KUISHI SAWASAWA NA NDOTO YAKO (LIVE YOUR DREAM)

Na Mch. Josephat Gwajima, Ufufuo na uzima, Kawe, Dar es salaam

Utangulizi:
Biblia imetaja sana kwa habari ya ndoto, ukisoma katika kitabu cha Mwanzo pekee, neno “ndoto ” limeandikwa zaidi ya mara 36. Pia, katika kitabu cha Daniel neno ndoto limeandikwa zaidi ya mara 29. Na ndio maana Mungu alipotaka watu wake wajenge ama madhabahu au hekelu aliwaonyesha kwanza katika ndoto; kumbe ujenzi wowote huanzia katika kuona. Vivyo hivyo hata watu wanaomtegemea shetani huingia ulimwengu wa roho na kujenga kile walichokiona kutoka kwa shetani.

TABIA YA MUNGU KATIKA NDOTO:
Kutoka 25:8-9; Mungu akitaka ujenge anaanza kukuonyesha; ndio maana alimwonyesha pia na Musa na kumtaka ajenge sawa sawa na alichomwonyesha “exactly like the pattern I will show you” Kutoka 25:37-40; Hii ni tabia ya Mungu kuwaonyesha watu kupitia ndoto na watu wengi pasipo kujua wamejikuta wakidharau ndoto.

Ukisoma katika kitabu cha Habakuki 2:2-3; Mungu alimwamuru Habakuki aiandike ile ndoto; kwasababu asingeweza kufanya kuona kwanza katika ulimwengu wa roho. Na ndio maana neno ndoto limeandikwa mara nyingi katika kitabu cha Mwanzo kwasababu hicho ndicho kitabu cha asili (origin). Hiyo inatufundisha kuwa mwanzo wa vitu huanzia katika ndoto.
Mambo ambayo Mungu anaweza kuyafanya kupitia ndoto:
i) Mungu anaweza kufumbua mafumbo kupitia ndoto:-
Mwanzo 40: 2-19; Hapa tunaona kwa habari ya mwokaji na mwoshaji wa Farao ambao walipata kujua hatari iliyokuwa imejificha kwa njia ya ndoto. Kwa njia hiyo wote wawili wakajua maisha yao siku tatu mbele. Kumbe ndoto yaweza kukufunulia mitego au hatari iliyojificha au kupangwa na watu wabaya.

Farao alikwisha kupanga kuwa siku ya tatu itakuwa hukumu yao lakini bila kuwambia; lakini waliweza kufunuliwa katika ndoto. Ni maombi yangu kuwa Mungu na akuonyeshe hatari zote ulizopangiwa sirini.

ii) Mungu anaweza kukurudisha au kukurudishia ulichokipoteza:-
Katika kitabu cha Danieli pekee, neno “ndoto” limeandikwa zaidi ya mara 29; Danieli alikuwa uhamishoni Babeli; akiwa huko Mungu akamwonyesha kwa habari ya kumrudisha mahali pake. Vivyo hivyo katika maisha yako inawezekana ulikuwa na mafanikio lakini sasa hayapo; au ulikuwa na afya nzuri lakini sasa haipo; katika ndoto Mungu aweza kukurudisha sehemu unayotakiwa kuwapo.

Na ndio maana kila siku huwa nasema Tanzania mpya niliyoiona katika ndoto inakuja; Tanzania yenye maendeleo; yenye hospitali nzuri, yenye gesi, Tanzania yenye madini inakuja na sifi leo ama kesho mpaka ndoto itimie.

Ni maombi yangu Mungu akurudishie ile hatma njema ya maisha yako ambayo shetani aliichukua katika maisha yako.

iii) Ndoto zinaweza kukuonya:-
Ndoto zaweza kukuonya usichukue maamuzi ambayo sio sahihi, uache tabia mbaya ambayo ina mwisho mbaya. Mathayo 2: 13-16; Baada ya Herode kugundua kuwa amedhihakiwa na mamajusi akaamua kuua watoto ili amwangamize Yesu; lakini Yusufu akapewa onyo na Mungu kuwa ampeleke mtoto Misri. Ni kweli Herode aliangamiza lakini walioangamizwa ni wale ambao baba na mama zao hawakuota ndoto.

Hapa tunaona athari moja ya kutoota ndoto, maana madhara yake yaliwahi kugharimu maisha ya watoto wao. Kupitia ndoto Yesu aliokolewa, Mungu huongea pia kupitia ndoto. Ndio maana ni muhimu kumwomba Mungu akupe ndoto ya kuokoa familia au ukoo wako.

iv) Mungu anaweza kutufariji katika ndoto:-
Katika maisha unaweza kupitia wakati mgumu, umezungukwa na madeni au kukata tamaa lakini Kupitia ndoto Mungu aweza kukuonyesha utakuwa nani baadaye. Kwa njia hii Yusufu alifarijiwa kupitia ndoto; kwa njia hiyo Yusufu alipokea faraja na kuhakikishiwa ushindi.

Yusufu alipoota ndoto zilisababisha achukiwe na ndugu zake, na wakamtupa shimoni na baadaye kumuuza Misri lakini ndoto yake ilibaki palepale. Haikutosha hapo, bali alisingiziwa ametaka kumbaka mke wa waziri mkuu wa Misri na akaja kufungwa. Lakini katika mateso yake Mungu alikuja kumfariji kupitia ndoto na kumrudisha katika nafasi yake.

Vivyo hivyo katika maisha yako inawezekana ulisingiziwa na kupoteza nafasi ambayo Mungu alikupa; leo kila aliyekunyang’anya nafasi naamuru uchukue nafasi yake; nafasi ya ndoa, nafasi ya umeneja, nafasi ya uongozi ninaiamuru irudi kwako katika jina la Yesu Kristo. Yule Yule aliyekupiga vita mwaka jana mwaka huu utachukua nafasi yake katika jina la Yesu.

