“KUDHARAULIWA NI DALILI YA UTENDAJI MBOVU KWA KIONGOZI YEYOTE”

NA MWL VICENT MWENGO.


BWANA YESU ASIFIWE NDUGU ZANGU,

Ninamshukuru mwenyezi Mungu aliye mwingi wa Rehema na neema kwa kuniwezesha kuwaletea habari hizi.
Je wewe ni kiongozi au una mpango wakugombea nafasi yoyote kuwaongoza watu? Au hauna mpango wowote wa kuongoza watu (umma) lakini unataka kujua misingi ya uzuri wa kiongozi wako, basi hebu fuatana nami mpaka mwisho.

Najua unajua kabisa, hususan kwa wale wakristo wenzangu kuwa Mungu ametuamuru kuziheshimu mamlaka za duniani. Habari za uongozi si mpya kabisa maana ni jambo ambalo lipo kiuhalisia; uongozi umekuwepo, upo, na utakuwepo tukwenye jamii yoyote. Kuna usemi usemao; "kwenye watu wawili, mmojawapo ni kiongozi wa mwenzake".. Ukiwa mwamini wa uwepo wa Mungu najua unajua kuwa ni lazima kuwaheshimu wanaokuongoza kwenye jamii yoyote, hii ikiwa ni pamoja na kuanzia ngazi ya familia, ukoo, kabila na hata kitaifa. Kwa hiyo sifa kuu ya anayeongozwa popote pale na ngazi yoyote ni kuwaheshimu wanaowaongoza.

Ushirikishwaji au wepo wa Mungu kwa viongozi wengi huwa hawachukulii maanani, kwani wengi wameendelea kujiaminisha katika uwezo wao wa kifedha na elimu zao, au umaarufu wao ndani ya jamii lakini matokeo yake mara nyingi huwa si mazuri.

NB: Hebu tujifunze kitu kutoka kwa mtumishi wa Mungu Ayubu, yako mambo aliyasema japo alikuwa akimlalamikia Mungu kwa sababu ya uchungu wa kuugua kwake akidhani Mungu amemuacha lakini ndani ya maneno yale alieleza vizuri ni nini kinatokea Kiongozi akiwa na Mungu na asipokuwa na Mungu pia.

:: Je uzuri wa kiongozi wako umeupima kwa vigezo/misingi ipi?

KIONGOZI YEYOTE ANAYEWAJIBIKA VIZURI ATAKUWA NA SIFA ZIFUATAZO

1. KUWATUMIKIA UNAOWAONGOZA
Kiongozi mzuri ni lazima awajibike kwa matendo, kuwaona anaowaongoza ni sehemu ya maisha yake; hii ikiwa ni pamoja na kukereka na udhalimu ndani ya uongozi, kukemea, na sio kukemewa juu ya rushwa, na mikamndamizo ya namna yoyote ile ya kibinadamu. Kuwa mtu wa msaada kwa wasiojiweza, kuhakikisha kila lililopangwa linafanyika. Yote haya yatakufanya kuwa mtu wa Baraka, maana kila ulimi utakapokuona utakubariki kwa ufanisi wako kiutendaji.

Rejea Ayubu 29:11 “Maana sikio liliponisikia ndipo likanibarikia na jicho liliponiona likanishudia, 12.kwa sababu naliwaokoa maskini aliyenililia, yatima naye na Yule asiyekuwa na mtu wa kumsaidia. 15 Nalikuwa macho kwa kipofu, nalikuwa miguu kwa aliyechechemea. 16.Nalikuwa baba kwa mhitaji”

2. MKONO WA ULINZI WA MUNGU UTAKUWA PAMOJA NA WEWE
Sura ya 29 mtumishi Ayubu anakumbushia kichwani mwake akidhani kwa sasa Mungu amemacha kwa kusema.
Ayubu 29:2 Laiti kama ningekuwa kama miezi ya kale, katika siku hizo Mungu aliponilinda.

Ayubu anakiri kuwa alilindwa na Mungu kwenye nyendo zake nyakati za uzima wake, vivyo hivyo dhana hii inaonesha kuwa kiongozi yeyote anayemtii Mungu ategemee kulindwa na ndio maana mara kadhaa pia Mungu anasema usiogope kwa sababu anauhakika atakulinda mwenyewe dhidi ya wabaya na mabaya yao.

