Rais Jakaya Kikwete kushiriki Mazishi ya Askofu Dr. Mosses Kulola.


Rais Jakaya Kikwete
RAIS Jakaya Kikwete leo anatarajiwa kushiriki maziko ya Askofu Mkuu wa Kanisa la EAGT, Moses Kulola (86), aliyefariki Agosti 29, jijini Dar es Salaam. Maziko hayo yatafanyika katika Kanisa la EAGT Bugando, ambapo ibada ya maziko, inatarajiwa kuanza kati ya saa 3 na 4 asubuhi na maziko yatakuwa kati saa 4 na 7.30 mchana.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Mkoa Mwanza, Evarist Ndikilo, alisema Rais Kikwete anatarajiwa kuwasili leo, ambapo atashiriki maziko ya Askofu huyo na baada ya hapo, atakuwa na ziara ya wiki moja mkoani Mwanza.

“Atafanya ziara katika wilaya zote saba za mkoa wa Mwanza na atakagua shughuli mbalimbali za maendeleo zinazofanyika katika wilaya hizo,” alisema Ndikilo.

Alisema baadhi ya shughuli anazotarajiwa kuzifanya ni kuzindua miradi ya nishati, ukiwemo mradi wa MCC unaofadhiliwa na Wamarekani katika wilaya za Sengerema, Ilemela, Misungwi, Nyamagana na Magu.

Alisema wilayani Sengerema kuna maeneo 30 ya mradi huo, Misungwi maeneo mawili, Ilemela mawili, Nyamagana mawili na Magu eneo moja la mradi, ambapo mradi huo utazinduliwa katika eneo la Bukokwa wilayani Sengerema. Pia katika ziara hiyo, Rais atazindua mradi wa kufua umeme wa megawati 60 katika eneo la Nyakato jijini Mwanza.

Kwa upande wa biashara, Rais ataweka jiwe la msingi katika jengo la kitega uchumi cha biashara lililopo eneo la Ghana na kufungua hoteli ya Gold Crest. Ndikilo alisema kwa maeneo ya afya, atazindua zahanati ya Rugeye, maabara ya hospitali ya wilaya ya Ukerewe na mashine ya X- ray katika hospitali ya Misungwi, ambayo ni ahadi yake ya muda mrefu, itakayowasaidia wananchi wa wilaya.

Kwa upande wa elimu, atafungua shule ya msingi Itulya iliyojengwa kwa msaada wa shirika la Marekani yenye madarasa saba na kuweka jiwe la msingi katika jengo la ghorofa tatu kwa ajili ya ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Magu. Aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi wakati Rais atakapokuwa kwenye ziara katika maeneo yao.

- Habari Leo -

Comments