Tahadhari imetolewa kwa wale wote wanaoifanyia biashara karama ya Mungu
kwa kutoza watu pesa ili waombewe kwa Mungu ili matatizo yao yaishe,
kwani huo ni ukengeufu wa imani na maadili.
Hayo yamesemwa na mwangalizi mkuu wa WAPO Mission International askofu
Sylvester Gamanywa wakati akifundisha katika mwendelezo wa operesheni
takasika inayoendelea jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa BCIC Mbezi
beach.
Askofu Gamanywa amewataka watu wanaotozwa pesa na watu hao ili wafanyiwe
maombi ni bora wazinduke sasa kwani karama za Mungu yakiwemo maombezi
hayauzwi kwa bei yeyote, bali ni bure, na wajue kuwa wanaofanya hivyo ni
washirikina.
"Kila muhubiri yeyote anayetoza fedha katika huduma za rohoni anafanya hivyo kwa roho ya uchawi na ushirikina", anasema askofu Gamanywa na kuongeza;
"hata kama ananukuu maandiko katika Biblia lakini kuifanyia biashara
karama ya Mungu ni pale fedha inapotumiwa kama kishawishi kwa mtu ambaye
anashida na uponyaji na muujiza kutoka kwa Mungu, pesa inatangulizwa
kama kishawishi kwamba akitoa fedha hiyo basi Mungu ataona kile
alichotoa ndipo amponye ndipo amtendee muujiza huo ndio ushirikina
ninaousema", alimaliza kusema askofu Gamanywa.
Aidha ameendelea kusema kwamba ameyasema yote hayo si kwasababu anataka
kumfurahisha mtu bali anasema kutokana na ukengeufu ulioingia katika
kanisa na hakuna anayekemea na watu wanafikiri ndivyo ilivyo. Amewaambia
vijana kwamba katika yote hayo yanayotokea suluhisho ni kumpokea kutubu
na kukubali kuwa Yesu ni Bwana na Mwokozi wao ili Roho Mtakatifu
achukue nafasi ya kuwaongoza.
chanzo:Gospel Kitaa
Comments