Viongozi wa kanisa wamshauri Rais wa Kenya asiende The Hague.


John Baptista Mugecha Karume
Askofu Mkuu wa kanisa la Africa Independent Pentecostal Church of Kenya, AIPCK, John Baptista Mugecha Karume (katikati)
Viongozi wa kanisa moja nchini wamejiunga na watu wanaomhimiza Rais Uhuru Kenyatta asiende The Hague, Uholanzi mwezi ujao wakati wa kuanza kusikizwa kwa kesi dhidi yake katika mahakama ya ICC.

WAKENYA wengi wanaendelea kumhimiza Rais Uhuru Kenyatta asihudhurie kesi inayomwandama katika mahakama ya kimataifa ya Uhalifu (ICC), huku Novemba ikikaribia ambapo Rais Kenyatta anahitajika kusafiri Uholanzi kwa kesi hiyo.

Baadhi ya viongozi na waumini wa Kanisa la African Independent Pentecostal Church of Kenya (AIPCK), katika ibada yao waliomba Rais Kenyatta asihudhurie kesi hiyo na wakamhakikishia kumuunga mkono kama kiongozi wao.

 Walisema kuwa kiongozi wa mashtaka Fatou Bensouda alikuwa anapoteza muda wa viongozi wawili wa nchi ya Kenya, Rais Uhuru na Naibu wake William Ruto, kwa kesi ambayo haina uzito wowote.
 
Wakiongozwa na Askofu Mkuu Mugecha Karume, Mwenyekiti Nchini Simon Kimani na Mwekahazina George Njuruba walisema kuwa kesi hiyo ilikuwa na mambo mengi yasiyoeleweka na hakukuwa na haki yoyote kwa kesi hiyo kuendelea.

Askofu Mkuu Mugecha aliomba Mkuu wa Sheria Githu Muigai na wakili wengine kuangalia katiba ya Kenya kwa undani ili kutoa viongozi walio humo ICC kutoka kesi hiyo.

“Wakenya walichagua Rais Uhuru kwa sababu wana imani naye, na hivyo basi kesi ya ICC inaendelea dhidi ya viongozi wa nchi kinyume na katiba ya Kenya,” walisema.

Bw Njuruba aliongeza, “Tunataka vongozi hawa wawili kuwa nchini ili wafanye kazi ambayo Wakenya waliwapatia kwa kuwachagua.”

Zaidi ya haya, walifanya dua kwa walioaga katika mkasa wa Westgate na kesi hiyo ya ICC katika ibada iliyokuwa katika Kanisa la AIPCK la Githunguri, Kiambu.

Wengine waliokuwa katika ibada hiyo ni: Naibu wa Gavana wa Kiambu Gerald Githinji, Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kiambu Nyokabi Gatheca na Mbunge wa Kiambu Mjini Jude Njomo.

Bi Nyokabi na Bw Githinji waliomba Wakenya waendelee na maombi ili nchi iwe na amani wakati wote, hata kesi za ICC zinapoendelea.

Mwishoni mwa wiki, kundi la Mururumo Mashaninani kupitia kiongozi Caleb Warari pia lilimtaka Rais Kenyatta apuuze kesi hiyo dhidi yake.

source:Gospel News media

Comments