Ushuhuda wa Uponyaji.


HISTORIA YA TATIZO NA MASHARTI YA DAKTARI:

Miaka kadhaa iliyopita nilianza kuwa na shida ya mafua makali sana yanayoambatana na chafya za mfululizo kila nikiamka asubuhi, mwanzoni nilidhani ni tatizo la kawaida tu, baada ya mda mfupi shida ikawa kubwa Zaidi na ikawa inaongezeka kila kukicha. Yaani nilikuwa pua zinawasha sana nabanwa na flu kali inayoambatana na chafya nyingi mwanzoni ilikuwa ni alfajiri baadae ikawa ni muda wote, then shida ikaongezeka nikaanza kutoka vidonda puani kwa ndani kabisa ambavyo vilipelekea kuwa na maumivu kila nikipiga chafya na pia damu na usaha kutoka nilipokuwa napiga chafya au kupenga.
Ndipo nilipoamua kwenda hospitali kuangalia shida hii inasababishwa na nini, baada ya kufanya vipimo (allergy test) nikaonekana nina Allergy ya vitu vifuatavyo: Mayai (egg white), Samaki aina zote, vumbi hasa la ndani au lililogandia sehemu muda mrefu, na flower pollen. Daktari alisema shida hiyo iko kwa kiwango cha juu sana (>1000) kwa hiyo nilitakiwa kuanza sindano aina ya Diplofos za kila mwezi; nikamuuliza daktari sasa hii ni dozi ya miezi mingapi? Akaniambia ni ya maisha yako yote, ukichoma kwa mda mrefu wa kutosha huku ukijitahidi usikutane na hivyo vitu vinavyosababisa hii allergy basi unaweza kuacha kuchoma kila mwezi na ukawa unachoma wakati tu ukiona hali inabadilika. Baada ya kutoka kwa daktari nilisema mimi kama mtoto wa Mungu sipaswi kuishi maisha ya mateso ya aina hii, kwa hiyo haikunisumbua sana akili yangu ingawa nilianza kuchoma sindano hizo.
Mwanzoni sikuwa nafuata masharti kikamilifu, kwanza kabisa kwa kuwa nilikuwa napenda sana samaki niliendelea kula samaki kama kawaida (mayai nilipunguza kula kwa sababu sikuwa nayapenda sana ingawa sikuacha), lakini pia zile sindano nilikuwa sichomi kila mwezi, nilikuwa nachoma moja na mwezi ukiisha siendi tarehe husika nakuja kwenda nikizidiwa (labda wiki moja au mbili baadaye).
Tatizo linazidi kuwa serious na ninaanza kufuata masharti:
Baada ya miezi kadhaa ya kuendelea kuvunja masharti huku nachoma sindano, tatizo lilikuwa kubwa Zaidi, pamoja na mateso nimeeleza hapo juu, ilianza shida ingine ya macho kuwasha sana sana, na yakianza kuwasha siwezi kufanya kitu chochote, hii ilikuwa inatokea sana mida ya jioni. Ilikuwa yakianza kuwasha nitaenda chumbani na nitakaa nimeyafunika macho kwa mda mrefu kwa kitambaa kisafi au wakati mwingine kitambaa kilicholowekwa kwenye maji na baada ya mda mrefu yanatulia. Nilifikiri hii ni shida ingine haihusiani na Allergy, lakini nilipoenda TMJ hospital kwa daktari wa macho aliniambia hii shida inahusiana na allergy zile zile. Pia nilianza kutoka vijipu ndani puani, nakumbuka kuna wakati kilinitoka kijipu kikubwa kikapelekea kufanyiwa operation ndogo ya pua pale TMJ; pia ikawa kila ninapoanza kupiga chafya naumwa sana kichwa hasa sehemu ya nyuma karibia na shingo.
Baada ya matatizo haya kuongezeka sasa niliona hii imekuwa serious kuliko nilivyokuwa nadhani, nikaanza sasa kufuata masharti kikamilifu ikiwa ni pamoja na kuacha kabisa kula samaki na mayai na kujitahidi kuepukana na vumbi ingawa haikuwa rahisi kuepukana na vumbi. Nilichoma hizi sindano kwa muda wa mwaka mzima lakini nilipoenda kucheki ilionekana bado nina allergy nyingi sana kwa hiyo niendelee na sindano na masharti.

JINSI NILIVYOPATA KUPONA:

Ilipita kama miaka miwili hivi bila unafuu ingawa nilikuwa naendelea kufuata masharti. Kama mtu anayemjua Mungu nilikuwa najua wazi na kuamini bila mashaka kuhusu uponyaji wa Mungu, pia nilikuwa naamini sio mpango wa Mungu niishi na tatizo hilo maisha yangu yote, hiyo ilinisaidia sana kutokuwa na wasiwasi lakini kwa upande mwingine sikuwa nimefanya uamuzi wa kuiandaa Imani yangu na kujilisha kiusahihi ili Imani ndani yangu izae matokeo ambayo kwa hakika nilikuwa najua ndio kusudi la Mungu na kwa sababu hiyo niliendelea kuteseka pamoja na kuwa na ujuzi huo. Katikati ya tatizo hilo nilianza kwenda kuabudu katika kanisa la Manna Tabernacle Bible Church kwa Pastor Carlos Ricky Wilson Kirimbai wakati naendelea kwenda kusali kila jumapili, pamoja na mafundisho mengine, mara nyingi nilikuwa nakutana na mafundisho ya Imani na kusudi la Mungu kuhusu kuishi katika afya; taratibu Imani yangu ilianza kujengeka, nikaanza kuelewa Zaidi juu ya undani wa kusudi la Mungu kuishi katika afya. Nikafika mahali Imani yangu ikawa imejengeka kiasi cha kutosha. Kwa kweli sikumbuki kwa uhakika lini niliombewa au nilijiombea kuhusu shida hii, ila ninachokumbuka ni kuwa ilifika mahali mda wa sindano umeisha siendi kuchoma na shida haipo, pia nilianza kula vitu vile nilikuwa sili, mwanzoni ilikuwa nikila samaki naanza kuhisi dalili lakini kwa sababu Imani ndani yangu ilikuwa imejengeka kiasi cha kutosha nilikuwa najua kukabiliana na dalili ikiwa ni pamoja na kukiri sawa na Neno la Mungu ambalo lilikuwa limejaa ndani yangu, na sijui ni lini hasa shida hii iliniisha jumla lakini hivi sasa nina Zaidi ya miaka miwili sina shida hiyo tena, na ninakula kila kitu.
Nikajifunza kuwa kujua kuwa Mungu anaponya na ni mapenzi yake tuishi katika afya haitoshi, ni lazima twende hatua ya ziada ya kujilisha Imani zetu na mafundisho sahihi, na pia kuchukua hatua kuhusu kile ambacho unajua ni makusudi ya Mungu uwe nacho. Pia kwa kadiri unavyoendelea kuilisha Imani yako mafundisho sahihi na kuyatendea kazi, kuna matatizo mengine utashtukia yameshaondoka hata hujui yaliondokaga lini, hicho ndio kilichonikuta mimi.
Sifa na utukufu ni kwa Yesu kwa matendo yake makuu.


Chanzo:Jesus vision
 
Bali wote waliompokea(YESU KRISTO) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; -Yohana 1:12

Comments