![]() |
Na Mchungaji Kiongozi, Ufufuo na Uzima; Josephat Gwajima |
UTANGULIZI:
Kwa
kichwa cha somo hili, utakuwa umejiuliza maswali kuwa “namaanisha ufalme wa
kwenye maji au namaanisha ufalme wa majini au pepo wachafu” lakini vyovyote
vile utakavyotafsiri katika maana hizo mbili utakuwa upo sahihi kwa ujumbe huu.
Ufunuo 2:12-13 “..napajua ukaapo ndipo
katika kiti cha enzi cha shetani…” ni muhimu kujua kuwa, huwezi kumshinda adui
bila kujua mbinu na silaha zake anazozitumia. Maombi ya wakristo wengi
yamejikita katika kujilinda dhidi ya shetani (Defensive Prayer) lakini kama unataka kumshinda shetani unatakiwa
uwe na maombi ya kumshambilia (Offensive
Prayers) na kuwa huwezi kumshinda adui bila kujua mbinu zake, ndio maana
tunajifunza kuhusu ufalme wake.
MAANA YA AKAAPO SHETANI:
Kwa
kawaida utawala wa shetani duniani, umeweka himaya yake katika maeneo tofauti
tofauti, na ndio maana katika kila mkoa au wilaya kuna mtu au eneo ambalo
linaogopewa na watu. Katika maeneo mengi utakuta mtu ambaye ama kwa nguvu zake
za rohoni au mwilini amekuwa akiogopwa na watu. Mtu huyo au mahali hapo ndipo
panaitwa pale akaapo shetani. Maeneo mengi ya vijijini huwa kunakuwa na mtu
anayeogopewa na mara nyingi husababishwa na uchawi wake; mtu huyo ndiye
anayeitwa kiti cha enzi cha shetani katika kijiji hiko.
Ili
kuweza kuitawala dunia, shetani ameweka tawala zake sehemu tofauti; maeneo hayo
sio kuzimu yenyewe bali ni ngome ya shetani katika eneo husika. Kimsingi, hata
katika maisha, kazi, masomo au biashara za watu kuna maeneo ambayo shetani
anakaa; hapo panaitwa kiti cha enzi cha shetani katika biashara, nyumba au
katika mwili.
NENO MAJINI KATIKA BIBLIA:
Mambo ya walawi 17:7, ukiangalia
kibiblia neno hili “Jini” kwa lugha ya kingeleza limetajwa kama “goat idols” Kimsingi katika agano la
kale kulikuwa na aina nyingi za miungu; na mojawapo alikuwa mungu mbuzi-dume.
Na ndio maana katika biblia wakristo hawafananishwi na mbuzi bali kondoo
kwasababu mbuzi dume alikuwa moja ya miungu iliyokuwa inaabudiwa kama mashetani.
2Mambo ya Nyakati 11:15, hapa pia
wanatajwa aina hiyo ya mashetani waliokuwa wanakaa ndani ya miungu-mbuzi “goat idols” Miungu mbuzi ilikuwa ni
mashetani waliokuwa wakiabudiwa na watu katika agano la kale ambao kwasasa ndio
walewale wanaofahamika kama majini.
UNDANI KUHUSU MAJINI:
Majini
ni mashetani ambao wanafuatana na tamaduni za nchi za kiarabu, lakini pia, majini
haya yalikuwa ni mashetani yanayofuatana na maji au mikusanyiko ya maji;
kwasababu makao yao makuu yalikuwa majini ukisoma, Ezekieli 29:3-5. Na ndio maana mfalme wa Misri, Farao alikuwa
anakwenda kuabudu katika maji, Ukisoma, Ezekieli
32:2-3 inaeleza jinsi Farao alivyotegemea miungu ya katika maji kiasi
biblia inamwita joka wa majini.
Kwasababu
ya mashetani hao wanaokaa majini, mara nyingi maji katika biblia yamekuwa
yakitumika kuonyesha uharibifu, Zaburi
18:16. Ndio maana hata kipindi cha Musa alipokuwa anamfuata Farao ili
kuomba ruhusa ya kutoka utumwani, maranyingi, alikuwa akimkuta anatoka au
anakwenda majini, Kutoka 7:18; 8:20;
Ilikuwa ni desturi ya farao kwenda kuabudu katika mikusanyiko ya maji. Maandiko
yameonyesha sana kuhusu mashetani wa baharini, katika Ufunuo 14:31; 20:13, Isaya 27:1, Ayubu 3:8.
