Jaji Augustino Ramadhani akiingia katika Kanisa la Anglikana Zanzibar 
kuendelea na huduma za kutangaza neno la Mungu.Picha Salim Shao 
            
      
                
    
    
        
            
Baba wa Taifa 
alipendelea sana kuitwa Mwalimu, kazi aliyoanza kufanya kabla ya kuwa 
Rais wa kwanza na hadi anastaafu urais jina la Mwalimu hakuliacha hadi 
mauti yalipomkuta.
                
              
Hii inakuwa ni vigumu kwa mtu aliyetumikia nafasi 
nyingi kwa nyakati tofauti na kwa mafanikio mazuri, nasema mazuri kwa 
sababu Jaji Augustino Ramadhani aliyestafu Ujaji Mkuu alipaswa pia 
kuitwa Brigedia Jenerali kwa kuwa pia alilitumikia Jeshi hadi kufikia 
ngazi hiyo ya Brigedia Jenerali kabla ya kuitwa katika sekta  ya sheria 
na kutumikia Mahakama hadi kufikia ngazi ya juu kabisa ambayo pia wengi 
hupenda kuandikwa kwa vyeo walivyowahi kutumikia na kwa sasa amepewa 
kazi ya ukasisi.
                
              
Mbali na kustaafu ujaji, wiki iliyopita alipewa 
kazi ya ukasisi, alitawazwa rasmi kuwa Mchungaji wa Dayosisi ya Kanisa 
la Anglikana lililopo Mkunazini Zanzibar  na hivyo kustahili kuitwa cheo
 cha Mchungaji Augustino Ramadhani.
                
              
Mchungaji Augustino aliiambia Mwananchi kuwa 
alizaliwa Visiwani Zanzibar, Mtaa wa Kisima Majongoo kwenye familia ya 
watoto wanne wa Mwalimu Mathew Douglas Ramadhani na Bridget Anna 
Constance Masoud akiwa ni mtoto wa pili katika familia hiyo, aliishi kwa
 miaka mitatu Visiwani huko na kisha alikuja Tanzania Bara (Tanganyika) 
akiwa na umri wa kuanza masomo hadi alipohitimu  masomo ya sekondari 
katika Shule ya Wavulana Tabora na wakati akiwa sekondari ndipo 
alilpojifunza kupiga kinanda akirithi kipaji cha babu yake Augustino 
Ramadhani.
                
              
Jaji Ramadhani alihitimu elimu ya sekondari mwaka 
1965 na kujiunga na elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam 
katika fani ya sheria hadi mwaka 1970 alipojiunga katika Jeshi la 
kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria, baadaye aliajiriwa katika Jeshi la 
Ulinzi la Wananchi (JWTZ) alikofanya kazi za sheria.
                
              
Mafanikio zaidi
                
              
Alifafanua kuwa aliitwa na aliyekuwa Rais wa pili 
wa visiwa hivyo, Alhaji Aboud Jumbe mwaka 1978 na kumteua kuwa Naibu 
Jaji Mkuu kabla ya kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar na mwaka huo huo aliitwa 
tena jeshini kwa ajili ya kushiriki vita ya Kagera, alipelekwa Uganda na
 kukaa kwa zaidi ya miezi kumi.
                
              
Baada ya vita kumalizika alirudi Tanzania 
kuendelea na kazi katika sekta ya Sheria na mwaka 1980 aliapishwa kuwa 
Jaji Mkuu wa Zanzibar.
                
              
Anasema, mfumo wa Mahakama  Visiwani haukuwa wa 
kisheria na alifanikiwa kuubadilisha na kuweka mfumo wenye ngazi za 
Kimahakama kutoka Wilaya,  Mkoa hadi Mahakama Kuu. Anabainisha kuwa hii 
ilitokana na kutokuwepo na watu waliosomea sheria ili kuajiriwa katika 
sekta ya sheria.
                
              
“Nilifanikiwa kuondoa mfumo wa mabaraza (Peoples 
Court) na kuweka mfumo wa mahakama uliofuata ngazi za kimahakama na 
mahakama ya Rufaa haikuwepo kabisa”, anasema.
                
