USINGIZI WA KIROHO * sehemu ya tano *

Na mtumishi Gasper Madumla


Bwana Yesu asifiwe…
Karibu tuendelee…

...katika maisha yetu ya kila siku,yeye shetani hutujia kama malaika wa nuru ili kusudi tusije tukamtambua kwa wepesi.
Lakini katika ujio wake ibilisi,
mkononi mwake amebeba kitu kilichokuwa ni kiovu kwa lengo la kukubadilishia kwa kile kizuri ulichopokea kwa Bwana pindi utakapo kuwa umelala kiroho.

*Mara zote shetani hupanga ratiba yake ambayo ni ratiba yenye uharibifu na ni ratiba ambayo huwa kinyume kabisa na ratiba ya Mungu .Yeye adui amepanga akupotoshe ili umuache BWANA MUNGU wako endapo utalala kiroho.

*Watu wengi bado hawajagundua siri hii,
kwamba,
shetani anaweza kukupa hata mafanikio ya kiuchumi ya muda mfupi pasipo kujijua kwa wewe uliyelala usingizi wa kiroho.

Tazama ;
kweli ulikuwa unataka ufanikiwe kiuchumi kwa njia ya ki-Mungu,
Lakini ukajisahau kukesha na Bwana,
Sasa gafla unajikuta unafanikiwa pasipo hata kutegemea na unaona kuwa hakuna haja ya Mungu tena,

Kumbuka hayo mafanikio yanakuja na ratiba zake ibilisi ambazo hazikupi muda wowote ule wa kumtukuza Mungu.
Hii yote ni kukufanya umsahau Mungu wako,na ukose ufalme wa Mungu. Lakini katika hayo mafanikio ya muda,
ujue,
huyo shetani ataitaka roho yako mikononi mwako,sababu yeye ni mchinjaji tu siku zote.

*Na ndio maana mimi nina mfananisha shetani kama mfuga kuku,
ambaye mara zote huwaangaikia kuku wake kwa kuwapa mahitaji yote,
kuhakikisha wanafurahi kwa kitambo tu,
Lakini nakuambia ipo siku mfuga kuku ana mkamata kuku na kwenda kumchinja hadharani,

na hata kama kuku huyo akilia sana kwamba “ mbona rafiki yangu unanichinja leo ?”
Lakini mfuga kuku hatajali hicho kilio chake bali atahakikisha ni lazima anamchinja tu,Kumbuka huyo ni kuku ambaye alipewa mahitaji na kupendeza kwa muda.

-Na hivi ndivyo hali ilivyo kwa shetani,
jinsi anavyoweza kukupa mambo ya kidunia kwa hali na mali,tena anaubadilisha ufahamu wako ambao utakufanya wewe usigundue chochote kile,
maana umelala kiroho.

-Katika mambo yote akupayo,kweli yataonekana ni mazuri kwa macho ya damu na nyama,Lakini ninakuambia ipo siku shetani atakuchinja tu kama kwa habari ya mfuga kuku.

• Mkristo ambaye amejisahau akalala kiroho,ujue ni lazima atajikuta yupo ndani ya ratiba ya shetani,
na kumbuka hii mpendwa ;

• Shetani akikupangia ratiba yake ni lazima utaifanya tu.Hukikwepa kuifanya kazi ya Mungu ujue utaifanya kazi ya shetani.

*Kati ya vitu vibaya katika maisha yetu ya kiimani ni KULALA USINGIZI WA KIROHO.
Sababu pindi ulalapo ujue adui yeye halali,bali huzunguka-zunguka akitafuta mtu ammeze

Biblia inatuambia ;
“ Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi,
kama simba angurumaye,
huzunguka-zunguka,
akitafuta mtu ammeze.” 1 Petro 5:8
( Be sober, be vigilant; because your adversary the devil walks about like a roaring lion, seeking whom he may devour.)NKJV

*Biblia inatuambia kwamba tuwe na kiasi na KUKESHA.
Yaani tunaambiwa tuwe macho kiroho,
tusilale kiroho,
maana ikiwa kama tutajisahau na kulala kiroho basi yupo ibilisi naye atatumeza.

*Mshitaki wetu ibilisdi yeye hana jipya sababu yeye ni marehemu tayari,bali alichonacho ni KUKUBADILISHIA KILE KIZURI KWA KIBAYA PALE UTAKAPOLALA KIROHO.

Neno la Mungu lilitufundisha sana katika fundisho lililopita juu ya habari ya NGANO na MAGUGU.(soma fundisho lililopita)

Mathayo 13:25-26
“ LAKINI WATU WALIPOLALA, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake.
Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu.”

*Sisi binadamu tulikusudiwa tuishi maisha ya kumpendeza Mungu wetu,maana tulifananishwa na mfano wa NGANO/WANA WA UFALME.Lakini iweje basi leo ,
watu wamekuwa ni upande wa shetani?
Na kumuacha Mungu wao aliyewaumba katika uzuri kabisa.

*Hii inatuonesha kwamba upo mbadilishano wa kiroho pale tulipokuwa tumelala.

Tazama hali ilivyo katika maisha ya NDOA
-Ndoa nyingi leo zimekosa watoto,
zina mafarakano,
yaani mume anamuona mke wake kama mnyama au kinyago fulani hivi ambacho hakina heshima yoyote ile,
Kwa kifupi hakuna PENDO lolote lile.

*Sasa unisikilize mpendwa;
Adui amebadilisha NDOA yako,
ameiba kizazi ulichopewa na Mungu Baba pale ulipo lala.yeye amekupa UTASA

-Adui amembadilisha mwenzi wako,na amekupa mtu mwingine kabisa usiyefanana naye katika ulimwengu wa roho.
-Adui amembadilisha Yule ambaye alitakiwa akuoe/umuoe na kisha unajikuta mpaka sasa unayempata kwa kuoa/kuolewa unamuona siyo,kwamba kila mnachopanga,mwisho lazima kivurugike.

Wapo baadhi ya watu wamevikwa mavazi ya kipepo ambayo huwafanya wakose kupendwa.

Mfano ;
katika ndoa unaweza kumuona mkeo hafai kitu,
si mzuri tena,
hana thamani tena machoni pako,N.K pindi uonapo haya yote ujue ULILALA KIROHO KISHA ADUI AKAJA NA KUKUBADILISHIA NA HATA KUVIKA MAVAZI YA KIPEPO.

*Tuige ule mfano wa yule kahaba aliyebadilishiwa mtoto wake kwa kupewa mtoto aliyekufa (1Wafalme 3 :16-27) Yeye alipoamka hasubuhi alikataa yale maelezo ya adui,

*Sasa imefika wakati wa kukataa maelezo ya adui juu ya mbadilisho uliyotokea kwako.Na inawezekana kupata urejesho wako ikiwa una-amini (Wafilipi4:13)…

• Usikose fundisho lijalo,lipo kusudi kwako hata kusoma ujumbe huu,kwa huduma ya maombezi mawasiliano ni 0655 111149

ITAENDELEA…
UBARIKIWE.

Comments