MAUAJI KANISANI MWANZA, MMOJA AUAWA WENGINE WAJERUHIWA KWA MAPANGA


Waumini wakitafakari hali iliyotokea kanisani hapo.
Mtu mmoja ameuawa na wengine watatu kujeruhiwa kufuatia shambulizi lililofanywa na kundi la watu wasiofahamika usiku wa kuamkia jumanne tarehe 22 October 2013, katika kanisa la Gilgal Christian Worship Centre lililopo eneo la Pasiansi wilaya ya Ilemela jijini Mwanza.

Tukio hilo lililotokea majira ya saa saba usiku linamtaja Elia Lunyamila (35) ambaye ni mlinzi pia ni mwenyekiti wa vijana wa kanisa kuuawa akiwa amejumuika kwenye ibada na waumini wengine Alex Msakuzi na Tumsifu Pungu ambao hali zao zinatajwa kuwa taabani wakipatiwa matibabu Hospitali ya Rufaa Bugando Mwanza baada ya kujeruhiwa vibaya kwa kukatwakatwa na mapanga sehemu mbalimbali za mwili.

Askofu wa kanisa hilo Eliabu Sentoz amelaani tukio hilo akilitaja kuwa ni la kinyama kwani limefanyika sehemu ya ibada akiwataka wananchi kuungana pamoja kulisaidia jeshi la polisi katika kutoa taarifa kuwabaini wahusika wa shambulio hilo na akiiomba serikali kuongeza nguvu kukabiriana na wahalifu hao.

Kamanda wa polisi mkoani Mwanza Ernest Mangu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo mpaka sasa hakuna taarifa za kuibiwa kwa kitu chochote ndani ya kanisa, hali ambayo inalifanya tukio hilo kuwa na maswali mengi likihofiwa kufananishwa na yale ya uchomaji moto Makanisa.

Wananchi wakitafakari tukio hilo nje ya jengo la Kanisa la Gilgal Christian Centre lililopo Pasiansi Ilemela jijini Mwanza.
Ndugu na majirani pamoja na waumini waliomfahamu marehemu Elia Lunyamila aliyeuawa kwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana wakiwa wamekusanyika nyumbani kwa marehemu kuomboleza .
Askofu wa kanisa la Gilgal Christian Centre Eliabu Sentozi. Picha kwahisani ya Gsengo, 

Chanzo cha habari Mjapinc.blogspot.com

Comments