UTUKUFU WA MUNGU UNAPATIKANA MAHALI YESU ALIPO (Sehemu ya Kwanza)



MAANA YA NENO UTUKUFU
Siku Moja mwaka 2010, nikiwa ofisini ninatafakari neno la Mungu, Roho wa Mungu aliachilia swali hili ndani yangu. Hivi unaposema utukufu ni kwa Bwana, unaelewa maana ya neno utukufu? Nikatambua kwamba inawezekana wakristo wengi tumekuwa tukitumia neno Utukufu pasipo kuelewa maana yake ni nini. Tafakari hii ilinichukua nikaanza kutafuta kujua maana ya kawaida kabisa ya neno “utukufu” kisha baadaye kulihusianisha na Mungu. Matokeo yake ni somo hili ambalo lina kichwa “Utukufu wa Mungu unapatikana mahali Yesu alipo.”
Naomba kuweka wazi kabisa kwamba kiu ya Moyo wangu ni kukusaidia kujua kwamba utukufu wa Mungu unaweza kuonekana, ni mahali gani ambapo unaweza ukauona utukufu wa Mungu, na kwa nini ni Muhimu kwa mtoto wa Mungu kuuona utukufu wa Mungu

MAANA YA KAWAIDA YA NENO UTUKUFU
Neno Utukufu, linalotumiwa katika lugha ya Kiswahili linatafsiriwa katika lugha ya kiingereza kama “Glory” neno hili katika kamusi limehusianishwa (synonym) na maneno kama RADIANCE yenye kutafsiriwa katika Kiswahili kumaanisha “ang’avu/enye kudhihirisha wazi upendo/furaha”, MAGNIFICENCE ambalo katika Kiswahili limetafsiriwa kumaanisha “adhimu/enye adhama/enye uzuri kabisa.” SPLENDOR ambalo linamaanisha “fahari/ubora wa hali ya juu” WONDER, hii ikimaanisha ajabu/enye kustaajabisha, BRILIANCE ikimaanisha enye akili sana/enye pande nyingi, CREDIT ikimaanisha heshima/Muamana/sifa njema, FAME ikimaanisha umaarufu/kufahamika/kujulikana/sifa njema, LAURELS ikimaanisha ufahamu/ujuzi wa namna ya kuwashinda washindani/mafanikio aliyopata mtu/heshima au sifa inayochungwa sana, STARDOM ikimaanisha kuwa kinara au nyota
Kwa tafsiri rahisi kabisa tunaweza kusema kwamba manemo yote haya kwa ujumla wake yanawakilisha mawanda (Scope) ya kile kinachoitwa utukufu.

UTUKUFU WA MUNGU
Tunapoyatafakari maneno yaliyoainishwa na kuyahusisha na Mungu hasa kwa habari ya kutafakari utukufu alionao Mungu, ni muhimu kuweka wazi kwamba Mungu ni wa milele, kina chake ni cha milele, itatugharimu milele kupata kumwelewa Mungu katika ukuu wake. Maneno haya hayatoshi kueleza maana ya utukufu wa Mungu, ila yanatuwekea msingi wa kutambua mawanda ya utukufu wa Mungu; hivyo kwa kwa maneno haya utukufu wa Mungu unaweza tafsiriwa kuwa jumla ya;
• Mng’ao au udhihirisho (Radiance) wa wazi kabisa wa Upendo, Furaha na Amani ya Mungu katika Kristo Yesu mahali watoto wa Mungu walipo.
• Ni kudhihirika kwa uzuri/wema wa Mungu unaovuta watu kumrudia Mungu na kushuhudiwa na kila mtu anayekuwa kwenye uwepo wa Mungu
• Ni kudhihirika kwa Fahari/Ubora unaoambatana na uwepo wa Mungu kila mahali anapopita. Mungu ni Mfalme wa dunia yote, uwepo wake huendana na fahari/ubora na ule ukuu wa kifalme unaodhihirika katikati ya watoto wake.
• Ni kudhihirika kwa akili au maarifa ya Mungu/Pande tofauti za maarifa ya Mungu zinazoudhihirisha uweza wa Mungu katikati ya watoto wake.
• Ni kudhihirika kwa ajabu za Mungu au matendo ya kustaajabisha yanayoambatana na uwepo wa Mungu miongoni mwa watoto wake
• Ni kudhihirika kwa Heshima/sifa njema na Imani inayoambatana na uwepo wa Mungu ambayo huwa ni muamana kwa watu wote waliopo uweponi mwa Mungu.
• Ni kudhihirika kwa ukuu wa Mungu kunakomfanya Mungu ajitofautishe na kila kiumbe na kujionesha kuwa ni wa pekee hivyo kuwa kinara, kuinuliwa na kutukuzwa ba watu wote waliopo uweponi mwake ambao hushuhudia kuwa yanayotokea ni matendo makuu ya Mungu na si vinginevyo
• Ni udhihiriso wa hekima, maarifa na ujuzi alionao Mungu unaompatia ushindi wakati wote dhidi ya falme na mamlaka za giza. Ni kudhihirika kwa shangwe za ushindi anaojipatia Mungu dhidi ya shetani na kazi zake.

