“KUDHARAULIWA NI DALILI YA UTENDAJI MBOVU KWA KIONGOZI YEYOTE” (sehemu ya mwisho)

 Na Vicent Mwengo

INAENDELEA

SIJUI VIONGOZI/WATAWALA WETU WANAELEWA KWELI!!
KAMA KUDHARAULIWA NI DALILI YA UTENDAJI MBOVU KWA KIONGOZI YEYOTE!!

Japo si kweli kuwa Ayubu alitenda dhambi ndio maana akapatwa na mateso yale. Lakini watu wakaanza kumdharau na dhihaka za maneno za kila namna, tena hata wale aliowadharau yeye kipindi cha uzima wake nao walimdhihaki sasa. Wale watu kwa kuwa walimjua vizuri Ayubu kuwa ni mtumishi wa Mungu, waliamini kwa vyovyote tu ayubu atakuwa ametenda dhambi, sasa kwa kuwa ameteda dhambi basi uwepo wa Mugu haupo tena ikawa ni kila mtu kusema na lake. Dhana hii kwa kiasi fulani pia inaonesha kuwa ukiwa kiongozi mzuri watu watakuheshimu, kinyume chake ni kudharauliwa!

Mwanzo ulikuwa kiongozi mzuri, sasa kila siku linapotajwa jina lako watu wanatema mate, wanajuta uwepo wako uongozini, kauli zako hazina nguvu tena, ukisema wewe kauli moja; kila mtu anakujia na kauli zake kadhaa, mashauri yako hayathamini tena, misaada yako inatazamwa kwa wasi wasi sana, kila ulimi unakukiri mabaya juu yako, hapana ulimi wenye kukubariki, wanaokubariki ni wale tu wanaokiriwa mabaya kama wewe. hujiuhoji tu ni kwa nini!

Rejea Ayubu 30:1 Lakini sasa hao walio wadogo wangu hunifanya mzaha, ambao baba zao niliwadharau hata kuwaweka na mbwa wa kundi langu,
8 Wao ni wana wa wapumbavu naam watoto wa wahuni; walifukuzwa watoke katika nchi. 9. Na sasa nimekuwa wimbo wao, naam nimekuwa simo kwao,11. Wala hawajizuwii tena kwangu

HUSSANI KWA VIONGOZI; HEBU MJIHOJI WENYEWE MIOYONI MWENU.

1. Zab 41:1 Inasema; “Heri amkumbukaye mnyonge, BWANA atamwokoa siku ya taabu”.
Ayubu 29:12.kwa sababu naliwaokoa maskini aliyenililia, yatima naye na Yule asiyekuwa na mtu wa kumsaidia. 15 Nalikuwa macho kwa kipofu, nalikuwa miguu kwa aliyechechemea. 16.Nalikuwa baba kwa mhitaji

Sasa jiulize mwenyewe, unawasaidia akina nani kila siku au ni wanyonge gani unaowasaidia, sio kama wale wanaokupigia makofi kwenye uchaguzi wa chama, wanaokutia moyo kwa maovu yako unayoyafurahia, Vipi kuhusu wale wasioweza kuongea kiingereza kuonesha nao ni wasomi, vipi kuhusu wale wasio na tsh 1500 ya kadi ya chama yamkini wagekuja nao wakupigie makofi, vipi kuhusu wale wasio na kipato cha kuwawezesha kupata matibabu, maji, umeme nk. Na kwa jinsi unavyojawa na hekima za dunia hii kujisifu tu maneno yako. Hebu fikiria tena, maneno matupu yanavunja mfupa?

2. Ayubu 29:11 “Maana sikio liliponisikia ndipo likanibarikia na jicho liliponiona likanishuhudia, Jina lako unapenda liwe linatajwa, je unajua jina lako lina tazwaje mitaani? Ni kweliwakati mwingine kwa sababu ya matendo mema na udhatiti wa kiongozi kiutendaji wa haki kuna kuchukiwa na watenda wabaya, inakuwaje sasa wewe unachukiwa na wapenda haki! Je unafurahia kejeli, unafurahia matusi japo hayakufikii moja kwa moja, unajisikia raha vijana wanapokukiri “hana maana huyo”.

