UMEUWEZA ULIMI WAKO AU UMEKUWEZA?

 

Mithali 18:20-21 inasema, " Tumbo la mtu litashiba matunda ya kinywa chake...Uwezo wa mauti na Uzima viko kwenye ulimi, nao waupendao watakula matunda yake"

Kwenye ulimi wako kuna maneno, na maneno hayo uyatamkayo yana athari kubwa sana kwako na kwa wale unaowatamkia...Kwenye mdomo wako yanaweza kutoka maneno ya kutia UZIMA au ya KUUA/MAUTI...Inategemea na we una uelewa kiasi gani kuhusu nguvu ya Ulimi wako...Silaha kubwa na ya mabadiliko hasi ama chanya kwenye ulimwengu wa roho ni maneno yako...Kwa maneno yako unatengeneza maisha na kwa maneno yako unatengeneza mauti yako na ya wale unaowatamkia!

Kwenye ulimi wako kuna nguvu ya ajabu, ambayo inafanya kazi hata kama unajua au hujui...ni silaha ifanyayo kazi mara tu uamuapo kufungua kinywa chako..."KWA KINYWA MTU UKIRI HATA KUPATA WOKOVU" (Warumi 10:10)...Kama ukinena maneno mema na kukiri mema katika hali zote bila kuangalia mazingira yako, uwe na uhakika unakuwa umefaulu kuulazimisha ulimwengu wa roho ufungue milango yake ya mema na mafanikio sawa ba ukiri wako mwema....Ukikiri au kuungama mabaya, kushindwa, lawama, manung'uniko na kutofanikiwa, sekunde ile ile mambo hayo yanatokea kwenye ulimwengu wa roho! Kwanini? Ni kwa sababu, "MUNGU UYAUMBA MATUNDA YA MIDOMO YETU" (Isaya 57:19) na sote tunajua kinachozaliwa toka mdomoni [matunda] ni MANENO YETU...Na Mungu anasema anayaumba tu, bila kujali ni mema au mabaya, kwanini? Kwa sababu ameshalisema hilo katika NENO LAKE, HAWEZI KULIBATILISHA NENO LAKE...ANALIANGALIA APATE KULITIMIZA (Yer 1:10-12)

KWANINI MANENO YAKO YANA NGUVU?

1.UMEUMBWA KWA SURA NA MFANO WA MUNGU (Mwanzo 1:26)
Mungu amekuumba wewe kwa sura na mfano wake, na alivyo Yeye ndivyo wewe ulivyo Ulimwenguni humu (1Yoh 4:17)
Aliumba vyote kwa NENO...Alisema na ikawa...na ameweka uwezo na asili yake hiyo ndani yako...ujue ama usijue haitabadili utendaji wa KANUNI HII YA UUMBAJI!

2.WEWE NI MUUNGU, MWANA WA ALIYE JUU (Zaburi 82:6)

Ulipompokea Yesu kuwa BWANA na mwokozi wa Maisha yako ulipewa uwezo wa kuwa mwana wa Mungu (Yoh 1:12) na ili kukupa udhibitisho na uhakika, Mungu amekupa ROHO WAKE MATAKATIFU anayeshuhudia na roho yako ya kuwa wewe ni mwana wa Mungu(Warumi 8:16) na kama mtoto wa nyoka alivyo nyoka, na hata mtoto wa Mungu ni Muungu...sisi ndio watawala na wamilki wa dunia hii (Ufunuo 5:8-11) ila lazima tubadili mambo kwenye ulimwengu wa roho kwanza...kwa MANENO YETU YA USHINDI NA IMANI...TUKISHIKA SANA MAUNGAMO YETU MEMA, NA YA MEMA (Waebrania 4:14)
Aliye DHAIFU na aseme nina nguvu, aliye tasa na aseme ninao watoto wengi, aliye mgonjwa na aseme Yesu amelipia Afya yangu pale Kalvari, aliye masikini na aseme Mungu wangu atanijaza yote ninayo yahitaji kwa kadri ya utajiri wake katika utukufu katika Kristo Yesu, aliye katika kufa na aseme Sitakufa bali nitaishi nami nitayasimulia matendo makuu ya Mungu wangu!
funguka dogo, umesoma hiyo?
UMUHIMU WA KUWA MTENDAJI WA NENO

Ikiwa kuna swali kubwa ambalo linawatatanisha wakristo wengi, basi ni swali la kukua kwa imani yao ya kikristo. Wengine wanaita ni kukua kiroho kwa wakristo.

