SABABU KUU 10 KWANINI VIONGOZI WENGI HUSHINDWA KATIKA MAMBO MBALIMBALI (sehemu ya pili)

 NA REV. PETER MITIMINGI

 
4. KANUNI YA NNE
VUKA MATARAJIO YA WATU WENGINE.
Viongozi ni tofauti na wafuasi katika ukweli kwamba wanatarajia zaidi ya vile wengine wanavyotarajia. Wanaongoza njia katika kuweka juhudi na kutaka timu zao kutenda kwa ubora.
Wanapandisha alama ya kiwango. Wanaweka viwango. Hawako tayari kuridhika tu na msemo unaosema, “Hiyo inatosha”.
Wanahimiza ubora zaidi. Hii inaweza kuwaudhi baadhi ya watu mwanzoni, lakini mwishoni, huwasababisha wengine kumheshimu kiongozi.
Usiweke matarajio ya chini kama kiongozi.
Matarajio yako hayapaswi kuwa sawa na matarajio ya wafuasi wako.

Yesu aliongea juu ya jambo hili, pale alipowafundisha wanafunzi wake:
• Kwenda maili moja zaidi.
Viongozi wanapaswa kwenda maili zaidi ya zile wanazokwenda wafuasi.
Viongozi kama watakwenda maili moja kama wafuasi wao, kuna hatari wafuasi wao wasimalize hata hiyo maili moja.

• Yesu Aliongelea juu ya Kuwapa wengine joho lako na sio shati tu
• Kugeuza na shavu jingine kama mtu akikupiga.

Jinsi ya kuvuka matarajio ya watu wengine
a. Weka viwango vyako binafsi vya juu.
Usiwe kiongozi wa bei rahisi sana
Yafanye mambo yako kuwa katika viwango vizuri.
Unakula wapi, unakaa na nani, katika mazingira gani, n.k

b. Yajue matarajio ya watu wengine.
Kuna aina tatu za watu wanavyokutarajia
i. Kuna watu wanaokutarajia na kukuombea ushindwe na uporomoke kabisa katika uongozi na katika maisha yako pia (wapo wengi sana)
ii. Kuna watu wanaotarajia ukifanikiwa sawa watakuwa na wewe na wanatarajia pia ukianguka sawa pia watakuacha na kwenda kwingine.
iii. Kuna wale wanaokutarajia mafanikio na kuwaongoza kuwafikisha mahali ambapo huenda wao wenyewe hawataweza kufika. Wanakuombea na kutamani kuona kwamba unafanikiwa na kwenda mbele kila iitwapo leo (wachache sana)
Jambo la Msingi hapa Unapaswa kuvuka matarajio ya makundi matatu yote ufanye zaidi sana kwa uzuri kuliko walivyokuwa wakitarajia.

c. Maliza kila kazi au mradi, na kisha uliza, “Nini zaidi kinaweza kufanyika na kumshangaza kila mtu?”

5. KANUNI YA TANO
SIMAMA IMARA KATIKA MISIMAMO SAHIHI NA KANUNI BORA
Kwa kawaida watu humpenda na kumuheshimu kiongozi mwenye msimamo na mwenye kufuata kanuni zilizowekwa.
Kiongozi asiye na msimamo hupoteza heshima yake kadri siku zinavyoendelea.
Watu hawamuheshimu kiongozi anaye ongoza kwa bendera fuata upepo.
Misimamo thabiti hutangulia matendo makuu.
Viongozi wanafahamu kwamba kama wakifuata misukumo toka kwa wenzao, wanakwenda chini ya viwango vyao.
Wanasimamia yale wanayoyaamini, wanawaalika wengine kufikia kiwango hicho. Kama unakwenda kwa kufuata kundi, hutakwenda zaidi kuliko kundi hilo. Viongozi ni lazima wajue kilicho sahihi na wachukue msimamo.

