Tusherehekee Krismasi kwa amani

WATANZANIA leo wanaungana na mamilioni ya waumini wa dini ya Kikristo ulimwenguni, kusherehekea sikukuu ya Krismasi. Sikukuu hii ambayo inaaminiwa na mamilioni ya Wakristo duniani, inaadhimishwa leo kukumbuka kuzaliwa kwake mtoto Yesu Kristo. Leo si nia yetu kuelezea historia ndefu ya kuzaliwa mtoto Yesu ambayo kwa imani za Kikristo alizaliwa kwenye zizi la kulala ng’ombe.
Tunaamini waumini hao, kwa namna moja au nyingine wamejifunza mambo mengi juu ya kuzaliwa kwa mwokozi wao, hivyo wana kila sababu ya kuonyesha furaha ya kupata mtoto.

Lakini wakati Wakristo wakiendelea na furaha hii kubwa, tumeona ni vyema tukawakumbusha mambo machache na ya msingi kwao.

Kwanza tunawataka leo na kesho wanaposherehekea kuzaliwa mtoto, kukumbuka kwamba wanayo kazi kubwa ya kuhakikisha wanasherehekea katika mazingira ya amani.

Tunasema hivyo, kwa sababu katika siku kama ya leo watu wengi wamezoea kutumia siku hii kufanya vitendo ambavyo haviendani kabisa na mapenzi ya Mungu.

Kwa msingi huo, tunaamini mahubiri yatakayotolewa leo na maoskofu, mapadre na wengine yatakuwa na ujumbe maalumu wa kuwakumbusha waumini kuishi kama ndugu.

Huu ndiyo msingi mkubwa, kwa sababu hakuna amani wala upendo kama waumini hawa wataishi bila kuwapo na uelewano, umoja na mshikamano miongoni mwao.

Tunawasihi kusikiliza kwa makini mahuburi ya leo ambayo yatakuwa na ujumbe wa kila aina.

Sisi RAI, tunapenda kutumia fursa hii kuwaasa waumini wa Kikristo kuhakikisha wanaendeleza mambo mema yote ambayo wamekuwa wakihubiriwa siku zote.

Hatutapenda kusikia baada ya kutoka kanisani na kwenda kuungana na familia zao, matukio ya ajabu, hata siku moja maandiko matakatifu hayaruhusu mambo ya aina hiyo.

Ndiyo maana tunasema leo mtoto kazaliwa, basi aonyeshwe upendo wa dhati ambao kupitia kwake utakuwa funzo kwa kila mmoja wetu.

Tunamalizia kwa kusema tunawatakia sikukuu njema, upendo, amani na umoja vitawale ndani ya Watanzania. Ndiyo sababu tunawataka Watanzania washerehekee kwa amani.


Source:Mtanzania 
 
Bali wote waliompokea(YESU KRISTO) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; -Yohana 1:12