Je, msalaba wa Yesu unamaana gani kwa kanisa la leo ?

Mwl. Sospeter Simon Ndabagoye/ New Elshaddai Ministries NEM-Tanzania.


Msalaba wa Yesu ni ishara ya nguvu ya Mungu itendayo kazi ; Uwezo wa kuishinda dhambi tulionao, asili yake ni nguvu ya msalaba wa Yesu. Uwezo wa kuacha pombe, kuacha sigara, ukahaba,umalaya, ugomvi, wizi, ujambazi,kulipiza kisasi n.k. chanzo chake ni msalaba wa Yesu. Ni kupitia msalaba wa Yesu,wachawi wameacha uchawi wao, walevi wameacha ulevi, wagomvi wameacha ugomvi,waliofungwa na magonjwa wamewekwa huru, watu wamepata pumziko la kweli ndani ya Yesu.
Msalaba wa Yesu ni ishara ya kuwekwa huru ; Yesu alipowekwa msalabani,alibeba mizigo yako yote, usikubali kung’ang’ania mzigo wo wote, mkabidhi Yesu, kama alivyokubali kuchukua mashitaka ya Baraba, akakubali kuwekwa kwenye mti badala yake, hata leo yuko tayari kuchukua mzigo wako ili uwekwe huru. Haiana haja ya kuendelea kujitesa, mkabidhi hati ya mashitaka yako Yesu. Kumbuka Yesu alikuja kwaajili yao waliopotea (Mathayo 9 :13) ili awarejeshe kundini. Usikubali kuendelea kukaa nje ya zizi, njoo leo kwa Yesu uwekwe huru. Kumbuka hati yako alisha iondoa, hukumu yako alishaibeba, kwanini uendelee kukaa gerezani ? kumbuka Yeye mwenyewe(Yesu) alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, …na kwa kuoigwa kwake, mliponywa (1Petro 2 :24).



Mambo gani yalitokea Baada ya Yesu kupandishwa Msalabani ?

Kwanza, Pazia la hekaru lilipasuka ; hii inamaanisha ushindi mkubwa wa mkristo. Pazia kupasuka kunamaanisha kuwekwa huru. Kuondolewa kwa vizuwizi vyote mbele yako.
Ikumbukwe kuwa, pazia, liliwekwa kuwazuwia watu wasiingie wala hata wasiweze kupaona patakatufu pa patakatifu. Mahali hapa,aliingia kuhani peke yake. Baada ya pazia kupasuka, kizuwizi kiliondolewa kwa yeyote kufika hapo. Kifo cha Yesu msalabani, kimeondoa dhambi zako, kimekupa kibali cha kunena kwa lugha kwa raha zako.

Pili, Tetemekeo kubwa; Tetemeko hili,liliambatana na giza nene,ikiwa ni ishara ya nguvu kubwa yenye utisho wa ajabu sana. Tetemeko hili, lilionesha uwezo ulio juu ya uwezo wote,nguvu inayozidi nguvu zote. tetemeko hili, lilidhihirisha kuwa kweli Yesu ni mwana wa Mungu, na yule mlinzi alishuhudia kwa kinywa chake. Hata leo, maisha ya mtu aliyeokoka, yanapaswa kudhihirika mbele za watu wote, kuwa kweli kuna nguvu mpya na uweza wa ziada ndani ya mtu aliyeokoka.

Tatu, Makabuli yalifunguliwa ; baada ya Yesu kushuka kuzimu, walio lala, wote wakaamka, wakatangaziwa uzima upya. Wakawa katika uzima wa milele pamoja na Yesu ; baada ya Yesu kumnyang’anya funguo za kuzimu ibilisi, akawa hana mamlaka tena, uwezo wake wote na mamlaka yote akawa amenyeng’anywa. Nguvu ya msalaba, ni nguvu inayoshinda mauti. Yesu ni zaidi ya mateso yote, ni zaidi ya kifo, ni zaidi ya magonjwa, ni zaidi ya kukata tamaa, ni zaidi ya umasikini, nguvu ya msalaba iko juu ya laana na vifungo vyote.