Ukiwauliza wakristo wengi ya kuwa ni tatizo gani wanaloliona kubwa, linalowakwamisha katika maisha yao ya kikristo; walio wengi watasema ni tatizo la imani.

Tatizo hili linatokea kati ya watu wa Mungu, kwa kuwa hawajui imani ni nini, na kwamba inapatikanaje. Na wengine wamekuwa wakijitahidi kuomba kwa Mungu kwa muda mrefu ili imani zao zikue, lakini bila mafanikio ya kuridhisha.

Kwani imani maana yake nini?

“Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana” (Waebrania 11:1)

Katika mstari huu tunaona mambo mawili makubwa.

Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo; na 2. Imani ni bayana ya mambo yasiyoonekana.

Imani inakupa uhakika sasa juu ya mambo ambayo unayoyatarajia. Imani inaweka wazi (bayana) mambo yasiyoonekana.

Chanzo cha imani ndicho pia chanzo cha uhakika wako katika maisha ya kikristo; pia ni chanzo cha uwazi wa mambo ya rohoni yasiyoonekana. Chanzo cha imani ndicho pia kinakupa uhakika wa maisha yako ya wokovu.

Chanzo cha imani ni nini? Imani huwa mtu anaipataje? Kwa maneno mengine unaweza ukauliza, chanzo cha uhakika ulio nao wa wokovu na ukristo ni kitu gani?

Mara nyingi watu wa mataifa huwa wanauliza maswali yafuatayo: Mtu atawezaje kuwa na uhakika wa kuokoka akiwa hapa duniani? Mtu atawezaje kuwa na uhakika ya kuwa amesamehewa dhambi wakati bado yupo duniani?

Maswali haya huwa yanatokea mara kwa mara kwa sababu hawajui uhakika wa mambo hayo unatoka wapi. Laiti wangejua, basi wangekuwa na usemi mwingine midomoni mwao juu ya wokovu.

Biblia inasema wazi kabisa kwamba yote yawezekana kwake aaminiye (Marko 9:23). Na kama biblia ambayo ni Neno la Mungu inasema yote yawezekana kwake aaminiye, mwanadamu ni kitu gani mbele za Mungu hata apinge?

Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana.

Imani chanzo chake ni nini?

“Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa Neno la Kristo” (Warumi 10:17)

Mstari huu wa biblia unatufahamisha kuwa imani chanzo chake ni kusikia Neno la Kristo. Hii ina maana ya kuwa uhakika wa wokovu, au ukristo na misingi yake unapatikana kutokana na kusikia Neno la Kristo.

Watu wengi utawasikia wakiomba na wakati mwingine kwa kufunga na kwa kuomboleza ili Mungu awape imani. Lakini mabadiliko katika maisha yao hayaonekani.

Biblia inatufahamisha wazi kabisa kuwa ‘imani chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa Neno la Kristo. Imani huja kwa Neno la Kristo. Imani huja kwa kusikia Neno la Kristo!

Watu wengi wamekuwa wakiomba imani na wanapoona haionekani katika maisha yao, wanaanza kumkemea shetani bila mafanikio yoyote. Watu wengi wanajikuta wamo katika hali ya kukwama kiroho na kudumaa kwa sababu hawajawa wasikiaji wa Neno la Kristo.

“Lakini iweni watendaji wa Neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu” (Yakobo 1:22)

Kwa mstari huu tunapata upeo mkubwa kidogo juu ya chanzo cha imani. Tunaweza sasa kusema, imani chanzo chake ni kusikia na kulitenda neno la Kristo.

Imani huja kwa kulisikia na kulitenda neno la Kristo. Uhakika tulio nao katika Njia hii ya wokovu katika Kristo unatokana na Neno la Kristo tulilolisikia na kulitenda.

Kuwa msikiaji tu wa Neno la Kristo haitoshi bila ya kuwa mtendaji wake. Neno la Kristo lililosikiwa na mtu, lisipowekwa katika matendo haliwezi kuonekana na watu wengine.

Watu wengi sana ni wasikiaji wa Neno la Kristo, utawakuta makanisani, wakiliskiliza Neno, utawakuta kwenye mikutano ya kiroho pia utawakuta kwenye semina za Neno la Mungu; lakini watendaji wa Neno hilo la Kristo wanalolisikiliza ni wachache sana.

