Mchungaji Josephat Gwajima ambaye ni Mchungaji kiongozi wa kanisa la Glory Of Christ Tanzania Church maarufu kama Nyumba ya Ufufuo na Uzima
lenye makao yake makuu Kawe, jijini Dar es Salaam; amefanya mahojiano
na Mtangazaji wa Radio Sauti ya Injili iliyopo mjini Moshi asubuhi ya
leo. Mahojiano hayo ambayo yalidumu kwa muda wa saa nzima yalilenga
kuelezea juu ya umuhimu wa neno la Mungu kwa kanisa la leo na pia kujua
undani wa mkutano wa Injili unaotarajiwa kuanza jumapili hii mjini
Moshi.
Mahojiano ya Mch. Josephat Gwajima na Deo Mosha wa Radio Sauti ya Injili - Moshi. |
Mtangaziji huyo aitwaye Deo Mosha aliandaa mada ambayo kwayo ilimpatia
wasaa mzuri kwa Mchungaji Josephat Gwajima kuelezea kwa undani juu ya
umuhimu wa neno la Mungu kwa wakristo. Akieleza kwa undani juu ya
umuhimu wa neno la Mungu, Mch. Gwajima alieleza historia fupi ya Ukristo
kuanzia kipindi cha Martin Luther hadi kipindi hiki cha kunena kwa
lugha. Alisema, injili ilitoka ulaya na kuja Afrika lakini katika
kipindi hiki cha mwisho waafrika ndio watakao kuwa risasi ya mwisho ya
injili kutoka katika bunduki ya Mungu.
Akieleza changamoto alizokutana nazo katika mkutano wa Injili wa Arusha,
Mch. Gwajima alisema kuwa changamoto zipo, kwasababu ya ukweli kuwa
mkutano wa injili ni mjumuiko wa mambo mengi sana. Akitolea mfano wa
Mkutano wa kanisa hilo jijini Arusha, Mch. Gwajima alisema,
"tumesafirisha vyombo vya mziki roli mbili na mabasi yaliyobeba
wachungaji wapatao mia mbili kutoka Dar es Salaam waliokuja kwa ajili ya
kuhudumia watu, kwa maana hiyo hizo gharama zote ni changamoto kwetu"
Pia alisema, "kanisa la Ufufuo na Uzima linajitegemea katika mikutano
yake bila kutegemea wafadhili kutoka nje ya nchi kwa maana hiyo
changamoto bado ni kubwa kwetu."
Akiongelea Mkutano wa Moshi unaotarajiwa kuanza tarehe 20 hadi 27
Oktoba, alisema kuwa mkutano huo utakuwa wa maajabu na miujiza ya kupita
kawaida, na akawaasa watu wa Moshi kujitokeza kwa wingi kuja kushuhudia
waliokuwa msukuleni wakirudishwa na waliokufa kurudi kwenye uhai wao
tena.
Mchungaji Josephat Gwajima akifanya mahojiano na mtangazaji Deo Mosha. |
Alipoulizwa kwa habari za Misukule na kufufua watu waliokufa; Mch
Gwajima alisema kuwa kazi hii si ya mtu mmoja bali ni kazi ya Bwana Yesu
ambayo Mtu yeyote wa Mungu atakayeamua kufufua na kurudisha; Mungu
atamtumia kwa nguvu ile ile. Akitoa andiko kutoka katika kitabu cha Mathayo 10:8;
alisema kuwa Biblia iko wazi sana kwa habari ya kufufua watu waliokufa;
na kusema kuwa tatizo la waafrika wengi ni vile wanashindwa kuthamini
kitu kikubwa ambacho Mungu anakianzisha kwao.
Mwisho, alitoa wito kwa wachungaji vijana kwa kusema kuwa "yatupasa
kuifanya kazi ya BWANA kungali bado asubuhi maana saa inakuja ambayo
hatoweza mtu kuifanya" kwa maneno hayo aliwaasa vijana kuifanya kazi ya
Mungu wangali vijana kwasababu mtu akianza kazi ujanani anapata muda
mzuri wa kusahihisha makosa yake lakini akianza kazi uzeeni atakosa muda
wa kusahihisha makosa na hivyo kushindwa kufanya vizuri.
Comments