KUWA UPANDE WA WENYE NGUVU

Mwl. Sospeter Simon Ndabagoye/ New Elshaddai Ministries NEM-Tanzania.

Ndugu msomaji wangu, BWANA YESU asifiwe sana; Napenda kwa heshima kubwa kwa Mungu wetu(YEHOVA) nikukaribishe katika kujifunza maneno matakatifu ya Mungu. Ndugu yangu mpendwa, pasipo na shaka, umekuwa ukijiuliza kila mara, kama leo ndiyo ingekuwa siku ya mwisho, je, Mungu angekukuta katika kundi gani, ni kundi la walegevu au kundi la wenye nguvu? Pengine swali hilo,kwa pamoja tunaweza tusiapate jibu, kwani hata mimi kwa nafsi yangu, inawezekana nikapata au nisipate jibu moja.
Katika somo letu la leo, tutajifunza kwa kuwaangalia wana wa Israeli, katika safari yao ya kutoka Misri, kwenye mateso, kwenye utumwa na adha,kuelekea Kanaani, nchi ya ahadi waliyopewa na Mungu, safari iliyochukua miongo minne, katika kuikamilisha kwao. Kijiografia, safari la kutoka Misri hadi Kaanani, pengine isingechukua hata siku mbili au tatu, lakini hakika, ilichukua miaka Arobaini. Maana yake ni kuwa, mtoto aliyezaliwa siku safari inaanza, alifika akiwa na umri wa miaka 40, kama ni wa kiume basi alikuwa ni mtu mwenye familia tayari, na kama ni wa kike, alikuwa ni mtu amabaye ana watoto tayari.
Katiaka mwaka wa Thelathini na tisa, wakiwa mwishoni kabisa mwa kumaliza safari yao, Mungu akaongea na Musa, namna ya kuiingia nchi ya ahadi Kanaani.
“Kisha Bwana akanena na Musa,akamwambia,Tuma watu waende wakaipeleleze nchi ya Kanaani, niwapayo mwana wa Israeli; katika kabila ya baba zao, mtutamtuma mtu mmoja,kila mtu na awe mkuu kati yao” (HESABU 13:1-2).
Misitari hiyo, inatupa picha kuwa, katika makabila 12 ya wana wa Israeli, ilipaswa, kila kabila litoe mwakilishi mmoja tu, yule mwenye nguvu, yule ambaye yuko mbele kwa wenzake!mwenye ushawishi. Mungu alikuwa na maana gani hapa? Mungu alitaka, waende watu, ambao watakaporudi,majibu watakayotoa,yaweze kuwaridhisha walio baki, na yawe ya kuaminika,kwakuwa yanatolewa na watu wakuaminika-Haleleuya!
Je, kipi kilifuata? Fuatana nami
Msitari wa 17 hadi 20” Musa akawapeleka ili waipeleleze nchi ya Kanaani,akawambia,Pandeni sasa katika Negebu mkapande milimani, mkaitazame nchi ni ya namna gani; na watu wanaokaa ndani yake, kwamba ni hodari au dhaifu,kwamba niwachache au wengi, na nchi wanayokaa kwamba ni njema au mbaya,kwamba wanakaa katika matuo au ngome, nayo nchi niyanamna gani, kwamba ni nchi ya unono au ya njaa,kwamba ina msitu au sivyo. Iweni na maoyo mkuu mkayalete matunda ya nchi. Basi wakati ule ulikuwa ni wakati wa kuiva zabibu za kwanza”
Tunang’amua kuwa, Musa, alitoa maelekezo juu ya kile cha kufanya, kwanza kabisa, aliwapa kazi ya kwenda kuchunguza ni nchi ya namna gani, na watu wake ni wa namna gani? Na maisha yao yakoje, ni ya kudumu au ni ya kuhama hama? Majibu juu ya upelelezi huu, ulitegemewa sana, kwa Musa, na wanaisraeli wote, ambao kwa kipindi kirefu, walikuwa wametembue jangwani, kwa miaka yote. Pengine, watoto walizaliwa njiani, na walikuwa wameshakuwa watu wazima tayari, na wengine walishakufa kabisa. Fikiria kama, ni ulimwengu wa leo, si angelikuwa alishauwawa Musa zamani tu?
Matokeo ya upelelezi wao yalikuwaje? Shughuli hii, ilichukua siku arobaini,yaani mwezi mmoja mzima na siku kumi au tisa hivi. Na majibu yalikuwa ndiyo
