Rose Muhando atajwa Tamasha la Krismasi


Mwimbaji wa Injili nchini, Rose Muhando, ni miongoni mwa Watanzania watakaoimba Tamasha la Krismasi Desemba 25 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 

Mwimbaji huyo anayesikika na albamu zake mbalimbali ikiwemo ya Utamu wa Yesu, pia ataimba Desemba 26 mwaka huu kwenye Tamasha la Krismasi litakalofanyika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro. 

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Krismas, Alex Msama alisema jana kuwa hatua ya kamati yake kumalizana na Muhando imewapa faraja kubwa, kwani huyo ni miongoni mwa waimbaji ambao Watanzania wanawapenda. 

“Mungu ni mwema, kila tunalolipanga anatusaidia sana, karibu waimbaji wote ambao mashabiki wanawapenda, wamekuwa na ushirikiano mkubwa na sisi. Hawana matatizo na si watu wenye tamaa, bali wanaweka mbele kutoa huduma. 

“Tayari hivi sasa waimbaji watatu wa Tanzania tumeshakubaliana nao ambao ni Upendo Nkone, Upendo Kilahiro na huyo Rose Muhando, kwa nje tumeshamalizana na Ephraim Sekeleti. Bado tunaendelea na mazungumzo na wasanii wengine wa ndani ya Tanzania na nje ya nchi ili wote waje kutumbuiza,” alisema Msama. 

Albamu ya Utamu wa Yesu ya Rose Muhando inabeba nyimbo saba ambazo ni Utamu wa Yesu, Raha Tupu, Tamalaki, Ndivyo Ulivyo, Woga Wako, Imbeni na Kusifu na Achia. 

Mbali na Utamu wa Yesu, Rose Muhando pia amewahi kuvuma na albamu za Uwe Macho, Nyota ya Ajabu (Zawadi ya Krismasi) na Jipange Sawasawa.

Pia amepata kung’ara katika wimbo wa Vua Kiatu, alioshirikiana na Anastazia Mukabwa wa Kenya katika albamu ya Vua Kiatu, ambayo ilikuwa na nyimbo kama  Vua Kiatu, Ee Mungu, Usiwe Manamba, Nzizilela, Nishike Mkono Bwana, Wanaokudharau na Mfalme.

source:

Comments