Skip to main content
WAZIRI WA ZAMANI AWA ASKOFU MKUU
 |
Kilontsi Mporogomyi |
MW
A N A S I A S A mkongwe nchini aliyepata kuwa Mbunge wa Kasulu
Magharibi kwa miaka 10 na Naibu Waziri wa Fedha enzi za utawala wa Rais
Benjamin Mkapa, baada ya kipindi kirefu cha ukimya, sasa ameachana na
siasa, amegeukia kumtumikia Mungu kama Askofu Mkuu.
Kilontsi Mporogomyi kwa sasa ni Askofu Mkuu wa Kanisa la Muujiza,
Uponyaji, Kufunguliwa na Utajirisho, ambalo lipo Makongo Juu, Dar es
Salaam na linahubiri utajiri wa hekima ya Neno la Mungu, fedha na afya
na linalopinga umasikini kwa kigezo cha wokovu.
Katika mahojiano maalumu na gazeti hili wiki hii, Askofu Mkuu Mporogomyi
alisema anafurahia kuwa mtumishi wa Mungu, kwa kuwa hajawahi kujutia
safari ya kumtumikia Mungu aliyoianza mwaka 2006 na kutimia 2009, lakini
anakerwa na namna umasikini unavyoendelea kulitafuna Taifa wakati uwezo
wa kupambana nao upo.
Alisema katika kipindi cha miaka kadhaa ijayo, maono yake ni kuwa na
waumini wenye uchumi mkubwa ambapo anajiandaa kufungua miradi ya
kiuchumi itakayowezesha waumini kujipatia kipato.
Alisema sasa anajiandaa kuendesha harambee ya ujenzi wa kanisa jipya
Oktoba, sehemu kubwa ya fedha za ujenzi ikitoka kwake na waumini kwa
hiari kupitia ‘kupanda mbegu’.
Mwanasiasa huyo mkongwe, alisema njia pekee ya Tanzania kumaliza tatizo
sugu la umasikini ni kuweka mkazo katika kukusanya kodi na kuondoa
msamaha wa kodi kwa baadhi ya kampuni kama za simu, madini na mafuta,
ikiwa ni njia pekee ya kuongeza mapato ya nchi.
Aidha, alishauri serikali ipange mkakati wa wazi wa kuwezesha wawekezaji
wazalendo badala ya kuelekeza nguvu kubwa kwa wageni. “Tunaweza kuiga
mfano wa nchi za wenzetu, kwa mfano Afrika Kusini, wameamua kuweka sera
za kuinua wawekezaji weusi kwanza, suala hili lipo wazi, tuache dhana
kwamba mtu mweusi hawezi, nani kasema hili?
“Serikali ijenge mazingira ya kuinua watu wake kuwekeza ili fedha zibaki
nchini na kuendeleza uchumi wa ndani badala ya kubebwa wote na
wawekezaji wa kigeni ambao asilimia kubwa ya faida inakwenda kujenga
kwao,” alisisitiza Askofu huyo ofisini kwake mtaa wa Indira Gandhi.
Alisema haikuwa rahisi kuacha siasa na kufanya kazi ya Mungu ingawa hata
wakati akiwa Mbunge, alikuwa Mchungaji wa Kanisa hilo ambalo sasa ni
Askofu Mkuu.
Alivyoanza Alisema sauti ya Mungu kumwita aliisikia kupitia mgonjwa
aliyemwombea India, alikokwenda kutibiwa baada ya kupooza baadhi ya
viungo vya mwili na kulazimika kufanyiwa operesheni zaidi ya mara tano.
“Mgonjwa nilimwombea apone saratani, akiwa kitandani hajiwezi, kwa
maombi yangu alikaa na kuzungumza nami kimwujiza, nilianza kumwona
Mungu, mgonjwa yule ni miongoni mwa wengi nilioombea wakapona katika
Hospitali ya Apollo. “Yeye alipoongea nami aliniambia Mungu ameweka
huduma ya kuombea watu ndani yangu na nikirejea Tanzania natakiwa
kuifanya, nilitii na ndiyo sababu naifanya, nimemwona Mungu katika
huduma hii,” alisisitiza Askofu huyo.
Alisema, yeye na waumini wake wapatao 150 wa Dar es Salaam, wanaamini
katika uzuri wa fedha na wala fedha si dhambi kama baadhi ya viongozi wa
kidini wanavyohubiri, alisema bila fedha huduma ya Mungu haisongi mbele
na kubaki kuombaomba, ukiwalazimisha waumini ambao ni masikini, nao
watoe hata wasivyonavyo, wengine wataishia kuiba ili wamridhishe
Mchungaji.
Alisema yeye anatoa sehemu ya mali na fedha zake kusaidia wahitaji na
anakiri kutokana na huruma yake katika kutoa, kusaidia watu kutatua
matatizo yao kwa kufungua miradi, kuwafadhili kwa mikataba rasmi, na
alipata kutapeliwa fedha zinazokaribia Sh bilioni moja na kwa kuwa ni
mtumishi wa Mungu, alisamehe akijua atapata zaidi ya hizo.
Alisisitiza kusikia baadhi ya wabunge kuwa na mabilioni ya fedha,
wengine kuzihifadhi nje huku akikiri kwamba wakati akiwa mbunge,
akitokea Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kuwa Mshauri wa
Masuala ya Uchumi akiiwakilisha Tanzania, hakuishi maisha ya ubunge kwa
starehe kutokana na kipato alichokuwa akipata, kuwa kidogo kuliko
mahitaji jimboni mwake.
“Mbunge au waziri mwenye fedha nyingi ameiba, ubunge si fedha, ni karaha
ikiwa kweli umeitwa kutumikia, ni lazima uwe tayari kuchangia ujenzi wa
madarasa, zahanati, barabara, madaraja na majanga yatakayotokea
jimboni, achilia mbali watu wanaokuja binafsi kuomba msaada mpaka
nyumbani kwako, utakuwa tajiri kivipi?” alihoji Baba Askofu Mporogomyi.
Akizungumzia hali ya Bunge sasa, alisema baadhi ya watu hawana maadili,
wanafanya Bunge mahali pa vurugu, anakiri nidhamu kushuka, hivyo
anashauri kanuni ziboreshwe na kurejesha heshima ya Bunge, akiongeza
kuwa wapo vijana wenye akili bungeni, wanaopaswa kupewa nafasi
kudhihirisha uwezo wao kwa Taifa.
Comments