UTUKUFU WA MUNGU UNAPATIKANA MAHALI YESU ALIPO (Sehemu ya Pili)

Na Daimon Nathan


UNAWEZAJE KUUONA UTUKUFU WA MUNGU?
Tunapoanza kujibu swali hili la msingi sana, ninapenda kukuhakikishia kwamba ni makusudi ya Mungu watoto wake wote wapate kujua kuuona utukufu wake ili wapate kuzijua njia zake. Hii ndiyo sababu Mungu aliamua kuudhihirisha utukufu wake katika mfano wa mwanadamu Yesu Kristo mwana wa Mungu aliyemtoa kwa anjili ya ukombozi wetu. Yohana 1:14 inashuhudia jambo hili kama ilivyoandikwa “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli”
Napenda kusisitiza tena zaidi katika sehemu hii kwamba Utukufu wa Mungu ni jambo la ufunuo linaloratibiwa na Roho Mtakatifu, hivyo ni vigumu kwa mtu asiyeokoka kuuona utukufu wa Mungu kwa kuwa imeandikwa katika 1Wakorintho 2:14 “Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni.” Lakini pia imeandikwa katia 1Wakorintho 2:12 “Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu.”
Ni dhahiri Mungu anataka tumjue, na ni kwa sababu hii ametupa Roho wake ili apate kutufunulia siri na mafumbo ya Mungu. Sifa ya kwanza inayomwezesha mtu kuuona utukufu wa Mungu ni kuwa ndani ya Yesu Kristo, yaani kuokoka na kufanyika kiumbe kipya, chenye roho na akili iliyohuishwa kwa neno la Mungu ili kuweza kuyatambua na kuyaelewa Mambo ya Mungu.
Katika injili ya Yohana 17:22 na 24 Bwana Yesu amenukuliwa katika maombi yake akisema maneno yafuatayo; “Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja.” “Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami po pote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu.”
Ndani ya maneno haya kuna siri nzito sana inayohusiana na udhihirisho wa utukufu wa Mungu kati kati ya wana wa Mungu, ninapenda kukuonesha mambo kadhaa ambayo Roho wa Bwana amenifundisha katika mistari hii kama ifuatavyo;
• Ile Jumla ya utukufu wote aliokuwa nao Bwana Yesu, kwa kiwango alichopewa na Baba tangu kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu, sawasawa na ulivyoshuhudiwa na Yohana (Yohana 1:14) Mungu ametupatia sisi, yaani wale waliompokea Yesu uwa Bwana na Mwokozi wa maisha yao na kufanyika watoto wa Mungu bure kabisa, unachohitaji ni Imani yako tu.
• Utukufu huu tuliopewa na Mungu ni jambo ambalo tunaliakisi kutoka kwa Yesu kristo Mwana wa Mungu. Ni mfano wa uhusiano uliopo kati ya Jua na Mwezi, Pasipo kuwepo Jua mwezi hupoteza Nuru yake, kwa kuwa Nuru ya mwezi inaakisiwa kutoka katika Jua. Kwa kadiri Mwezi unavyokuwa mbali na mzunguko wa jua ndivyo nuru yake huzidi kuwa hafifu, kadhalika kwa kadiri mwezi unavyokuwa karibu na mzunguko wa Jua ndivyo nuru yake inavyozidi kuwa angavu. Ukaribu wetu tulio nao na Yesu Kristo mwana wa Mungu ndio unaowezesha mng’ao wa utukufu wa Mungu katikati yetu kuonekana, kadhalika tunapokuwa mbali na Yesu kristo mwana wa Mungu ndivyo tunavyopoteza ile nuru ya mng’ao wa utukufu wa Mungu katika maisha yetu.
• Ukaribu wetu na yesu kriso Mwana wa Mungu ni jambo linalowezekana ikiwa tutatembea na kuwa naye popote alipo (Yohana 17:24), na si yeye kutemmbea na sisi na kuwa na sisi popote tulipo. Tofauti ya sisi kutembea na yesu, na yesu kutembea na sisi ni hii. Sisi tunapotembea na Yesu; Yesu ndiye mwenye maamuzi ya wapi anataka kwenda na nini anataka kufanya, na sisi tunamfuta kwa vipaumbele vyake. Kwa upande mwingine, Yesu anapotembea na sisi maana yake ni kwamba sisi ndio wenye mipango na maamuzi ya wapi tunataka kwenda, na Yesu anatufuata na kutusaidia katika lile tunalomhitaji.
• Pasipo kufunuliwa, kuutazama na kuuona utukufu wa Yesu kristo mwana wa Mungu unaodhihirika kila siku katikati yetu tukiwa karibu na Kristo, haiwezenani sisi kutembea katika kiwango cha utukufu tuliopewa na Mungu. Kupanda toka ngazi moja ya utukufu na kwenda nyingine ni matokeo ya sisi kuutambua utukufu alionao Yesu kristo mwana wa Mungu kama ilivyoandikwa katika 2Wakorintho 3:18 “Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana, aliye Roho.
• Kudhihirika kwa utukufu wa Mungu katikati yetu ni matokeo ya upendo wa Mungu kwetu. Ni katika upendo huo biblia inaweka wazi kwamba Mungu alimtoa mwanawe wa pekee kwa ukombozi wa ulimwengu (Yohana 3:16). Akisha kumtoa Kristo kwa ukombozi wetu, Mungu ametupa kufanyika wana wa Mungu (Yohana 1:12), tena katika waraka wa kwanza wa Yohana 2:1 imeandikwa “Tazameni ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; NA NDIVYO TULIVYO. Maana yake ni kwamba kiwango kile kile cha utukufu alionao Bwana Yesu ndicho kinachopaswa kuonekana katika maisha yetu, pasipo kufunuliwa na kuona utukufu alionao kristo ni vigumu kwa jambo hili kudhihirika kwetu.
• Utukufu wa Mungu katikati yetu unadhihirishwa na zile attributes/sifa zinazoonesha uwepo wa Mungu katikati yetu. Kufunulia kwa sifa hizi kunatuwezesha kumjua zaidi Mungu, hatimaye sisi pia kubadilishwa na kuzidhihirisha sifa hizo popote tunapokuwa. Kwa kadiri tunavyozidi kuwa karibu na Yesu na kufunuliwa attributes za Mungu ndivyo tunavyozidi kubadilishwa tufanane naye hivyo kutimiza andiko lisemalo tunabadilishwa tufanane nay eye toka utukufu hadi utukufu.

Usikose sehemu ya tatu...

By Daimon Nathan


Bali wote waliompokea(YESU KRISTO) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; -Yohana 1:12