Hebu jifikirieni vizuri na kauli kama hizi zinazotamkwa mitaani bila kuogopa ziwaume; eti “Mmeonesha ukomavu kutoka kwenye shingo kwenda chini na sio juu.” (kejeli ya hali ya juu sana hii). Nilidhani mngeshtuka cha ajabu bado mmeendeleza utamaduni wenu wa kupigiana makofi. Mungu atusaidie sana.!

3. Ayub 29:21. Anasema “Watu walitega masikio kunisikiliza na kungoja, wakanyamaa kimya wapate sikia mashauri yangu. 22.Hawakunena tena baada ya kusikia maneno yangu, matamko yangu yakadondoka juu yao. 23.Walikuwa wakiningojea kama kungojea mvua. Wakafunua vinywa vyao kama mvua ya masika”.
Mwanzo watu walikuamini wakaamua uwaongoze lakini sasa kwa muda mrefu watu wamekuwa wakikulalamikia wewe, mara ya kwanza, oooh watu hawa hawajui tuu.! Mara ya pili, oooh watu hawa hawajasoma…! Mara ya tatu, kuna watu wakorofi wanataka kuvunja Amani ndio wanaowachochea. Swali langu; Kwa nini wewe tu? Je wewe ni mkamilifu kwa makosa? Au wewe ukikosea hautakiwi kuambiwa?
Siku zote mtu akisema umenikanya, usimwambie nyamaza, mwambie pole, wapi umeumia na kama kaumia sana unachukua hatua. Lakini sasa hali ilivyo kwa viongozi wetu waliowengi ni balaa, Mungu atusaidie sana!
Kwa sababu ya hekima za mtumishi Ayubu alisikilizwa sana na kwa hamu kweli kweli, ukisoma Mith 15:2 mwandishi anasema “Ulimi wa mwenye hekima hutamka maarifa vizuri, bali vinywa vya wapumbavu humwaga upumbavu” sasa hebu wale mlioviongozi wetu hekima mlizonazo mnazitoa wapi, japo si wote lakini wale wengi wao. Kwa kweli hebu mjipime wenyewwe mjue mna uzito kiasi gani.

4. Ayubu anasema “Niliwachagulia njia, nikakaa kama mkuu wao…” (Ayubu 29:25) ndugu yangu usichoke, endelea kujihoji tu; Watu walipoamua au kukubali uwaongoze wewe kama kiongozi ni njia ya aina gani uliwachagulia watu wako? Na kama njia hiyo ilikuwa nzuri kwa nini maisha yao yanaendelea kuwa magumu zaidi kitu kinachosababisha malalamiko yao. Sasa jamii haijizuwii tena kwako kama kiongozi, wenyewe wanasema hivi “Kama ni kweli uwezo wake wa kufikiri ulikomea hapo na akaona uamzi huo uko sahihi basi tumpigie makofi”, ni kwa sababu tuu ya maamuzi yako. (ni kauli ya kejeli kwelikweli, kwa nini haikuumi na ubadilike utendaji wako?)
Mungu awasaidie HEKIMA na maarifa ndugu zangu kwa kweli.

BAADA YA KUTAMBUA MISINGI YA UZURI WA KIONGOZI NIMALIZIE KWA KUSEMA;
MYAZINGATIE HAYA;

• ZITAMBUENI HEKIMA/ MAARIFA SAHIHI
1Korintho 2:6-7 Inasema “Walakini iko hekima tusemayo kati ya wakamilifu; ila si hekima ya dunia hii, wala ya hao wanaoitawala dunia hii, wanaobatirika; bali twanena hekima ya katika siri, ile hekima iliyofichwa, ambayo Mungu aliiazimu tangu milele kwa utukufu wetu”
1Korintho 3:18 “Mtu asijidanganye mwenyewe; kama mtu akijiona ni mwenye hekima miongoni mwenu katika dunia hii na awe mpumbavu, ilia pate kuwa mwenye hekima. 19 Maana hekima ya dunia hii ni upuuzi mbele za Mungu 20.Na tena BWANA anajua anayafahamu mawazo ya wenye hekima ya kwamba ni ubatili.”

