Mungu anawapenda sana wanadamu na Biblia inasema wazi kuhusu
hili katika kitabu cha Maombolezo 3:31;
Ni raha yake kuona hatuna matatizo na tunaishi kwa amani. Mungu hakumuumba
mwanadamu ateseke bali alimuumba afanikiwe akiwa duniani na kuishi kwa furaha.
Wakati huohuo, shetani kwa asili hapendi mtu aliyeumbwa na
Mungu afanikiwe na ndio maana katika Luka
3:16 inasema, “…ambaye shetani amemfunga miaka kumi na minane…” (Matendo 10:38; 2Wathesalonike 2:18-19)
kwa maandiko hayo tunaweza kujua kuwa shetani anaweza kufunga, kuzuia, kupinga
na kushindana na mtu. Kwa asili shetani ni mshindani na furaha yake ni kuwatesa
wanadamu ambao wanapendwa na Mungu. Yeye hufanya hivi ili kuumiza moyo wa Mungu
kupitia wanadamu walioumbwa na Mungu.
SHETANI ANAWEZA
KUMFUNGA MTU:
Kama tulivyoona kuwa shetani anapenda kuwatesa wanadamu na
ili kutimiza lengo lake njia mojawapo anayotumia ni kuwafunga watu. Na tunapotaja
vifungo, tunakuwa tunazungumzia vifungo vya aina kuu tatu, yaani, Vifungo vya
mwilini, Vifungo vya rohoni na vifungo vya nafsini kwasababu mtu ni roho
inayokaa ndani ya nyumba iitwayo mwili. Katika hatua hii ya kwanza tunaanza
kuangalia kwa undani kuhusu vifungo vya mwilini:-
Mwili ni nini?
Hatuwezi kujua namna mwili unavyoweza kufungwa bila kujua
asili ya mwili wa binadamu. Tuanze kwa kuangalia andiko hili Mwanzo 2:7 “BWANA Mungu akamfanya mtu
kutoka katika mavumbi ya ardhi…” kumbe asili ya mwili wa mwanadamu ni mavumbi
au udongo. Na ndio maana katika Isaya 64:8 Biblia inasema, “… sisi tu udongo
nawe ni mfinyanzi wetu...” nabii Isaya ambaye aliwahi kumuona Mungu lakini
alijua ukweli huu kuwa mwili ni mavumbi (Ayubu
7:21, 34:15). Kumbe pamoja na kuwa umevaa vizuri au umeupamba mwili vizuri
lakini asili yake ni udongo na katika ulimwengu wa roho huonekana kuwa ni
udongo kabisa. Kwa ufupi mwili wa mwanadamu ni udongo na mtu anapokufa mwili
huirudia nchi (Mhubiri 12:7) yaani
mavumbi.
Ndio maana hata watu wanapooana ni miili ndio ambayo inakuwa
imeoana na si roho kwasababu mbinguni hakuna kuoa wala kuoana kule ni katika
roho. Kwa kujua kuwa mwili ni udongo basi namna ambayo unaweza kuutendea udongo
wa kawaida ndivyo vilevile waweza kuutendea mwili wa binadamu. Udongo wa
ardhini waweza kuoteshwa mimea na kuchimbwa, vilevile na mwili wa binadamu
waweza kufanyiwa hivyo.
TOFAUTI KATI YA MWILI
NA UDONGO WA KAWAIDA:
Kuna mambo mawili makuu yanayosababisha mwili wa binadamu uwe
tofauti na udongo wa kawaida.
1. Mwili uliwahi kushikwa na mikono ya Mungu maana hakuna
kitu kilichowahi kushikwa na Mungu na kikabaki kama kilivyo.
2. Ndani ya mwili wa mwanadamu kuna roho ambayo huuisha mwili
na kuupa uhai. Kwasababu hizo mwili wa mwanadamu hutofautina na udongo wa
kawaida.