Wasomaji wa biblia ni wengi sana, lakini watendaji wa Neno hilo wanalolisoma ni wachache sana. Na kwa sababu hii siku hizi ni vigumu sana kuweza kutofautisha kati ya mkristo na mtu wa kawaida, au mtu aliyeokoka na mtu asiyeokoka, kwa kuwaangalia matendo yao.

Mtu anajiita mkristo au ameokoka lakini matendo yake yako mbali sana na Neno la Kristo. Huu ni unafiki mkubwa – unaohitaji kutafutiwa ufumbuzi.

Wakati umefika, na wakati wenyewe ndiyo huu wa watu kujulikana maisha yao ya kikristo yamesimama katika msingi upi. Ikiwa msingi huo ni Neno la Kristo, basi neno hilo ni budi lionekane katika matendo yao ya kila siku.

Imeandikwa; “Lakini iweni watendaji wa Neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu”.

Kuwa mtendaji wa Neno la Kristo maana yake nini?

Kuwa mtendaji wa Neno la Kristo maana yake ni kuwa mtumiaji wa Neno la Kristo ulilolisikia. Kuwa mtendaji wa Neno ni kulitumia Neno na Neno nalo likutumie wewe.

Wewe unakuwa ndani ya Neno la Kristo na Neno la Kristo linakuwa ndani yako. Neno la Kristo lililondani yako unalitumia kuwa utukufu wa Mungu. Na wewe ukiwa ndani ya Neno la Kristo, unatumiwa na Neno hilo kumtwalia Mungu utukufu.

Ndiyo maana Yesu Kristo alisema;

“Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi; akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote. Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni, yakateketea. Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wanafunzi wangu,” (Yohana 15:4-8)

Kwa mistari hii tunaona kuwa imani ya kikristo ni matokeo ya mtu kuunganishwa na Kristo mwenyewe. Na matokeo ya matunda mazuri ya kikristo yanategemea jinsi ambavyo mtu anavyolisikia na kulitenda Neno la Kristo.

Pia, tunaona kuwa matokeo ya maombi ya mtu aliye mtendaji wa Neno la Kristo ni mazuri na yenye mafanikio kuliko matokeo ya mtu aliye msikiaji tu wa Neno na wala si mtendaji.

Watu wengi ni wasikiaji wa Neno la Kristo, lakini hawalitumii wala Neno haliwatumii kabisa. Na wengine ni wasikiaji na watumiaji wa Neno la Kristo katika sehemu chache tu za maisha yao.

Lakini imeandikwa wazi kabisa kuwa hao wanajidanganya nafsi zao wenyewe, wala hawamdanganyi Mungu, shetani wala mtu yeyote, bali wao wenyewe; kwa kuwa wamekuwa wasikiaji wa neno la Kristo lakini si watendaji.

Na ndiyo maana Roho wa Mungu aliomboleza kwa kupitia kwenye kinywa cha Nabii Hosea akisema; “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa ……” (Hosea 4:6)

Na Yesu Kristo, pia, alikuwa na haya ya kusema juu ya watu wa namna hiyo:

“Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu” (Mathayo 22:29)

Ni kweli kabisa kuwa kanisa ambalo ni mwili wa Kristo, limekuwa katika hali ngumu kiroho kwa sababu ya kukosa maarifa ya Mungu yanayotokana na kulisikia na kulitenda Neno la Kristo.

Imeandikwa;

“Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu. Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo.” (Yakobo 1:22-24)

Tunakumbuka wakati fulani tulikuwa tunaongea na mtu mmoja juu ya maisha yake ya wokovu. Tulimuuliza swali hili; “Ni kitu gani kinachokutofautisha wewe na mkristo mwingine wa kawaida?”

Akasema; “Ni kwa sababu nimemwamini Mungu”

Tukasema; “ Hiyo haitoshi kwa sababu hata wao wanamwamini Mungu. Je! hujasoma ya kuwa mashetani nao wanaamini na kutetemeka?”

Akauliza; “Sasa kitu gani kinacholeta tofauti?”

Tukasema; “ Ni maisha yako mapya yanayopatikana baada ya kumpokea Kristo moyoni mwako”.

Tukamsomea waraka wa pili kwa Wakorintho Sura ya tano na mstari wa kumi na saba, unaosomeka hivi; “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! Yamekuwa mapya”

Unapompokea Kristo (Neno) moyoni mwako unapewa uzima wa Mungu ndani yako, na tabia mpya inayoongozwa la Neno la Kristo.