• ITAFUTENI NA KUSHIKA HEKIMA PAMOJA NA MASHAURI.
Mith 19:2 Inasema “Tena si vizuri nafsi ya mtu ikose maarifa/hekima…..”! Ayubu 28:12 anahoji kuwa hekima na ufahamu vinatoka wapi? Anajibu mwenyewe Ayubu tena kuwa hekima na ufahamu vinatoka kwa Mungu (Ayub 28:28)
Muh 2:14 Anasema “Macho ya mwenye hekima yapo kichwani”. Hapa elewa vizuri kwa maana ya uongoozi/utawala; Uongozi/utawala mzuri unategemea sana na weredi wa kihekima wa kiongozi mwenyewe aliye madarakani.
Lakini pia sote tujue kuwa viongozi wakishaurilwa vizuri taifa linajengwa vizuri sana, rejea Mith 11:14 “Pasipo mashauri taifa huanguka, bali kwa wingi wa washauri huja wokovu”

• OGOPENI UDHALIMU NA HILA
“Kupata akiba ya mali kwaulimi wa uongo, Ni moshi upeperushwao, ni kutafuta mauti 7.Jeuri ya wabaya itawaondolea mbali, kwa sababu wamekataa kutenda hukumu”. Mith 21:6
“Ole wako wewe uharibuye ila hukuharibiwa, utendaye hila wala hukutendwa hila! Utakapokwisha kuharibu utaharibiwa wewe; na utakapokwisha kutenda kwa hila, wao watakutenda hila wewe”. Isaya 33:1

Ukiwa kiongozi kuwa makini na washauri wako pia, soma Mith 13:20 Enenda na wenye hekima nawe utakuwa na hekima, bali rafiki wa wapumbavu ataumia

• MTUMAINIE MUNGU.
Kumtumania Mungu ni pamoja na kuishi maisha yenye hofu ya kimungu kwa matendo na sio kwa kuhudhuria tu kwenye nyumba za ibada. Kama unavyojua siku zote uovu hututenga na Mungu; Isaya 59:1 Uovu umetutenga na Mungu. Lakini mwandishi anasema Zab 40:4 Heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake, wala hakuwaelekea wenye kiburi, wala hao wanaogeukia uongo
Pia kiongozi akumbuke kuomba msamaha pale anapokosea maana ni ubinadamu kukosea na Mungu atakufanya kuwa nyota inayong’aa ndani ya jamii unayoiongozoa. (Kuomba msamaha soma Zab 25)

• KWA WASIO VIONGOZI
Ukisoma Marko 2:15-17 Yesu alipokuwa ameketi na watoza ushuru na wenye dhambi, alipoulizwa kwa nini ameketi na wenye dhambi akasema mwenye Afya hahitaji tabibu; naomba unielewe vizuri hapa, simaanishi kuwa viongozi ninaowazungumzia wana dhambi kwa maana mwenye kuhukumu hivyo ni Mungu tu na haturuhusiwi kuhukumu, bali yako makosa wanayoyafanya na yanaonekana kwa macho haya ndiyo ninayoyazungumzia. Sasa ndugu zangu juu ya haya wewe unayeyaelewa maandishi haya mimi ninaomba watu mnapokuwa karibu na hao, msemezane nao kwa upole, kwa lugha ya ushawishi kuwaonesha kuwa wanachokifanya sio kizuri. Haviipendezi jamii zaidi havimpendezi Mungu. Na Mungu atusaidie sana.!

BIBLIA INASEMA; WABARIKINI WANAOWAUDHI; BARIKINI, WALA MSILAANI (Rum 12:14)
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi viongozi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye, macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo.

MWISHO NISEME HAYA KWA AJILI YAKO;

MUNGU AKUBARIKI SANA MSOMAJI,
MUNGU AWABARIKI SANA NA KUWAONGOZA VIONGOZI WETU,
MKONO WAKE MKUU WA ULINZI UWE PAMOJA NAO,
JAMII YETU IKABARIKIWE NA BARAKA ZOTE ZA MUNGU WA MUNGU ALIYE BABA YETU.
JAMII YETU IWE YENYE AMANI NA FURAHA PIA DAIMA.

:: KATIKA KRISTO; Vicent Mwengo
August 2013.

Comments