MWILI WA MWANADAMU
UNAWEZA KUPANDIWA VITU:
Biblia iko wazi kuwa Mungu wa mbinguni anaweza kupanda, (Mwanzo 2:8); kumbe Mungu ambaye ni
roho (Yohana 4:24) anaweza kupanda katika
ardhi kabisa vivyo hivyo shetani naye ni roho naye ana uwezo wa kupanda katika
mwili ambao kwa asili ni udongo. Hapa ndipo lile andiko la “KILA PANDO AMBALO
BABA WA MBINGUNI HAKULIPANDA LITANG’OLEWA” linapoleta maana; Mapando ambayo
hayajapandwa na Baba wa mbinguni ni lazima yatakuwa yamepandwa na shetani. Ndio
maana ya mfano wa Yesu katika Mathayo
13:25 “lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya
ngano, akaenda zake.” Huyo ambaye Yesu anamwita adui ni shetani mwenyewe. Kumbe
unapolala au kujisahau shetani huja na kupanda magugu, hili jambo linatendeka
katika ulimwengu wa roho. Ni muhimu kujua siri hii kwamba kama vile udongo
unavyopandwa vivyohivyo shetani naye anao uwezo wa kupanda juu ya mwili wa
mwanadamu.
Unaweza kumsikia mtu analalamika kuwa mwili unachoma lakini
kumbe katika ulimwengu wa roho mtu huyo amechomwa mkuki au kisu. Kufikia hapa sasa twaweza kujua kwanini Mungu
alikataza kupanda mbegu mbili za tofauti katika shamba moja (Mambo ya Walawi 19:19). Mungu alisema
hivi akitufundisha kuwa mahali ambapo Mungu amepanda shetani hatakiwi kupanda
mahali pale. Mtu anaweza kuhisi vitu
vinatembea mwilini kumbe amepandiwa wanyama wanaotembea katika mwili wake.
PEPO ANAWEZA KUJIGEUZA
NA KUWA CHOCHOTE:
Tulijifunza kuhusu sheria mbili za rohoni, hapo tuliona uwezo
wa pepo wachafu kujigeuza na kuwa kitu kingine yaani kuvaa sura mbali mbali ili
kutimiza kazi zao. Jambo hili twaweza kuliona katika (1Wafalme 22:19-23) huyu pepo kwa asili hakuwa wa uongo lakini
aliweza akaenda na akawa pepo wa uongo. Yule pepo akaingia katika vinywa vya
manabii wa Mfalme Ahabu na kuwafanya wamtabirie uongo. Kwa maana hiyo tunaona
uwezekano wa pepo mchafu kujigeuza na kuwa kitu chochote ili kutimiza lengo
alilokusudia.
Sasa twaweza jua kuwa mapando tuliyokuwa tunayazungumzia ni pepo
wachafu ambao hujigeuza na kuwa kile kitu na hivi ndivyo vinavyoitwa “Vifungo
vya mwilini”. Wakati
mwingine pepo anaweza kujigeuza na kuwa kinywa cha mtu, kama pepo wa katika (1wafalme
22:19-23) alivyofanya. Hivyo; unaweza kumuona mtu anatukana matusi ya ajabu
bila hata aibu, kumbe pepo kajigeuza na kuwa kinywa chake. Pepo anaweza kuwa
uso wa simba, unamkuta baba mwenye nyumba mkali kwa watoto na mkewe kumbe ni
uso wa simba. Kwahiyo; pepo wanaweza kujigeuza maumbo mbalimbali kama nyani, simba,
paka hata bundi ili mradi kuharibu hatma ya mtu. Mnamkuta dada aolewi kumbe uso
wake umefunikwa kwa sura ya simba, kila mwanaume anayetaka kumchumbia haoni
sura nzuri bali anaona simba. Na ndio maana kuna baadhi ya wadada watumia muda
mwingi kujipodoa lakini bado hawapendezi kwa kuwa uso sio wa kwake.
KUNG’OA KILA KILICHOPANDWA KATIKA
MWILI WAKO:
Imeandikwa
kila pando asilolipanda Baba wa mbinguni litang’olewa, hivyo Mungu ametupa
mamlaka ya kung’oa kila pando la kishetani yaliyopandwa katika mwili. Miili
yetu ni Hekalu la Roho Mtakatifu hivyo shetani hatakiwi kugusa sehemu yoyote ya
mwili wako.
Tumia mamlaka
yako kung’oa kila pando ambalo shetani amepanda katika maisha yako mapando ya
magonjwa, homa zisizoisha, ukimwi, mwasho wa mwili na matatizo mbalimbali. Jina
la Yesu lina mamlaka yote dhidi ya kazi zote za shetani katika maisha yako.
Comments