NDOTO NA JINSI ZINAZOFANYA KAZI KWA WANADAMU

  Na Mch. Josephat Gwajima, Ufufuo na uzima


i) Mungu anaweza kufumbua mafumbo kupitia ndoto:-
Mwanzo 40: 2-19; Hapa tunaona kwa habari ya mwokaji na mwoshaji wa Farao ambao walipata kujua hatari iliyokuwa imejificha kwa njia ya ndoto. Kwa njia hiyo wote wawili wakajua maisha yao siku tatu mbele. Kumbe ndoto yaweza kukufunulia mitego au hatari iliyojificha au kupangwa na watu wabaya.

Farao alikwisha kupanga kuwa siku ya tatu itakuwa hukumu yao lakini bila kuwambia; lakini waliweza kufunuliwa katika ndoto. Ni maombi yangu kuwa Mungu na akuonyeshe

ii) Mungu anaweza kukurudisha au kukurudishia ulichokipoteza:-
Katika kitabu cha Danieli pekee, neno “ndoto” limeandikwa zaidi ya mara 29; Danieli alikuwa uhamishoni Babeli; akiwa huko Mungu akamwonyesha kwa habari ya kumrudisha mahali pake. Vivyo hivyo katika maisha yako inawezekana ulikuwa na mafanikio lakini sasa hayapo; au ulikuwa na afya nzuri lakini sasa haipo; katika ndoto Mungu aweza kukurudisha sehemu unayotakiwa kuwapo.

Ni maombi yangu Mungu akurudishie ile hatma njema ya maisha yako ambayo shetani aliichukua katika maisha yako.

iii) Ndoto zinaweza kukuonya:-

Ndoto zaweza kukuonya usichukue maamuzi ambayo sio sahihi, uache tabia mbaya ambayo ina mwisho mbaya. Mathayo 2: 13-16; Baada ya Herode kugundua kuwa amedhihakiwa na mamajusi akaamua kuua watoto ili amwangamize Yesu; lakini Yusufu akapewa onyo na Mungu kuwa ampeleke mtoto Misri. Ni kweli Herode aliangamiza lakini walioangamizwa ni wale ambao baba na mama zao hawakuota ndoto.

Hapa tunaona athari moja ya kutoota maana madhara yake yaliwahi kugharimu maisha ya watoto wao. Kupitia ndoto Yesu aliokolewa, Mungu huongea pia kupitia ndoto. Ndio maana ni muhimu kumwomba Mungu akupe ndoto ya kuokoa familia au ukoo wako.

iv) Mungu anaweza kutufariji katika ndoto:-
Katika maisha unaweza kupitia wakati mgumu, umezungukwa na madeni au kukata tamaa llakini Kupitia ndoto Mungu aweza kukuonyesha utakuwa nani baadaye. Kwa njia hii Yusufu alifarijiwa kupitia ndoto; kwa njia hiyo Yusufu alipokea faraja na kuhakikishiwa ushindi.

Yusufu alipoota ndoto zilisababisha achukiwe na ndugu zake, na wakamtupa shimoni na baadaye kumuuza Misri lakini ndoto yake ilibaki palepale. Haikutosha hapo, bali alisingiziwa ametaka kumbaka mke wa waziri mkuu wa Misri na akaja kufungwa. Lakini katika mateso yake Mungu alikuja kumfariji kupitia ndoto na kumrudisha katika nafasi yake.

Vivyo hivyo katika maisha yako inawezekana ulisingiziwa na kupoteza nafasi ambayo Mungu alikupa; leo kila aliyekunyang’anya nafasi naamuru uchukue nafasi yake; nafasi ya ndoa, nafasi ya umeneja, nafasi ya uongozi ninaiamuru irudi kwako katika jina la Yesu Kristo. Yule Yule aliyekupiga vita mwaka jana mwaka huu chukua nafasi yake katika jina la Yesu.

Kutoka katika ufungwa gerezeni hadi kuwa mkuu katika nchi ya Misri, yote hii ilianza katika ndoto. Kumbuka ndoto za Yusufu zilianza alipokuwa na miaka 16 lakini alikuja kuimiliki akiwa na miaka 40. Tatizo la watu wengi wanakata tamaa mapema; hutakiwi kufa moyo, hapo katikati wakati unaisubiria ndoto unaweza ukapitia mateso na mabonde lakini ndoto itakuja na itatimia usipozimia moyo.
MUNGU awabariki.

Comments