Kweli ambazo viongozi Bora Huzijua Wakati Wanapoongoza watu:
a. Ni lazima ujifunze kutenganisha maoni na misimamo.
Pokea maoni kadri iwezekanavyo.
Tendea kazi maoni kutokana na kanuni muafaka.
Usilazimishe misimamo mahali ambapo hapahitaji kuweka misimamo.
Sio kila maoni nilazima yafanyiwe kazi.
Sio kila maoni niyakupuuzia.

b. Huwezi kuwa kiongozi bora kama hujui kile unachoamini.
Unaamini nini juu yako wewe mwenyewe
Unaamini nini juu ya wale unaowaongoza
Unaamini nini juu ya nafasi na dhamana uliyopewa kama kiongozi.

c. Ni lazima uonyeshe njia na kuongoza kwa mfano ili upate heshima.
Moja ya mawe ya msingi ya kujengea heshima ya kiongozi ni kuongoza kwa mfano.
Sio kuwaambia watu hii ndio njia ya kwenda na wewe mwenyewe huikanyagi wala kuipita hiyo njia.
Kiongozi maana yake unatangulia mbele na wafuasi wanafuta nyuma.
Kila hatua unayoinyanyua wafuasi wako wanabandika.

d. Ni pale tu unapokuwa tayari kufa kwa ajili ya kitu Fulani ndipo unastahili kuishi.
Kama hautakuwa tayari kufa kwaajili ya kile unachokiamini basi bado hujajua kusudi lako la maisha ni nini.

6. KANUNI YA SITA
UWE NA UKOMAVU AMBAO UNAPITA UMRI WAKO, ELIMU YAKO NA UZOEFU WAKO.

Hebu na tukabili ukweli huu. Jambo moja linalokuza heshima popote pale ni wakati mtu anapoonyesha ukomavu ambao unazidi sana miaka yake, elimu yake na uzoefu wake.
Pale viongozi wanapoonyesha hekima au bidii inayozidi umri wao, wanapata kuaminiwa na watu na kuheshimiwa.
Weka akilini kwamba kuna kitu kama “Ukomavu tofauti”. Hii ina maana watoto wadogo wanaweza kukomaa kupita umri wao. Kwa mfano tunaweza kusema, “Kijana yule amekomaa zaidi ukilinganisha na umri wa miaka mitano.” Katika kanuni hii, tunaongelea viongozi kuonyesha ukomavu kupita umri wao au viwango vya uzoefu wao.
Kuna baadhi ya viongozi unashindwa hata kuelewa uwaweke kwenye kundi gani maana mambo wanayoyafanya hata wale wafuasi wao wa hali ya chini hawawezi kufanya mambo ya kitoto na yasiyo na ukomavu kama wao.
Viongozi kama hao hawawezi kujenga heshima kamwe katika uongozi wao na badala yake watajenga migogoro, marumbano na magomvi yasiyoisha katika uongozi wao.



Alama tano za Ukomavu wa Kiongozi:
a.ALAMA YA KWANZA YA UKOMAVU WA KIONGOZI
Kuwajibika:
Ukomavu hauji na umri; unakuja na kukubali majukumu na kuwajibika ipasavyo.
Unaweza kukuta katika familia mzaliwa mwa kwanza (firstborn) ambaye ndio angetegemewa kuwa msimamizi wa familia anakuwa ni kiongozi asiye na ukomavu, last born aambaye ndio alikuwa anachukuliwa kama mdogo wa kusaidiwa amekomaa kiasi kwamba ndiye amebeba majukumu ya kuwatunza wazazi na hata kaka zake na dada zake. Kwahiyo ukomavu ni zaidi ya umri. Sio swala la kuwa na mmvi nyingi bali ni swala la mabega yako yanauwezo kiasi gani katika kubeba majukumu.