Kutoka katika ufungwa gerezeni hadi kuwa mkuu katika nchi ya Misri, yote hii ilianza katika ndoto. Kumbuka ndoto za Yusufu zilianza alipokuwa na miaka 16 lakini alikuja kuimiliki akiwa na miaka 40. Tatizo la watu wengi wanakata tamaa mapema; hutakiwi kufa moyo, hapo katikati wakati unaisubiria ndoto unaweza ukapitia mateso na mabonde lakini ndoto itakuja na itatimia usipozimia moyo.

v) Mungu aweza kukuonyesha utakuwa nani baadaye katika ndoto:-
Mungu hutenda kazi tofauti na sisi tunavyowaza; Yule mtu unayemuona mdhaifu ndiye ambaye Mungu anamuona shujaa; vivyo hivyo kwa habari ya Yesu, yeye alizaliwa katika hema ya ng’ombe; Samweli alizaliwa na Hana ambaye alikuwa hazai hapo mwanzo; Musa naye alitupwa kwenye mto akakulia kwa baba wa kambo; Samson alizaliwa na mama ambaye alikuwa tasa hapo mwanzo; na ndio maana hata siku moja usidharau mambo madogo kwasababu ndiyo ambayo Mungu huyatumia.
vi) Mungu anaweza kutuonyesha ushindi juu ya adui zetu katika ndoto:-
vii) Mungu aweza kukuonyesha adui zako katika ndoto:-
Kila mtu ana adui wa maisha wake; awe rais, waziri, mchungaji, au askofu lazima utakuwa na adui wa maisha yako. Yaani kwa kila hatua unayopiga unatengeneza marafiki na adui wengi kwasababu hiyo kila mtu ana adui zake. Lakini Mungu anaweza kukuonyesha ushindi wako katika ndoto. Ukisoma katika kitabu cha Waamuzi utaona kwa habari za Gideoni ambaye alitakiwa kupigana na Wamidiani; lakini kabla ya kwenda vitani Mungu akatumia ndoto kumwonyesha ushindi unaokuja mbele.

Ni maombi yangu Mungu akuonyeshe ushindi juu ya adui zako katika jina la Yesu Kristo. Kumbe kupitia ndoto unaweza kuonyeshwa adui ambaye hapendi mafanikio yako yaani Mungu akupe ushindi dhidi ya hila zake mbaya katika Jina la Yesu.

NDOTO:
Sikumoja nilikuwa nasafari kutoka nchi moja kwenda nyingine, nikakata tiketi ya kusafiri kesho yake; usiku wake nikiwa nimelala nikaota ndoto nipo ndani ya lile basi ghafla nikajiona nipo ndani ya basi na likawa linakwenda; gari likiwa linaendelea kwenda kulikuwa na mzigo juu ya siti niliyokuwa nimekaa ghafla mzigo ule ukaniangukia na kila nilipojaribu kuinuka nikashindwa ghafla gari likaanguka alafu nikashtuka kutoka ndoto.

Nilipoamka nikaanza kuomba kwa bidii na kwa muda mrefu kufika kituoni nikakuta gari limeshaniacha; basi nikaomba kusafiri na gari linalofuata la kampuni hiyo. Cha ajabu tukawa tunafuatana na hilo gari ambalo nilitakiwa nipande mimi; mbele ya macho yangu nikaona gari lile limepata ajali mbaya na moyoni nikasikia niende kuangalia katika ile siti niliyotakiwa kukakaa; ndipo nikakuta Yule mtu amepondwa na jeki iliyokuwa ndani ya begi.

viii) Mungu anawezakukuonyesha jinsi ya kumtendea mtu katika ndoto:-
Kupitia ndoto Mungu anaweza kukuonya juu ya uamuzi mbaya unaotaka kuuchukua juu ya mtu fulani katika ndoto; hii tunaiona kwa habari ya Yesu ambapo mkewe pilato alionywa katika ndoto juu ya hatua alizotaka kuchukua Pilato juu ya hukumu ya Yesu. Kumbe Mungu aweza kumuonya mtu juu ya uamuzi mbaya ambao waweza kumgharimu mtu huyo kupitia ndoto.

Mungu anaweza kukuonya juu ya uamuzi unaotaka kuchukua juu ya mtu wakati wa hasira, wakati wa uoga au wakati mgumu. Mungu huonya kupitia ndoto na ndio maana ni muhimu kutokufanya maamuzi yoyote wakati wa hasira; hofu; wakati mgumu kwasababu unaweza kujikuta unafanya maamuzi ambayo sio sahihi. Watu wengi wamevunja mahusiano mazuri na watu kwasababu ya maamuzi mabaya lakini kupitia ndoto Mungu aweza kukuonya na kukuonyesha njia ya kufanya.

NINI CHA KUFANYA UNAPOOTA NDOTO:
- Baada ya kuota ndoto ambayo si nzuri unatakiwa usimame kinyume katika maombi. Sambaratisha ndoto zote na wasimamizi wake wote katika ulimwengu wa roho.

- Na ikitokea umeota ndoto nzuri unatakiwa uiteke na kuimiliki ndoto hiyo; kushindwa kuchukua hatua kutakufanya usiimiliki hiyo ndoto. Ukiota umefanikiwa katika biashara fulani, unatakiwa uanze kwa kuomba halafu chukua hatua ya kuimiliki ndoto hiyo.

- Ukiota ndoto halafu huilewi ni nzuri au mbaya unatakiwa uamuru katika maombi kuwa kama ndoto hii ni mbaya ninaisambaratisha katika jina la Yesu na kama ndoto hii ni nzuri imiliki katika jina la Yesu.

Comments