MUNGU NDIYE ANAYEJUA NJIA YA KUKUPITISHA KUELEKEA MAFANIKIO YAKO. (sehemu ya tatu)

Mwl Nickson Mabena katika huduma.


Kutoka 13:17-18a

Baada ya sehemu ya pili kuangalia mifano kadhaa kutoka kwenye Biblia ya watu ambao Mungu aliwachagulia njia ya kupita kuelekea mafanikio yao, japokua kibinadamu njia zao zilionekana ni ngumu, mbaya ila Mwisho wao ulikuwa ni wa kishindo kikuu, kwani YESU KRISTO alikuwa pamoja nao.

Japokuwa ipo mifano mingi kwenye Biblia, ila hiyo michache iwe kielelezo.

Bwana ni mwaminifu siku zote; japokuwa tunakutana magumu ya kila namna katika safari zote ambazo niliziorodhesha katika sehemu ya kwanza ya somo hili; ila Mungu anatuwazia mema, kitu cha msingi ni Usije ukathubutu KUTENDA DHAMBI, kwani dhambi siku zote huharibu hali ya baadaye ya kila jambo.

MADHARA YA KUCHAGUA NJIA ZA KUPITA (bila uthibitisho toka kwa Mungu) KUELEKEA MAFANIKIO.

Ruthu 1:1-6.

Elimeleki, baada ya kuona kuna njaa Bethelehemu ya Yuda, wakaamua bila ya kumuuliza Mungu, yeye na mke wake Naomo pamoja na watoto wao Maloni na Kilioni, kuondoka Bethelehemu ya Yuda na kuelekea Nchi ya Moabu kwenda kutafuta chakula, kwani njaa ilizidi sana kwenye nchi yao.
Lakini cha ajabu ni hiki walipofika nchi ya Moabu, Elimeleki badala ya kupata chakula akauawa, pia na watoto wake wote wawili wakafa.
Naomi akawa amefiwa na mume, na wototo wake wote wawili.

Bethelehemu maana yake ni NYUMBA YA MKATE. Yaani walitoka nyumba ya mkate kwenda kutafuta mkate, unaweza ukawaona kama watu wa ajabu katika maamuzi yao.

Ndivyo ilivyo katika maisha ya wengi sana, huwa wanaondoka nyumba ya mkate kwenda kuutafuta mkate.

Yesu ni mkate wa uzima (Yohana 6:35,48)

Hakuna mafanikio ya kweli nje ya Yesu Kristo, watu humwacha Yesu ili kwenda kutafuta mafanikio Duniani, nikwambie tu; usione watu wa dunia wanapata mafanikio basi ukataka kuwaiga wao, huwezi jua njia walizotumia hadi kufika walipofika.

Mimi sijui njaa yako ni nini, Je! ni Mke/Mume au watoto, kazi, pesa?
ila nakusihi katika jina la Yesu Kristo, usije ukamwacha Yesu kwa sababu ya mambo ya ulimwengu huu ambayo ni ya kitambo tu!
Yesu ni Mwanzo na Mwisho, anakuwazia mema kuliko unavyofikiri ndiyo maana upo hai hata leo. Duniani huko kuna kifo, na uharibifu wa roho yako.

Naomi aliamua kurudi Bethelehemu baada ya kusikia Mungu ameleta chakula huko.

Siku zote Mungu hawezi kuwaacha watu wake, ndiyo maana alileta chakula Bethelehemu ya Yuda, Hata kama leo tunalia njaa ila kesho Bwana ataleta tu chakula.
Haina haja ya kwenda Moabu, utapata mapigo bure ndipo ukumbuke kurudi Bethelehemu.

Maombi yangu kwa Mungu, kila alisomaye somo hili Mungu afungue milango ya mafanikio kwako. Chamsingi Usimwache Yesu kama wewe Umeokoka, pia kama HUJAOKOKA ni LAZIMA UOKOKE ili Yesu aishi ndani yako pia akupe uzima wa milele.

MUNGU AKUBARIKI SANA.
by
Mwl Nickson Mabena

Comments