INJILI YA KWELI LAZIMA ICHOME MOYO WENYE DHAMBI

Na Daimon Nathan

Yeremia 23 : 29 - Je! Neno langu si kama moto? Asema Bwana; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande? Waebrania 12 : 29 - Maana Mungu wetu ni moto ulao.

Leo nimekusudia kuaddress ishu hii muhimu kwa mwenendo wa kanisa kwa wakati huu. kanisa limekuwa na injili ya kubembelezana sana, watu wanataka kuhubiri kile ninachoita "upendo uliochakachuliwa" wa kuchukuliana na waovu na kubembelezana nao kwa unafiki pasipo kujua kuwa watu hawa wakiangamia roho zao zitadaiwa miongoni mwetu.

Biblia inaweka wazi katika Yeremiah 23:29, kwamba neno la Mungu ni Moto, linapoachiliwa kwa mtu, linakuja kama moto kuteketeza kila aina ya uovu na dhambi ndani ya mtu. kwa mtu wa kawaida, wa mwilini aliyeshikamana na nguvu ya dhambi na mauti, moto wa neno la Mungu ukimjia NI LAZIMA UMCHOME MOYO, kwa kuwa kwa mujibu wa Bwana Yesu, huko ndiko kutokako uovu wote umtiao mtu unajisi (Marko 7:20).

Kamwe haiwezekani mtu achomwe na moto mkali mwilini asiungue, injili ya kweli lazima ichome mioyo ya watu, Ni lazima ishughulikie dhambi, ni lazima isababishe watu kutapatapa na kutafuta msaada wa Mungu. Injili ya Petro katika Matendo ya Mitume 2 : 37 ilibeba nguvu hii, ilishughulikia dhambi ndani ya watu na kuwafanya watafute msaada wa Mungu, imeandikwa "Basi, watu waliposikia hayo, walichomwa moyo, wakawauliza Petro na wale mitume wenzake: Ndugu zetu, tufanye nini?"

Biblia katika Yeremia 23:29 inasema neno la Mungu ni kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande. Imani ni kitu hatari sana, mtu akishaamini kitu fulani ni ngumu sana kumbadilisha. inahitaji injili yenye nguvu kama nyundo kuvunja moyo wa jiwe ulio ndani ya Mtu. Elimu za kidunia zinajenga ngome za fikra kwenye akili za watu zinazowazuie wasimwamini Mungu, neno la Mungu na injili ya kweli lazima iwe na Nguvu ya kuvunja ngome hizi.

Hata siku moja haiwezekani mtu akapondwa sawasawa na ile nyundo ya kuvunjia mawe halafu asisikie maumivu. Yaani kila jumapili mtu huyo anapondwa lakini hasikii maumivu, wala havunjiki? Lazima hapo kutakuwa na tatizo, aidha hiyo nyundo ni ya sponji au mgongaji hana nguvu sawasawa. injili ya kweli ni lazima ichome mioyo ya watu, HII INJILI YA URAFIKI YA KUHUBIRIANA KUPENDANA NA WAOVU NDIYO INAYOLETA UHARIBIFU (CORRUPTION) NDANI YA KANISA KWA KUWA MAZINGIRA YA KANISA YANAKUWA RAFIKI KWA WAOVU KUSHAMIRI.

Ni lazima injili ya kweli yenye nguvu kama moto iwafanye waovu wakose raha wawapo kanisani. Ukiona injili inamfanya mchungaji apendwe na kila mtu hapo kuna tatizo. Hata Yesu mwenyewe hakupendwa na kila mtu. paulo alichukiwa na rafiki zake wale wale waliokuwa wanamtuma kuua watu baada ya kuanza kuhubiri injili ya kweli. Petro alikuwa na maadui wengi tu.
INJILI YA KWELI HAIPINDISHI WALA KUPUNGUZA UKALI WA MANENO KUWASTAHI WATU FULANI, Yesu aliwahi kumwita mtu "Mbweha" (luka 13:32) kwa sababu ya tabia zake. Amewahi kuwaambia wakuu wa makuhani machoni pao kuwa ni watoto wa ibilisi na tamaa za baba yao ibilisi ndizo wazitendazo (Yohana 8:44).

kama wewe ni mhubiri na unapendwa na kila mtu, jiulize vizuri wewe ni mhubiti kweli au vinginevyo. Haiwezekani ukasimamia kweli ya Mungu usipigwe vita, Haiwezekani ukasimamia kweni ya Mungu, Ukaihubiri injili ya kweli halafu ukapendwa na watu wote, ukihubiri injili yenye nguvu kama moto au nyundo ivunjayo, lazima watu wapondeke mioyo na watafute kumrudia Mungu.

HIYO NDIYO TAFAKARI YA LEO, BWANA NA ASEME NA WEWE SAWASAWA NA KIWANGO CHA UTUMISHI WAKO.

BARIKIWA.

By  Daimon Nathan

Comments