3. MATAMKO YAKO YATAHESHIMIWA KAMA UTAKUWA NA MUNGU
Ayubu anaendelea kusema 29:21.Watu walitega masikio kunisikiliza na kungoja, wakanyamaa kimya wapate sikia mashauri yangu. 22.Hawakunena tena baada ya kusikia maneno yangu. Matamko ni dalili ya kuheshimika pia, kwa sababu ya hekima na busara zako njema, hata matamko yatakayotoka kwako yatabeba mtazamo mwema ndani ya jamii na kumfanya kila mmoja kukosa neno kupinga maana linaleta majawabu ya shida zao.

Siku zote jamii huwa inaheshimu, busara, maarifa na hekima za mtu, na sio elimu ya mtu cheo au mali za mtu. Jiulize viongozi wangapi wamekejeliwa, wamesemewa mabaya na kutukanwa hata na watoto wadogo, hata kama haikuwa moja kwa moja kwa sababu tu ya maneno au matamko yao. Naamini utaungana name kuuamini msingi huu. Mungu atusaidie sana!

4. KUFANYA MAAMUZI SAHIHI NA MATAKWA YA WATU
Tunajua kabisa kitu kama hekima, maarifa na busara zinatoka kwa Mungu mwenyewe, lakini upeo, ufahamu na elimu tunazitafuta wenyewe toka kwa watu wanaojua mambo hayo. Ukiwa kiongozi siku zote unategemewa kufanya maamuzi ya busara yenye maslahi ya wanaoongozwa, lakini pia ili iwe hivyo, haina budi kuwa na busara, hekima na maarifa juu ya mambo yanayokaabiliana na uongozi wako. Kwenye hayo yanayotoka kwa Mungu kiongozi anapaswa kuomba kwa Mungu na ndio maana uwepo wa Mungu ni muhimu sana.

Mpendwa wa Mungu Ayubu anakiri kuongozwa na Mungu; Ayub29:3. Akisema “hapo taa yake ilimulika juu yangu kichwani, nami nilitembea gizani kwa mwanga wake; 4.kama nilivyokuwa katika siku zangu za kukomaa, hapo siri ya Mungu ilipokuwa hemani mwangu. 5.Wakati Mwenyezi alipokuwa angali pamoja nami”. Mungu tunaomba uwepo wako ndani ya jamii yetu.

5. MUNGU ATAKUHESHIMISHA NA KUKUHEKIMISHA.
Zek 3:7 “BWANA wa majeshi asema hivi, kama ukienda katika njia zangu na kama ukishika maagizo yangu, ndipo utakapoihukumu nyumba yangu, nawe utazilinda nyua zangu, nami nitakupa nafasi ya kunikaribia kati ya hao wasimamao karibu nami.”

::Kwa vigezo hivyo vichache naamini utaweza kujipima navyo au kuwapima viongozi wako. Naamini sasa utaweza kuzipima kelele za viongozi wako huhusan wanasiasa majukwani, kujisifu kwingi kwao, mbwembwe za misaada ambayo mpaka watangazwe ndio wanatoa; (mcheza ngoma ndugu zangu hajisifu, anasifiwa na waangaliaji).

Ninayaandika haya, ili jamii ijue! Najua kipindi ninawaandikia makala hii, viongozi hussani wanasiasa walioko madarakani na wasio madarakani eti wamepata roho ya upendo upya tangu walipopata uongozi na wengine tangu walipokosa uongozi. Kwa sasa wanaendelea kuwa karibu sana na vijana, na wazee ikiwa umebaki muda mfupi kufikia uchaguzi wa 2015. Wanawapenda kweli kweli hawa ndugu! Sasa misaada kama vifaa vya michezo kwa vijana vimeanza kumiminika nk, wazee nao misaada yao ndio imefika sasa ya nguo na vijisenti vya kujikimu nk. Mmh viongozi wako pamoja sana na jamii na wanaitetea kweli kweli. Wale walioko uongozini pia wanaendelea kuwatia moyo hao ndugu kuwa wakubari mafanikio waliyoyafikia maana si kazi rahisi. Wanaendelea kusema; huduma za umeme, maji vijijini, Afya na elimu ni mambo mtambuka lakini tayari vimeshafanyiwa uchambuzi yakinifu na viko kwenye mchakato wa utekeleezaji. INAKERA SANA!
!

ITAENDELEA.

BY MWL VICENT MWENGO.

Comments