Nne, Tamko la Ushindi likatolewa ; tamko la ushindi lilitolewa rasmi Yesu aliposema (Imekwisha). Kauli ya Yesu iliashilia kufikia mwisho kwa mateso yote, uonevu, laana, mikosi na vifungo vyote. Kauli ya Yesu inatufundisha nini aliposema Imekwisha? Kwa mtazamo wa ndani zaidi, ilimaanisha, kukamiliaka kwa kazi yake iliyomleta duniani ambayo ilikuwa ni ukombozi. Kumweka huru kila mtu ili asipotee, bali awe na uzima wa milele. Kwa maelezo mengine tuseme kuwa, Msalaba wa Yesu, ulibadirisha Historia ya Ulimwengu wote na kuweka utamaduni mpya.

Tano, Msamaha wa dhambi ulitolewa; kupitia mauti ya msalaba wa Yesu, msamaha wa dunia ulitangazwa. Kupitia kifo cha msalaba, toba kwa ulimwengu ilipatikana. Kifo cha msalabani, kinatupa maji ya uzima, kinatupa pumziko la kweli, kina tuhesabia haki. Wakati wayahudi walidhani wanakomesha, kumbe agano la Mungu linatimia kwa ulimwengu, kuwa Mtu hatafika mbinguni ila kwa njia ya Yesu Kristo. Kupitia kifo cha Yesu, mlango wa kuiendea mbingu ilifunguliwa wazi kwa wote wampokeao na makao yao yakaanza kuandaliwa tangu hapo. Hata leo, ukiokoka, makao yako yanaanza kuandaliwa leo.

MAOMBI
Ndugu yangu, natumai umesoma ujumbe huu, leo Roho wa Mungu amenituma kwako, nikuueleze habari hii ya Msalaba, sijui umeteseka kwa kiwango gani katika hali hiyo uliyonayo, wala sijui hamu yako ya kumtumikia Mungu inalinganaje, wala sifahamu umesongwa kwa kiwango gani, pengine umefikia hatua ya kukata tamaa, huoni msaada utatoka wapi, lakini ujumbe huu umefika kwako muda huu; upo msaada usioisha,upo uweza usioshindwa, ipo nguvu isiyoteteleka, nayo ni nguvu ya Msalaba wa Yesu Kristo, aliye chukua laana na uovu wetu ili tupate kuwa huru. Aliyechukua dhambi zetu, aliyebeba magonjwa yetu, huzuni zetu na kila adha; unapo pata habari hizi, nakusihi sana usikubali kuendelea kukaa katika vifungo hivyo, toka gerezani, Mungu amekukumbuka, amekuona,usifanye moyo wako kuwa mgumu, jiachilie kwake uwe huru, kwa Jina la Yesu Kristo. Pokea kwa kadri ya uhitaji wako, unayetaka mwenza, unayetaka mtoto, unayetaka kuinuliwa katika masomo, usiye na kazi, unayeteswa na madeni, kila kona unavutwa shati, kwa Jina la Yesu, unayeonewa kazini kwako, umeshushwa cheo, umeonewa vya kutosha, kwa Jina la Yesu, pokea uweza mpya na nguvu mpya. Uwe huru sasa, ufurahi tena, ububujike amani tele moyoni, kwa Jina la Yesu Kristo.

Kama unahitaji kuokoka, au ungependa kupata ushauri wowote maombezi au kutoa ushuhuda, wasiliana na

Mwl. Sospeter Simon Ndabagoye/ New Elshaddai Ministries NEM-Tanzania.
Kwa Mobile +255(0)7 (57/84) 464 141/ 12 909 021.
Au Email sos.sesi@yahoo.com / newelshaddai@gmail.com
Tunakushauri, utembelee kanisa la kiroho lililo jirani yako, kwaajili ya mafundisho zaidi na Ushirika. (Kumbukumbu la Torati 28:6)

.

Comments