              
Pia aliapishwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa 
mwaka 1989, mwaka 1990 alihamia jijini Dar es Salaam na Mwaka 1993 hadi 
2003 aliteuliwa pia kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Tanzania 
Bara na mnamo mwaka 2002-2007  aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya 
Uchaguzi Zanzibar na katika kipindi hicho hicho alikuwa mmoja wa Majaji 
sita wa Mahakama ya Afrika Mashariki, pia alikuwa ni mmojawapo wa Majaji
 11 waliochaguliwa na Marais wa Afrika kwa ajili ya kuitumikia Mahakama 
ya Afrika ya Haki za Binadamu na ndipo mwaka 2006 alipoteuliwa na Rais 
Jakaya Kikwete kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania.
                
              
Baada ya kustaafu kazi ya Ujaji Mkuu mwaka 2010, 
Jaji Augustino Ramadhani alikataa kuendelea na kipindi kingine baada ya 
kufanikiwa kufafanua kifungu kinachokataza Jaji kuendelea na kazi ya 
Ujaji baada ya umri wake wa kustaafu na kuendelea kwa  mkataba  wa 
ajira, ila anaruhusiwa kuongeza kipindi kimoja tu hata kama bado anazo 
nguvu za kutumikia Taifa.
Bali wote waliompokea(YESU KRISTO) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; -Yohana 1:12
Mara baada ya kusimikwa kuwa Mchungaji anasema,  hakuna tofauti 
kati ya kazi ya Mahakama na kazi ya  Uchungaji kwani zote ni kazi za 
kufanya maamuzi ya watu wanaodai wapatiwe haki na kubainisha kazi za 
mahakama ukiamua umeamua ila za kanisa zinataka makubaliano na 
maridhiano japo zote ni kazi za Mungu.
                
              
“Kazi hii ya uchungaji mimi sikuifikiria hata siku
 moja kwamba nitaifanya ingawa nilisomea nchini Uingereza  na kutunukiwa
 stashahada. Pia nilikuwa nikishiriki katika shughuli za madhabahuni 
hasa wakati wa kuwasimika maaskofu kwa kuwa nilikuwa mwanasheria wa 
kanisa hili hadi nilipoteuliwa kuwa Jaji Mkuu ndipo nilipoamua kuacha 
wadhifa huo ili kuepuka migongano,”anasema Jaji Ramadhani.
                
              
Atafutwa
                
              
“Askofu alinifuata mara kwa mara ingawa nilikuwa 
nikimkatalia lakini mwisho nilikubali kwa kuona kuwa ni sauti ya Mungu 
iliyokuwa ikiniita kupitia kwake na ndio  leo hii baada ya kutumikia 
ushemazi kwa zaidi ya miezi sita  nimesimikwa rasmi kuwa mhudumu wa 
madhabahuni.”
                
              
Kwa upande mwingine Jaji anasema, lengo lake 
lilikuwa baada ya kustaafu akafundishe na lengo hilo limetimia kwani pia
 kwa sasa ni  Makamu Mkuu wa Chuo cha Tumaini Iringa anapofundisha 
sheria.
                
              
Pia itakumbukwa kuwa wiki hii amekamilisha kazi ya
 kuunda rasimu mpya ya katiba alipoteuliwa mwaka jana kuwa Makamu 
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Tanzania.
                
              
Hali ya Zanzibar
                
              
Akizungumzia hali ya vugu vugu la hali ya visiwani
 humu kuhusu kushambuliwa kwa viongozi wa dini na kuharibiwa kwa nyumba 
za ibada anasema tangu miaka ya nyuma akiwa mdogo anakumbuka jinsi 
walivyokuwa wakishirikiana vizuri na majirani zao kuadhimimisha sikukuu 
za kidini bila kujali tofauti ya za dini.
                
              
“ Nakumbuka wazazi wangu walikuwa wanamwita 
Mwislamu kuja kuchinja kuku ili wasikwazike wanapokaribishwa kujumuika 
katika chakula, kwa kuwa walijua kuwa nyama wanayokula  imechinjwa kwa 
taratibu za dini yao na haitamkwaza na wao pia walikuwa wakitualika 
kwenye sikuku zao na tulikuwa tukifurahia pamoja.”
                
              
Mwananchi pia ilishuhudia amani iliyokuwepo wakati
 misa ya kumwapisha Jaji Mstaafu Augustino Ramadhani ilipokuwa 
ikifanyika na hakuwa na uvunjivu wa aina yoyote ya amani licha kuwepo na
 ulinzi wa kawaida na hakukuwa na Polisi  kama ilivyokuwa wakati wa 
mkesha wa Siku Kuu ya Krismasi.
                
              
Wageni walikuwa wengi na kanisa lilijaa watu waliokuja kushuhudia tukio hilo la kusimikwa kwake.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
Comments