Kanisa la Kiinjili Kilutheri Tanzania (KKKT), limemfukuza kazi mmoja wa
wainjilisti wake katika mission ya Rukwa, kwa madai ya kupotosha waumini
wake, huku mwenyewe akishikilia msimamo kuwa anakinywea kikombe
alichonyweshewa Martin Luther, na atashikilia msimamo huo hadi pumzi
yake ya mwisho hapa duniani.
Mwinjilisti huyo, Goodlove Kyenda, amesisitiza kuwa hatahama wala
kuanzisha kanisa lake, bali atashikilia msimamo wake wa kupinga fundisho
jipya lililopo katika kitabu kipya cha Mwongozo wa ibada kilichotolewa
mapema mwaka huu, kiitwacho “Tumwabudu Bwana” kilichochukua nafasi ya
kile cha zamani kiitwacho, “Mwimbieni Bwana.”
Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na mchungaji wa KKKT, Usharika
wa Rukwa, Zebedayo Mbilinyi, mwinjilisiti Kyenda aliamuriwa kuondoka
mara moja na kikao cha Kamati Tendaji ya Misioni ya Rukwa iliyoketi
kujadili shauri hilo mwezi Septemba mwaka huu, ambapo iliiagiza
Halmshauri ya usharika wa Luther kuwa Kyenda aondoke ndani ya siku tatu
(saa 72) katika nyumba aliyokuwa akiishi ambayo ni mali ya kanisa.
Akielezea mkasa huo, mwinjilisti huyo alisema kuwa haogopi hali
iliyomkuta kwa kuwa anatetea kweli na lengo lake ni kuponya kanisa kama
alivyofanya Martin Luther alipopinga baadhi ya mafundisho ya kanisa
katoliki akiibuka na hoja 95 zilizodhihirisha mapungufu makubwa.
Akifafanua alisema kuwa katika kitabu hicho kipya kilichotolewa mwaka
huu, katika ukurasa wa 607, kuna mafundisho ya kuwaenzi watu waliokufa,
yaani Mungu amhamishe kutoka alipo (pugatolio) jambo ambalo ni kinyume
na Neno la Mungu.
Mwinjilisti huyo amekumbana na mkasa huo ikiwa ni mwaka mmoja tu, tangu
apewe barua ya ajira, katika utumishi ndani ya kanisa lenye jumla ya
waumini 400.
Alisema sakata lilikuwa hivi: “Oktoba 28, 2012 ilikuwa ni siku ya
Matengenezo kama ratiba ya kitabu cha “Tumwabudu Bwana” Kilichohakikiwa
na wasomi nchini Ujerumani kikiwa na nyongeza ya vipengele tata;
kinavyoonesha, na mimi ndiye niliyeongoza ibada.”
Kisha aliongeza: “Nilifundisha, lakini ilipofika kipengele cha kuwaenzi
wafu kama kitabu kinavyoonesha niliweka sawa fundisho hilo kama
linavyoelezwa kwenye Biblia kitabu cha Mhubiri 9:4-6 kwamba hakuna
namna yoyote unayoweza kumuombea mtu aliyekufa akapata rehema,
niliwaambia hatma ya maisha ya kila mmoja inategemea maisha yake
aliyoishi duniani.”
Mwinjilisti huyo alikiambia chanzo cha blog hii kuwa, baada ya hapo
vilianza vikao vya uongozi wa misheni hiyo kimyakimya huku yeye
akishiriki kikao kimoja, na kwamba ndani ya vikao hivyo kulikuwa na
makundi mawili; ya wanaomuunga mkono elimu aliyowapa na wanaopinga.
Kiongozi wa kanisa alilofukuzwa mwinjilisti Kyenda, Mchungaji Mbilinyi,
akiongea na chanzo cha habari hii alisema kuwa mwinjilisti huyo alikiuka
mwongozo wa taratibu za ibada kwa kufundisha mafundisho yanayopingana
na imani ya KKKT.
Alisema mwongozo wa ibada zote uko kwenye kitabu cha Tumwabudu Mungu
ambacho kimeandikwa na wasomi na wanatheologia wabobevu wa kanisa hilo
duniani, ambacho mhubiri anapaswa kukifuata na kwamba mwinjilisti
alikwenda mbali zaidi ya kile kilichomo kwenye mwongozo huo.
“Ikiwa ataomba msamaha kwenye Halmashauri, kanisa linaweza kumsikiliza,
la! Hajafanya hivyo, basi hatokuwa na sehemu ya uongozi wa kanisa,”
alisema.
Hata hivyo, chanzo cha habari hii kilienda mbali zaidi na kutaka
ufafanuzi kutoka kwa viongozi wa KKKT, hususan kipengele hicho ambacho
kimebainishwa kuwa kinaleta msuguano wa chini kwa chini hivyo
kutengeneza makundi mawili.
Chanzo cha habari hii Kiliongea na Katibu wa kanisa hilo ambaye
alisema: “Mimi niko safarini Bukoba, siwezi kusema chochote, subirini
hadi nitakaporudi, nimekuelewa sana! Ila siwezi kujibu chochote.”
Hatukuishia hapo, tuliongea na Mkuu wa Dayosisi ya Arusha, mchungaji
Godwin Lekashu, naye alikuwa na haya ya kusema: “Siko ofisini, nipo
mahali pagumu, nitakupigia baada ya dakika ishirini.”
chanzo cha habari hii kilisubiri dakika hizo 20, lakini hakupiga kama
alivyosema, na zilipokatika dakika 30 lilimpigia tena, lakini mtumishi
huyo hakuweza kupokea simu baadala yake simu ya mkuu huyo ilikuwa ikiita
tu bila kupokelewa.
Sakata hilo limesababisha baadhi ya wazee wa kanisa usharikani hapo kupita nyumba kwa nyumba kwa baadhi ya wazee wa mitaa wa kanisa kulinusuru na mpasuko uliopelekea kutokea makundi mawili ya Mchungaji wa kanisa hilo na Mwinjilisti.
Comments