b. ALAMA YA PILI YA UKOMAVU WA KIONGOZI
Kujiamini:
Hakuna kitu kinachoshawishi watu kama roho ya kujiamini.
Watu huwafuata watu wanaojiamini. Usipojiamini unapoteza nguvu ya kuaminika.
Kujiamini ni mtaji wa kwanza wa kiongozi.
Hata kama ulikuwa huna kitu au huna hata kitendea kazi, ukiwa na kujiamini tayari una mtaji, tayari unamahali pa kuanzia. Watu hupeleka pesa, mali vitendea kazi kwa kiongozi anayejiamini.
Unapokwenda kufanya usaili (interview) mbalimbali katika kwaajili ya kazi au visa au chochote kabla hawaja angalia vyeti vyako au document zako, cha kwanza wanachoangalia ni ujarisi wako na kujiamini kwako kabla hata ya vingine. Unaweza ukapewa visa au kazi hata kabla hujafungua document yoyote.
Kumbuka kwamba Kama hujiamini mwenyewe, huwezi kuaminika.

c. ALAMA YA TATU YA UKOMAVU WA KIONGOZI
Kudumu
Watu hufanya kile wanachokiona.
Wanasahau ujumbe wako, lakini wanafuata nyayo zako.
Kiongozi mwenye ukomavu ni yule anayedumu kufanya kile alichokianzisha hata kama anapitia nyakati ngumu anadumu kutekeleza kile anacho amini ameitiwa kwacho.
Usiwe mtu wa kuanzisha vitu vipya kila siku hata kabla havija komaa umeshaacha na kuanzisha kitu kingine.
Mfano unaanzisha hoteli hata kabla wateja hawajaanza kuzoea unabadilisha watu wanakuja kununua chakula hapo hotelini mara wanakuta kibao mlangoni MITIMINGI AUTO SPARE PARTS kumbe umeshaacha kuuza chakula sasa una uza spare za magali, mara kesho na kesho kutwa watu wanakuja kununua spare za magari wanakuta kumbe imeshakuwa ni mashine ya kusaga nafaka. Kiongozi anaye heshimika ni yule anayedumu kufanya kile alichoitiwa kukifanya hata kama anakabiliana na upinzani mkubwa namna gani.

d. ALAMA YA NNE YA UKOMAVU WA KIONGOZI
Mwenendo:
Mtu mwenye uwezo wa kufanya maamuzi kwa kuzingatia kanuni na mambo ya msingi.
Wewe ni mtu yule yule ukiwa kwenye mwanga na kwenye giza ni mtu mmoja.
Watu watakavyokukuta kwenye mwanga ndivyo watakavyo kukuta gizani.
Mwenendo wako ni mawe ya kujenga msingi imara wa uongozi wako.
e. Usalama:
Watu hutafuta kuwa salama, na kiongozi salama huleta mazingira salama.
Kiongozi mwenye usalama wa ndani atasababisha wafuasi wake kujisikia wapo salama pia.
Kiongozi mwenye hofu ya kupinduliwa kila siku, hujipindua mwenyewe na mwishoni atapindua wafuasi wake pia.
Kiongozi mwenye usalama wa ndani haogopi kugawa majukumu kwa watu wake maana ana usalama wa kutosha.
Kiongozi mwenye usalaama wa ndani hugawa vyote yaani madaraka na mamlaka.
Viongozi wengi leo kwasababu ya tatizo la kukusa usalaama wa ndani wanagawa madaraka tu lakini hawagawi mamlaka. Wanagawa vyeo lakini hawagawi nguvu.
Kiongozi mwenye usalama atakuwa ni mtu mwenye heshima na kupendwa katika wakati wote wa uongozi wake na kwa vizazi vijavyo pia.

PLZ UKIMALIZA KUSOMA USISAHAU KUANDIKA COMMENT YA KILE KILICHO KUGUSA
KUMBUKA THIS IS A CLASS NOT JUST A POST OF READING AND LIKING IT REQUIRES A FEEDBACK. Blessings

Comments