Cecilia Ricardo, binti aliyepofuka macho akiwa mdogo, aliyetamani kujiua
Ilikuwa mwaka 2011 mwezi wa saba katika eneo la
Visole Manispaa ya Morogoro, Cecilia Ricardo anasema kuwa wakati huo
akiishi kwa dada yake, Theresia Patrick Ricardo alimtuma mtoto wa dada
yake, Evodia kwenda dukani kununua sumu ya kuua panya ili anywe kwa
lengo la kujiua, maamuzi hayo alichukua kutokana na mateso yaliyotokana
na maumivu makali ya macho ambayo baadaye yaliyopoteza kabisa uwezo wa
kuona hadi leo.
Zilikuwa siku nne za mateso makali ya maumivu
ikiambatana na maumivu ya kichwa mfulululizo na macho kutoka maji, hali
ambayo ilimshawishi kumtuma mtoto aende dukani kununua sumu ya panya ili
kujiua.
Hata hivyo mtoto huyo alifichua siri hiyo kwa kaka
aliyekuwa nje na kunyang’wa fedha na kwa sababu hakuwa na uwezo wa
kuona mbinu yake ya kuijua iliishia hapo, anasema Cecilia katika
mahojiano na mwandishi wa makala haya eneo la Madizini Kilakala mkoani
Morogoro.
Cecilia anaeleza namna mkasa huo ulivyomtokea
baada ya kutoka katika mji mdogo wa Turiani Wilaya ya Mvomero mwezi
mmoja baada ya kufika kwa dada yake Manispaa ya Morogoro kwa lengo la
kujipumzisha huku akiwa amebeba kiasi cha fedha Sh30,000 fedha alizopata
kutokana na mradi wa kuuza maji baridi.
Baada ya kuishi Morogoro Mjini kwa muda wa mwezi
mmoja aliona upo umuhimu wa kuwasiliana na familia iliyoko Turiani hivyo
njia pekee ya kuwasiliana nao ni kununua simu ya kiganjani ndipo
alipomwambia dada yake kumpeleka mjini ili akanunue yenye uwezo wa
kuweka nyimbo ili kuweza kupata nafasi ya kuweka nyimbo za injili.
“Nilinunua simu dukani na kwenda kusajiliwa lakini
nilimwomba dada niwekewe nyimbo za injili ikiwa njia moja wapo ya mimi
kuniriwaza pindi ninapokuwa na mawazo juu ya maisha yangu hasa baada ya
kupoteza kabisa uwezo wa kuona,” anasema Cecilia huku akiwa mwenye
furaha na kuonyesha tabasamu.
Anasema kuwa wakati wamefika eneo la kibanda cha
kuweka nyimbo katika simu yake, Cecilia alichagua nyimbo nyingi za kwaya
ya Kanisa la Katoliki, jambo hilo lilimpa mshangao mmiliki wa kibanda
hicho, Noah Mgeni na kuhoji kwa nini dada huyo amekuwa akitoa masharti
ya kutoingiza nyimbo nyingine tofauti na nyimbo za injili tu.
Theresia Patrick Ricardo dada mkubwa wa Cecilia
alimwondolea mshangao huo Noah kwa kumweleza kuwa huyo mdogo wake ni
mlemavu wa macho (haoni kabisa) na hapo kabla ya kupata ulemavu huo
alikuwa mwanakwaya hivyo njia pekee ya kujiliwaza kutokana na ulemavu
huo ni kusikiliza nyimbo za kwaya.
Noah aliendelea kuhoji je, anaweza kuimba na
kucheza licha ya kuwa mlemavu... Kama anaweza basi mimi nitamuunganisha
na mtu ili aweze kutumbuiza katika kumbi za sherehe za harusi, kipaimara
na kadhalika.
“Baada ya kugundua Cecilia kuwa ni mlemavu wa
macho, nilimwomba namba yake ya simu ili nimuunganishe na yule mtu
ambaye niliamini angeweza kumsaidia,” anasema.
