NDANI YA IBADA MUNGU ANAZUNGUMZA NA WATU WAKE



Ni jambo la kawaida sana kwa Mungu kuzungumza nawe ikiwa umekaa kwa namna ipasayo.Haijalishi wakati huo unasifu, unaabudu, unasoma au kusikiliza neno Mungu atazungunza nawe.Lengo lake ni kukupa mwongozo wa mambo mbalimbali ya wakati uliopo au ujao ili uweze kuboresha ibada yako.

“Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana Ibada na kufunga, Roho mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia.Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono juu yao, wakawaacha waende zao”.Matendo ya mitume 13:2-3.

Hawa lengo lao kuu lilikuwa kumfanyia Mungu Ibada lakini Roho mtakatifu anawapa mwongozo (directions) na mambo ya kufanya.Mara nyingi Mungu anatamani kusema nasi katika Ibada zetu binafsi hata za ushirika lakini kuna mambo ambayo yamekuwa vizuizi(limits) kwake kusema nasi.Mambo hayo ni kama vile kutokuwa na usafi wa moyo(utakatifu), utayari na kuwa na mazoea katika Ibada.

Imekuwa ni mazoea hata katika maombi, kunena kwa lugha watu wanafanya mazoea.Kwa wale wenye simu watanielewa kuwa katika kisanduku cha kupokelea meseji(inbox) kikijaa, meseji nyingine zinazotaka kuingia unaandikiwa hakuna nafasi “no space for new message” maana yake lazima ufute zile meseji zisizo na maana au zilizopitwa na wakati na hazina umuhimu ili zile mpya ziingie.Wakati mwingine meseji za kimungu zinashindwa kuingia ndani ya ufahamu au roho yako.Lazima ufute mawazo uliyoyahifadhi ndani yako ili meseji za Mungu ziingie.

Pia wakati mwingine utulivu wa ndani usipokuwepo Mungu anaweza kuzungumza nawe halafu usisikie.Kitu kingine ni kupuuza neno la nyuma au maagizo ya nyuma aliyokupa uyafanye kwa mfano;wakati Yesu hajafa alikuwa anazungumza na wanafunzi wake kuwa imempasa, kuteswa, na kukataliwa na watu na kufa na siku ya tatu atafufuka hivyo, wamsubiri Galilaya lakini wao walipuuza.Soma Yohana 20:10-18 na Luka 24:1-8.

Siku moja nikiwa shule nilipanda mlimani na wenzangu wawili kwenda kuomba, na mahali hapo ilikuwa ni mara kwa mara tunafanyia maombi.Tulipofika kila mmoja aliingia kumshukuru Mungu na kukabidhi eneo na kipindi mbele za Mungu.Wakati huo nikiwa nimefunika macho nikaona na tazama, uchafu Fulani wa majimaji mweupe ukitiririka.Nikaingia kumuuliza Mungu ni nini hicho ninachokiona?Mungu akaniambia kabla ya yote tusiondoke mahali hapo ila tuombe utakaso kwa ardhi ile.Nilipofumbua macho ghafla nikaona kwa mbali kikaratasi Fulani mbele yetu.Nikamwambia mmoja wa wale niliokuwa nao asogee na kukitazama akasema ni kikaratasi cha mpira wa mapenzi(kondomu) tulimshukuru Mungu tukaingia kuomba toba ya eneo lile Baada ya hapo ama kwa hakika tulimwona Mungu sana kwenye maombi hayo isivyo kawaida.

Kuna madhara makubwa sana usipojenga mazoea ya kumuachia Mungu azungumze nawe.Moja, unaweza kufanya kusudi la Mungu lisitimie na kazi yake ivurugike.Pili, unafanya usipate mambo ambayo Mungu ameahidi kukupa.Kwa mfano; fikiria ungekuwa ni mwanafunzi halafu unakwenda kwa baba yako kuomba vitu mbalimbali vya kimasomo kama vile daftari, kalamu,vitabu mbalimbali n.k halafu unajieleza na ukimaliza tu unaondoka kabla hata ya yeye kuzungumza kitu.Nakuambia hata kama ana uwezo wa kukupa hivyo vitu itakuwa vigumu kwani kuna maelekezo ya kukupa ambayo yangekufanya uvipate hivyo vitu umeyakosa.Mara zote unganishwa (be connected) na uelekezwe (be directed) na Mungu nakuhakikishia Ibada yako itakuwa na nguvu ya Mungu isiyo ya kubahatisha wakati wote.

Tunaona pia baada ya Sulemani kufanya Ibada, Mungu anazungumza naye. “Tena madhabahu ya shaba, aliyoifanyiza Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, ilikuwako huko mbele ya maskani ya BWANA; Sulemani na kusanyiko wakaiendea.Sulemani akaipandia huko madhabahu ya shaba mbele za BWANA, iliyokuwako hemani pa kukutania, akatoa sadaka elfu za kuteketezwa juu yake.Usiku ule Mungu akamtokea Sulemani, akamwambia, omba utakalo nikupe”.2Mambo ya nyakati 1:5-7.

Unafahamu ni mara ngapi Mungu anatamani kusema neno hilo kwako lakini anashindwa kwa sababu umeharibu Ibada yako?Tengeneza mazingira ya kusema na Mungu kila wakati.Watu wengi hasa vijana wanapenda kusikiliza au kuona hadithi za kutungwa, vichekesho(komedia) na nyimbo za waimbaji au wasanii mbalimbali wa kidunia hivyo kunakuwa na ugumu katika mazingira hayo kwa Mungu kusema nao.

Kuna siku moja nilimuuliza mtu mmoja kuwa je, ametafuta nyimbo mbadala za injili zenye ujumbe kama ule anaosema uko kwenye mziki wa kidunia ameshindwa?mpaka anang’ang’ania nyimbo za kidunia?Hakunipa jibu na sijui kwako msomaji wangu unasemaje juu ya hilo.

Mungu anakwambia, “Kwa nini kutoa fedha kwaajili ya kitu ambacho si chakula?Na mapato yenu kwa kitu kisichoshibisha?Nisikilizeni kwa bidii, mle kilicho chema, Na kujifurahisha nafsi zenu kwa unono”.Isaya 55:2.

Comments