji sana, wakati ingefaa zaidi kutoa faragha ya kutosha katika siku zile zinazotakiwa kwa mwanamke.

Vilevile, wakati wa ‘bleeding’, mwanamke huwa na hali Fulani za tofauti lakini hali iliyozoeleka ni ile ya kuwa na hasira inayoweza ambatana na kiburi. Hii ni hali inayosababishwa na mambo ya vichicheo vya mwa mwili, na si uhiyari wake. Hivyo nikamsahuri huyo kijana kuchukuliana na mke wake wakati anapokuwa katika siku hizo, ili kudumisha mahusiano yao na kutomchukulia vibaya.


Comments