Noah anaeleza kuwa baada ya kupata namba ya simu
ya Cecilia alimpigia na kufunga safari ya kumtembelea nyumbani kwa dada
yake Visole ambako alikuwa anaishi
kwa lengo la kumfahamu zaidi na hilo alilifanya na
kumvutiwa naye huyo dada kwa sababu yeye ni msanii na alikuwa anaigiza
kucheza muziki wa injili kama mlemavu wa macho.
Bali wote waliompokea(YESU KRISTO) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; -Yohana 1:12
“Baada ya kuonana naye Cecilia kwa mara ya pili nyumbani kwao,
nilimshauri kuwa kutokana na umbo alilokuwa nalo, ni vizuri zaidi kama
atakuwa anacheza, naye akakubali,” anasema.
Noah alisema kuwa alianza kumfundisha kucheza,
wimbo wa kwanza ni ule wa wasanii wa muziki wa injili kutoka nchini
Burundi wa kwaya ya Ambasado kupitia wimbo wa kwetu pazuri na aliweza
kumudu vema kucheza kwa hisia jambo ambalo yeye Noah alikuwa analitaka.
“Mimi ni msanii na ninacheza katika sherehe
mbalimbali zikiwemo harusi, nacheza nyimbo za injili tu na kuigiza kama
mtu nisiyeona na wageni waalikwa hunitunza fedha, lakini nilipogundua
Cecilia ni mlemavu wa macho niliona bora nafasi hiyo awe anacheza yeye
kwa uhalisia tofauti na mimi hicho ndicho chanzo cha binti huyu kuingia
fani ya kucheza muziki”anafafanua Noah.
Cecilia Joseph Ricardo anasema mawazo ya kutaka
kujitoa uhai kwa kunywa sumu ya panya kwa sasa hayapo tena katika kichwa
chake, ni kutokana na ushawishi wa Noah Mgeni ambaye amembadilisha kwa
kumwingiza katika fani ya muziki.
“Sasa hivi nimepata faraja kubwa kupitia muziki wa
nyimbo na nimekuwa nikicheza show katika sherehe za harusi na wasamalia
wema wamekuwa wakinitunza fedha ambazo natumia katika kuendesha maisha
yangu mwenyewe bila utegemezi wowote kutoka kwa wazazi wangu akiwemo na
dada yangu na nina amani sana moyoni na huu upofu ni kama makusudi yake
katika mitihani kama binadamu wengine” anasema Cecilia.
Kuna aina nyingi za ulemavu na kukumbwa na
changamoto mbalimbali katika jamii inayoizunguka lakini wapo ambao
wanaweza kufanya jambo la kuweza kuendesha maisha yao wenyewe bila
kuhitaji utegemezi labda kuwezeshwa nyenzo tu na mambo mengine kufanya
wenyewe hilo linawezekana endapo kutakuwa na mtu wa kukushika mkono,”
anafafanua.
Hali ilivyokuwa awali
Cecilia anasema kuwa yeye kabla ya macho yake
kupoteza kabisa nuru ya kuona alikuwa na malengo mengi kama binadamu
wengi na kati ya malengo hayo ni kuwa mtawa; enzi za utoto wake alikuwa
mwimbaji katika kwaya ngazi ya shule na kanisa Katoliki.
Amekuwa akipenda wasanii wakubwa wa nyimbo za
injili wakiwemo Christina Shusho hasa kupitia wimbo wake wa Nipe Macho,
Anastazia Mkobwa katika wimbo wa Nishike mkono na Ambasada wimbo wa
kwetu pazuri.
