Waumini wa huduma ya Mtakatifu Prince Mission yenye Makao Makuu yake
Sinza jijini Dar es Salaam, wameomba msamaha kwa Mungu kwa baadhi ya
viongozi wa umma kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kuusaliti umma
wanaoungoza.
Hatua hiyo inatokana na matumizi ya misahafu wanapokula viapo vya
kuutumikia umma, kisha kutotimiza azma hiyo badala yake kujinufaisha
binafsi na ‘kuwaangamiza’ raia wanaowachagua.
Kiongozi huyo wa kiroho, Nabii Cres1, aliwaambia waumini hao
wanaojulikana kwa jina la Wateule katika ibada iliyofanyika mapema
wiki jana kuwa, watu wengi wamekuwa wakiapa bila kujua madhara
yanatokana na viapo hivyo.
“ Viapo vingine vinasababisha mahangaiko makubwa, na hii inatokana
kukosa uaminifu binafsi, wapo wanaohangaika kwa ajili ya hilo, tumuombe
Mungu atuondolee adhabu hiyo,” alisema akiwalenga viongozi hao.
![]() |
Kiongozi wa kiroho, Nabii Cres1 |
Alisema, baadhi ya viongozi wa serikali duniani, wanaapa katika
maeneo mbalimbali kwa kutumia vitabu vitakatifu ambavyo ni neno la
Mungu, kuwa watenda kwa mujibu wa haki sawa na maslahi kwa watu wote,
lakini wanapomaliza inakuwa kinyume chake.
“Baadhi yao wanaapa kuwa watalinda mali za wananchi, watatenda haki,
lakini badala yake wanatenda tofauti na wengine wakijitajirisha wao na
familia zao, jambo ambalo ni dhambi mbele za Mungu,”alisema.
Nabii Cres1, alisema miongoni mwa matendo yaliyo kinyume na viapo hivyo,
ni kwa baadhi ya viongozi kuishi maisha ya kuhangaika moyoni na kukosa
amani, kuondokewa na mvuto wa kupendwa na wananchi, pamoja na kuwa ana
mali nyingi.
“Wengi unakuta wanaapa huku wakijua hawataweza kutenda kama
walivyoaapa. Inatakiwa kuwaombea msamaha kwa Mungu kwani viapo visivyo
vya dhati huleta madhara kwa jamii mzima,” alisema.
Aliongeza, “inakuwa laana kwa taifa, kama tunapenda dunia ipone, lazima
tuombee viongozi wote walioko madarakani, kuanzia ngazi ya juu hadi
familia ili Mungu awawezeshe watende mema na kuzingatia viapo vyao kwa
ustawi wa taifa letu na jamii kwa ujumla.”
CHANZO: NIPASHE
CHANZO: NIPASHE