Ufunuo 12:1-16; Joka jekundu ni ishara
ya shetani. Kama nilivyosema mwanzoni, majini ni mashetani yanayofuatana na
desturi za kiarabu, na yanaitwa majini kwasababu yanatokea katika maji. Mashetani
haya ndiyo ambayo yalikuwa yakiabudiwa na Mfalme wa Misri, Farao na ndio maana
katika maeneo ambayo yametawaliwa sana na waarabu lazima utakuta kuna aina hii
ya mashetani. Na mashambulizi mengi ya rohoni huanzia kwa majini hawa.
Hili
ni kundi la mashetani, wanaofanya kazi zao ndani ya maji; pia, majini haya
yanauwezo wa kukaa nchi kavu na kuishi kama watu, wakaongea na kupanda gari kama
watu. Ndio maana matatizo yote ya rohoni katika maeneo ya pwani husababishwa na
majini, kuanzia katika tawala za kiserikali mpaka katika nyumba za mtu mmoja
mmoja. Asilimia kubwa ya matatizo ya watu yamesababishwa na majini, ambao
hutenda kazi kumwakilisha shetani mahali husika. Majini ni aina ya mashetani
yanayotumiwa kuvuruga makanisa, kuleta visasi, kufanya watu kuwa wazinzi,
kuharibu amani, kuleta kutokuamini (ukiondoa majini kuna baadhi ya dini
zinakufa) na magonjwa yote; kazi hizi zote hufanywa na majini.
DALILI ZA UWEPO WA MAJINI KATIKA MAISHA YA
WATU:
- Dalili zifuatazo ni za mtu ambaye ama ana majini au anafuatiliwa na majini:-
- Unakuwa unaota ndoto upo ndani ya maji; ama unatembea ndani ya maji, unaingia majini au unatembea juu ya maji.
- kila wakati unajikuta umeona au umeokota pete za dhahabu; mara nyingi majini wanaotaka kukutana kimwili na wanadamu hutegesha mikufu au pete ili kuunganishwa naye.
- Mara nyingi unapotembea unakuwa unasikia harufu ya udi, ubani au marashi. Si lazima majini hayo yawe ndani yako lakini yanaweza kuwa yanakufuatilia ili kukudhuru.
- Wakati wa usiku unasikia vitu vimepigwa kwenye bati au darini bila kujua chanzo na mwisho wake.
- Kudondoka chooni ni dalili nyingine ya mtu anayefuatiliwa na majini.
- Wewe ni mkristo lakini ukisikia adhana unajisikia kuipenda; na ndio maana watu wengi wakija kuombewa wanalipuka mapepo yanayopiga adhana.
- Kukonda kupita kiasi.
- Kupenda kuvaa nguo za nusu uchi.
2 Wathesalonike 2:8, alisema Mtume Paulo alikua amepakwa mafuta
na Mungu kutenda mambo makubwa lakini pamoja na hayo shetani aliweza
kumzuia kwenda Thesalonike kuifanya kazi ya Bwana. kumbe kupitia majini
shetani aweza kutenda kazi ama ndani au nje ya watu ili kufanikisha azma
yake ya kutesa maisha ya watu.
USHINDI DHIDI YA MAJINI:
Ili
kupashinda na kupaondoa pale akaapo shetani ni lazima kuwashambulia majini ambao ndio
wanaotenda kazi katika maisha ya watu. Huwezi kutatua tatizo bila kushughulika
na chanzo chake, na kama tulivyoona hapo juu kuwa majini ndio wanaosababisha
matatizo ya watu wengi, hivyo ukishambulia majini kwa Jina la Yesu Kristo
unajiondoa mwenyewe katika tatizo ambalo limeletwa na shetani katika maisha yako.
Ukiokoka
unapokea mamlaka ya kuteketeza kazi za shetani, tumia mamlaka hiyo kuharibu
kazi zote za majini katika maisha yako.
Comments