“Wakarejea baada ya kuipeleleza nchi, mwisho wa siku arobaini. Wakaenda wakafika kwa Musa, na kwa Haruni na kwa wana wa Israeli katiaka jangwa la Parani,...Wakasema” tuliona nchi ile uliyotutuma” na hakika yake, ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali, na haya ndiyo matunda yake(Hesabu 13:25-).
Lakini watu wanaokaa katika nchi ile ni hodari, na miji yao ina maboma nayo ni makubwa Sana....(30-33)
Kwa mtazamo huu, tunapata kujua kuwa, majibu yaliyokuja, yalikuwa yanasigana. Kutokana na uchunguzi wao, kuna kundi la watu,tena walio wengi, lililokuja likisema, kuwa, watu wa nchi ile, wana nguvu sana, na hata kuingia kwenye nchi yao, haiwezekani!ni heri warudi Misri utumwani tu. Baada ya makutano kupata taarifa hiyo, wote wakalia sana, na kumlaumu Musa na Haruni, kwa kuwa wamewataabisha muda mrefu sana, bila mafanikio yoyote.
Baada ya ghadhabu kuwa kubwa, na majonzi makuu kutandana ndani yao, wakaona ni vema,hata wawapige mawe wafe! Ndipo Yoshua na Kalebu, wakasimama, miongoni mwa wapelelzi kumi na wawili, wao peke yao, wakasimama kwa ujasiri, na kurarua mavazi yao, na kusema, nchi ile ni nzuri, na wanaweza kuiteka, kwakuwa wamehidiwa na Bwana-Haleluya!
Ndugu yangu mpendwa, haijalishi wanaokuunga mkono ni wangapi, au walioko upande wako ni wa ngapi? Wewe simamia ukweli tu, utashinda!Hutateteleka hata siku moja. Biblia, inatueleza hayo katika sura ya 14 kuanzia msitari wa kwanza; ....wala msiwaogope wale watu,maana wao ni chakula kwetu, uvuli uliokuwa juu yao,umeondolewa,naye BWANA yu pamoja nasi, msiwaogope. (Hesabu 14:9).
Na hapa, tunaona wakipata ari ya kusonga mbele! Tunoana wakitiwa moyo, japo kundi kubwa,makabila kumi yote, yalikuwa tayari kurudi Misri, tunaona, sasa, wakianza kugawanyika vipande vipande na kungana na akina Yoshua na Kalebu.
Ndugu yangu, ndoa yako, haihitaji watu wengi sana waiunge mkono, wala masomo yako,wala biashara yako,bali, Bwana. Kufaulu kwako, hakumtegemei mwanadamu, bali kunamtegemea Mungu. Haijalishi wangapi wanakusema vibaya, wala haijalishi ni vikwazo gani unavyokutana navyo, ila lazima ujue kuwa, ahadi za Bwana maishani mwako, lazima atazitimiza. Usishitushwe na uamati, unaoshangilia upande uliokinyume na wewe, wee iangalie ahadi ya Bwana, kwa jicho la suhindi, nawe utauona Utukufu wa Mungu Maishani Mwako. USIKUBALI KUKAA UPANDE WA MWANADAMU, BALI UWE UPANDE WA MUNGU. Kibiblia, kauli ya wengi wape, haipo, bali wenye imani, watatawala-Haleluya! Usiangalie kuwa jana umeshindwa, bado tumaini lipo, kama si leo, pengine zamu yako ni kwesho, usiseme, nitafanikiwaje,Bwana mwenyewe, atakuelekeza njia utakayopita. Usikubali kukatishwa tamaa kwa vile umengoja sana, au kwakuwa, hauna wateja kwenye Biashara yako, au kwa kuwa huna ndugu wa kukusaidia,ukasema huwezi, hapana, mwangalie Mungu, lazima ahadi zake kwako, atatimizia tu.
Nakutakia Ushindi wa Kristo Maishani mwako. Ameni.

Kama unahitaji kuokoka, au ungependa kupata ushauri wowote maombezi au kutoa ushuhuda, wasiliana na

Mwl. Sospeter Simon Ndabagoye/ New Elshaddai Ministries NEM-Tanzania.
Kwa Mobile +255(0)7 (57/84) 464 141/ 12 909 021.
Au Email sos.sesi@yahoo.com / newelshaddai@gmail.com
Tunakushauri, utembelee kanisa la kiroho lililo jirani yako, kwaajili ya mafundisho zaidi na Ushirika. (Kumbukumbu la Torati 28:6).

Comments