Ni vigumu sana kumtofautisha mtu wa Mungu na mtu wa kawaida kwa kusikia wanachosema tu peke yake. Ni lazima maisha mapya ndani ya Kristo, maisha ya wokovu yaandamane na tabia mpya.

Tabia mpya hiyo haionekani siku hizi kwa sababu, watu hawajawa watendaji wa Neno. Yakobo anauliza:

“Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je! ile imani yaweza kumwokoa?.....

Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake” (Yakobo 2:14,17)

Hii maana yake mtu asipokuwa mtumiaji wa Neno la Kristo, anaonekana kama vile si mkristo. Utafahamu ni mkristo kwa sababu anakwenda kanisani jumapili au jumamosi, lakini si kwa sababu umeona matendo ya kikristo maishani mwake.

Na hata watu wengi waliookoka wanaliabisha Jina la Bwana kwa kujiita wao ni watu wa Mungu, watoto wa Mungu, wana wa mfalme, watumishi wa Bwana; kwa sababu matendo yao hayafanani na maneno wanayosema.

Yafaa nini basi, mtu kusema ameokoka wakati bado anatawaliwa na matendo ya dunia? Yafaa nini, basi mtu kusema yeye ni mkristo, wakati maisha yake yana matendo kama ya mtu asiyemjua Kristo?

“Lakini mtu atasema, wewe unayo imani, nami ninayo matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha imani yangu KWA NJIA YA MATENDO YANGU”. (Yakobo 2:18)

KWA NJIA YA MATENDO watu watajua kuwa imani yako ni ipi. Kwa njia ya matendo yako watu watajua ya kuwa wewe in mkristo au La.

Imani yako na ijulikane mbele za watu kwa njia ya kuwa mtendaji wa Neno.

Umefanyika kuwa kiumbe kipya ndani ya Kristo, kwa hiyo matendo yako ni mapya, pia, matendo ya kale yamepita. Kwa matendo yako yaliyosimama ndani ya Neno la Kristo, ulimwengu utajua ya kuwa umeokoka au La.

“Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda vema. Mashetani nao waamini na kutetemeka. Lakini wataka kujua, wewe mwanadamu usiye kitu, kwamba imani pasipo matendo haizai?....

Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa” (Yakobo 2:19,20,26)

Mashetani yanamjua Mungu ya kuwa ni mmoja, na yanaamini hivyo na kutetemeka. Mashetani yana hofu ya Mungu, lakini watu wengi hawana hofu ya Mungu ndani yao.

Kwa kutokuwa mtendaji wa Neno, unajikuta kuwa utamu wa maombi, utamu wa kushuhudia, utamu wa Neno la Mungu unafifia ndani yako.

Imani haiji kwa kuomba, kukua kwa imani yako hakutakuja kwa kuomba, bali huja kwa kusikia na kulitenda Neno la Kristo.

Si kwamba tunadharau sehemu ya maombi katika maisha ya mkristo, la hasha. Maombi ni muhimu sana kwa mkristo kama vile petroli ilivyo muhimu kwa ajili ya gari.

Ukijaza petroli kwenye gari haina faida yoyote hadi hapo utakapoingia ndani ya gari na kuliendesha toka mahali lilipo na kwenda mahali pengine unapotaka.

Maombi bila kuwa mtendaji wa Neno, ni bure. Maombi PAMOJA na utendaji wa Neno vinaleta mafanikio makubwa katika kukua kiroho. Neno ndilo linakuongoza unapotaka kusogea kiroho.

Maombi PAMOJA na utendaji wa Neno ni muunganiko wenye maana kubwa katika kuifanikisha kazi yetu tuliyotumwa kuifanya hapa ulimwenguni; kazi ya kuwa wajumbe (mabalozi) kwa ajili ya Kristo.

Lakini tunajua kuwa “sisi tu wafanyakazi pamoja na Mungu” (1Wakoritho 3:9). Kuwa mfanyakazi pamoja na Mungu maana yake ni kuwa mfanyakazi pamoja na Neno, kwa sababu Mungu ni Neno (Yohana 1:1)

Kuwa mfanyakazi pamoja na Neno maana yake ni kuwa mtenda kazi pamoja na Neno; ni kuwa mtendaji wa Neno; ni kuwa mtumiaji wa Neno.

Si kwamba watu wanapenda kutokuwa watendaji wa Neno, bali wengi hawafahamu ni namna gani ambavyo watafanya ili neno la Kristo walilolisikia au kulisoma lionekana katika maisha yao.

MUNGU awabariki sana

Comments