Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC) la Ubungo Kibangu, Anthony
Lusekelo, amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinashinikiza kusainiwa kwa
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013,
ili ipatikane katiba itakayokibeba chama hicho.
Wakati Lusekelo
akieleza hayo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gosper Bibble Fellowship
(FGBF), Zacharia Kakobe, amesema kuwa diwani, mbunge, waziri na rais
haina maana kuwa una mamlaka yote dhidi ya Watanzania.
Kauli za
viongozi hao wa dini, zimekuja katika kipindi ambacho vyama vya siasa,
wanaharakati na wananchi wamekuwa wakimshinikiza Rais Jakaya Kikwete,
kutosaini muswada huo na badala yake, urejeshwe bungeni, ili ukafanyiwe
marekebisho kwa maelezo kuwa una kasoro nyingi.
Akizungumza na
gazeti hili Lusekelo maarufu kama ‘Mzee wa Upako’ alisema CCM inatambua
kuwa mapendekezo yaliyomo katika Rasimu ya Katiba kama yakipita, chama
hicho kitakuwa katika wakati mgumu, hivyo ni lazima kihakikishe kuwa
hatua hiyo inakwama.
“Hiki chama kinaweza hata kung’oka madarakani
kama mapendekezo ya sasa yatapita. Namshauri Rais Kikwete asikilize
malalamiko ya Watanzania kuhusu muswada huu, asisaini na aurudishe
bungeni ili ufanyiwe marekebisho,” alisema na kuongeza kuwa;
Kitendo
cha wabunge wa chama kimoja kuwa wengi katika Bunge la Katiba, Zanzibar
kutokushirikishwa katika utoaji wa maoni na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba kumaliza majukumu yake baada ya kukabidhi rasimu katika Bunge la
Katiba, ni kasoro kubwa zilizoibuliwa na wanasiasa lakini zikapuuzwa.
Mbali
na kuiponda sheria ya mabadiliko ya katiba, Lusekelo alisema lingekuwa
jambo la busara kama Bunge la Katiba lingekuwa na wajumbe ambao sio
wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa upande
wake, Askofu Kakobe wakati akizungumza katika ibada ya misa ya pili
kanisani kwake Mwenge Dar es Salaam, alisema viongozi wa nchi
wamechaguliwa kwa neema ya mungu, wasitumie nafasi zao kuamua kila jambo
hata kama halina maslahi kwa nchi na wananchi wanaowaongoza.
“Viongozi
wanatakiwa kuacha kujigamba na kujiona wao ni kila kitu, nafasi
walizonazo ni dhamana tu na siku moja Mungu anaweza kuwanyang’anya na
kuwapa wengine,” alisema kiongozi huyo wa kidini.
Chanzo: Mwananchi
Comments