Skip to main content
ASKOFU SHAO APINGA WACHAGA KUZIKANA KWENYE 'VIHAMBA'...
 |
ASKOFU Dk Martin Shao |
ASKOFU
wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya
Kaskazini, Dk Martin Shao, amekosoa utamaduni wa wakazi wa mkoa wa
Kilimanjaro, ambao wengi ni Wachaga, wa kuzikana nyumbani (vihamba) na
kusema ni utaratibu wa hovyo.
Akifafanua kauli hiyo juzi, Askofu huyo alielezea hofu ya kupotea kwa
mashamba ya mibuni mkoani humo, kutokana na utamaduni uliosababisha
ongezeko la makaburi kwenye mashamba hayo.
“Naomba Serikali mkoani, iweke utaratibu wa kudumu wa maeneo ya maziko
badala ya watu kuzikwa ovyo majumbani… ardhi hii ni ndogo, lakini bado
tunaimega kwa kuzika, hapo baadaye hatutakuwa na mashamba ya mibuni,”
alisema.
Askofu huyo aliiomba Serikali kuelimisha wakazi hao, ili wabadili mfumo
wa kugeuza makazi na mashamba yao sehemu ya kuzika ndugu zao, ili
kutotumia vibaya ardhi ndogo iliyopo.
Alisema hayo wakati wa harambee ya kuchangia Sh milioni 95 za ujenzi wa
Kanisa la Usharika wa Nanjara wilayani Rombo na kusisitiza umuhimu wa
Serikali kuweka utaratibu wa maeneo ya kudumu ya maziko.
Makazi
Kwa mujibu wa Askofu Shao, licha ya hatari ya kupunguza mashamba ya
mibuni ambayo ndiyo nguzo ya uchumi wa mkoa, lakini pia utaratibu wa
sasa wa kuzikana majumbani, utaathiri vizazi vijavyo na kusababisha
vikose maeneo ya ujenzi wa makazi.
Alisema kutokana na mkoa kubuni miradi mikubwa ukiwamo wa soko la
biashara la kimataifa la Lokolova na mji wa kitalii wilayani Siha, ni
matumaini ya Kanisa kuwa pia Serikali itaandaa utaratibu wa kila wilaya,
kutenga maeneo ya maziko ya jumuiya.
Dk Shao alisema iwapo mpango wa kila wilaya kutenga maeneo hayo
utashindikana, Kanisa litakuwa tayari kununua ardhi kwa ajili ya waumini
wake.
Akijibu ombi hilo, Naibu Waziri wa Nchi, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi), Aggrey Mwanri, alisema amelisikia na atalifikisha kwa
Kamati ya Ushauri ya Mkoa ili ufumbuzi upatikane.
Mwanri pia alishukuru Kanisa kwa kutambua mchango wa Serikali kuleta
maendeleo ya wananchi. Katika harambee hiyo, Sh milioni 35.5
zilipatikana.
Comments