Utukufu wa Mungu ni kitu kinachotembea na Mungu popote aendapo, utukufu wa Mungu huudhihirisha uwepo wa Mungu. Utukufu wa Mungu ni suala la ufunuo, ni matokeo ya kusudi la Mungu kutaka kujifunua kwa watoto wake ili wapate kumjua zaidi na kuzielewa njia zake. Mtu anapofanikiwa kuuona utukufu wa Mungu anapata neema ya kumjua Mungu zaidi na kuzielewa njia zake.
Katika kitabu cha Kutoka 33:13 na 18 tunaona ukweli wa jambo hili katika maombi ya Musa akimwomba Mungu na kusema;
“Basi, sasa nakuomba, ikiwa nimepata neema mbele zako, unionyeshe njia zako, nipate kukujua, ili nipate neema mbele zako; ukakumbuke ya kuwa taifa hilo ndilo watu wako.”
Tamanio la Musa ilikuwa ni kumjua zaidi Mungu, apate kujua jinsi ya kutunza uwepo wa Mungu ili apate neema mbele za Mungu ya kumfanikisha kuwaongoza wana wa Israel. Anaomba zaidi katika mstari wa 18 akisema “Nakusihi unionyeshe utukufu wako.” Mungu anamjibu Musa katika Kutoka 33:19-22 kama ilivyoandikwa;
…Nitapitisha wema wangu wote mbele yako, nami nitalitangaza jina la Bwana mbele yako; nami nitamfadhili yeye nitakayemfadhili; nitamrehemu yeye nitakayemrehemu. Kisha akasema, Huwezi kuniona uso wangu, maana mwanadamu hataniona akaishi. Bwana akasema, Tazama, hapa pana mahali karibu nami, nawe utasimama juu ya mwamba; kisha itakuwa wakati unapopita utukufu wangu, nitakutia katika ufa wa ule mwamba, na kukufunika kwa mkono wangu hata nitakapokuwa nimekwisha kupita"
Katika habari hii kuna mambo kadhaa ya msingi ya kujifunza kama ifuatavyo;
• Mwanadamu wa kawaida aaliye chini ya laana ya dhambi na mauti, hawezi akamwona Mungu akaishi, Mungu ni mtakatifu sana na macho yake hayawezi kuitazama dhambi asiiadhibu. Ni kwa sababu hii Mungu anapokuja katikati ya wanadamu hajidhihirishi jinsi alivyo kwa kujionesha katika ulimwengu wa Mwili damu na nyama, bali yeye hudhihirisha sifa zake (attributes) kama wema, Rehema, fadhili ambazo ni sehemu ya utukufu wake ili watu wapate kumjua na kutambua uwepo wake.
• Kudhihirika kwa attributes /sifa za Mungu ni dalili inayoonesha Mungu yupo mahali fulani kwa kuwa attributes/sifa za Mungu haziwezi kutengwa na Mungu, ni sehemu kamili ya utukufu wa Mungu inayokwenda naye kila alipo.
• Attributes /sifa za Mungu ndicho kitu pekee tunachohitaji kukiona katika ulimwengu huu ili tupate kuutambua uwepo wa Mungu, kumjua zaidi Mungu na kupokea neema mbele zake. Utukufu wa Mungu ni jumla ya sifa zote (attributes) za Mungu zinazomfunua Mungu jinsi alivyo na kuwawezesha wanadamu kuzijua njia za Mungu.
• Kudhihirika kwa attributes (sifa) za Mungu ni alama kuu ya Rehema za Mungu kwa watu wake, inaashiria jitihada ya Mungu kuwarehemu watu wake wasiangamie uweponi mwake kwa dhambi zao. Sifa kuu ya kwanza inayodhihirika kama sehemu ya utukufu wa Mungu akishuka mahali ni Rehema zake kama ilivyokuwa kwa Musa (Kutoka 34:5 -7 imeandikwa; “Bwana akashuka ndani ya lile wingu, akasimama pamoja naye huko, akalitangaza jina la Bwana. Bwana akapita mbele yake, akatangaza, Bwana, Bwana, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli; mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi; wala si mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe; mwenye kuwapatiliza watoto uovu wa baba zao, na wana wa wana wao pia, hata kizazi cha tatu na cha nne.”)
• Ni vigumu kwa mtu kuweza kuona utukufu wa Mungu asipofunuliwa na Roho wa Mungu, Inahitaji akili iliyohuishwa kwa neno la Mungu kuweza kupokea ufunuo wa utukufu wa Mungu kama unavyodhihirishwa na sifa (attributes) za mungu zinazoonekana pale Mungu alipo.

ITAENDELEA ..........USIKOSE SEHEMU YA PILI

By Daimon Nathan



 Bali wote waliompokea(YESU KRISTO) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; -Yohana 1:12