Alivyopata ulemavu
Akiwa na umri wa miaka 10 akisoma darasa la tatu
shule ya msingi Mtibwa wakicheza mchezo wa kujaza mchanga kwenye chupa
ya soda na wenzake saa 7 mchana siku ya jumamosi eneo la kanisa la
Anglikana, mtoto Ambe Oden alirusha mpira wakati yeye Cecilia Ricardo
akijaza mchanga huku amekaa chini katika chupa, alikwepa mpira huo na
uso wake kugonga katika mdomo wa chupa katika jicho lake la kushoto.
Cecilia anasema kuwa baada ya kuinamisha uso wake
wakati akikwepa mpira uliorushwa na Ambe Oden na kujibamiza katika jicho
la kushoto, aliona nyota nyingi usoni katika macho yote na maumivu
makali na mchezo uliishia hapo. Baadaye wenzake walimshika mkono na
kumrudisha nyumbani huku macho yakipoteza nuru ya kuona, na maumivu
makali.
Baada ya dakika 10 baadaye macho yake yalirejea katika hali yake
ya kawaida na kuanza kuona huku yakiwasha na maumivu yalidumu kwa siku
mbili na macho yakiwa yamevimba, anafafanua.
Siku ya tatu tangu apate tatizo hilo alipelekwa
hospitali ya misheni ya Bwagala Turiani, hiyo ilikuwa mwaka 2000,
alipimwa na kugundulika kuwa ana presha ya macho na kutakiwa kufanyiwa
operesheni.
Alilazwa kwa siku mbili na siku ya tatu hatimaye
alifanyiwa operesheni katika jicho la kulia badala ya kushoto na siku ya
saba baada ya kufanyiwa operesheni alirejea nyumbani na kuendelea na
masomo ya shule ya msingi huku macho yakiwa katika nuru mzuri ya kuona,
ikiwa ni baada ya kufanyiwa oparesheni lile lililoumia.
Anawataja watoto wenzake enzi hizo kwa kutaja timu
ya mchezo huo wa kujaza mchanga katika chupa baina ya mtaa wa kanisani
na bondeni kwa majina, katika timu yake ya kanisani iliwakilishwa na
yeye, Jamhuri Seif, Mwajabu Sufian, Ramadhan Wania, Ruth Elias,
Christina Daniel na Christina Anthony.
Wakati timu ya wapinzani wao iliundwa na Amba
Oden, Patrick Richard, Mariam Seif, Winfrida Anthony, Halima Abdallah,
Anna Anthony, Mwanahamis Sufian, Jesca Pius na Georgina Kulabuku ambao
wamefariki dunia.
Hali inajirudia
Akiwa darasa la tatu mwaka 2006 macho yake
yalianza kupoteza tena uwezo wa kuona taratibu. Alilazimika kuomba
kuomba ahamishiwe kutoka dawati la nyumba ambako alikuwa anakaa na
kuhamia mbele ili kuweza kuona kilichoandika ubaoni.
Kabla ya likizo ya mwezi wa sita akiwa kidato cha
pili shule ya sekondari ya kata ya Turiani wilaya ya Mvomero mkoani
Morogoro akiwa na umri wa miaka 16, licha kusogezwa dawati la mbele ili
kuweza kuona kilichoandikwa ubaoni wakati huo ikiwa ni mwezi wa tano
mwaka 2006 dawati lake tena lilisogezwa jirani na ubao ambako maandishi
yalikuwa anaona.
Hali imeendelea kuwa mbaya kadri muda ulivyokuwa
unaenda mbele, hata baada ya kurudishwa hospitali, hakuweza tena kuwa na
uwezo wa kuona.
Mama mzazi wa Cecilia Patrick Ricardo, Evodia Lucas (53) anasema suala hilo anamuachia Mungu.
Evodia anasema baadhi ya madaktari walisema tatizo
la mwanaye amerithi kutoka kwa bibi yake lakini jambo hilo yeye
anapinga akida hakuna mwenye tatizo hilo ukiachilia mbali kwa mama yake
na mtoto wake tu.
Source: Mwananchi
Source: Mwananchi
Comments