JE KUNA VYAKULA AMBAVYO UKILA NI DHAMBI?

Na Sam Balele


Katika mambo ambayo yamekuwa yanaleta mjadala hata katikati ya wakristo wenyewe kwa wenyewe ni hili suala la unajisi katika vyakula. Hili suala lingekuwa limebaki kati ya wakristo na waislamu aha wala nisingeshangaa lakini nashangaa kwakuwa linaleta kikohozi hata katikati ya wakristo wenyewe, ila pia sishangai sana kwakuwa pia lilileta kikohozi hata katikati ya wanafunzi wa Yesu Kristo wale waliokuwako katika Kanisa la kwanza, japo picha ya kipindi kile ni rahisi kuichora kwakuwa mvutano ulikuwa katikati ya wanafunzi wayahudi waliomuamini Bwana na wanafunzi wa mataifa, na hata katikati ya wanafunzi wa kiyahudi wenyewe pia. Mvutano uliokuwako katika Kanisa la kwanza ni rahisi sana kuuelezea kwakuwa ulikuwa unachochewa zaidi na wale wayahudi waliokuwa na msimamo mkali juu ya mapokeo ya torati juu ya vyakula na mambo mengine ikiwemo suala la kutahiriwa na kadhalika. Petro alitumwa kupeleka Injili kwa Wayahudi, Paulo alitumwa kupeleka Injili kwa Mataifa ambao ni sisi, tusiokuwa Wayahudi kwa asili.

Injili ilipoenda kwa Wayahudi, kuna ambao waliamini neno lake na kuokoka, wakimpokea Yesu Kristo kuwa Bwana wao. Injili ilipoenda kwa Mataifa, kuna ambao waliamini neno lake na kumuamini Yesu Kristo kuwa Bwana wao. Na kuna watu ambao walikataa kuamini kama tu ilivyo leo, popote Injili ya Yesu Kristo iletayo Wokovu inapohubiriwa kwa usahihi kabisa. Sasa hawa Wayahudi walioamini Injili na kuokoka, na kuwa wanafunzi wa Yesu, wale waliokuwa na msimamo mkali juu ya Torati ndo walianza kuleta kikohozi ndani ya Kanisa la Kristo kwa habari ya beliefs kadhaa ikiwemo suala la vyakula. Hata Petro pamoja na utumishi wake wote ule bado alikuwa na shida juu ya vyakula, mpaka Mungu alipomfungua ufahamu Yeye mwenyewe na kuiangusha ile ngome ya fikra aliyokuwa nayo. Hii ilitokea wakati Mungu anamtuma kwenda kuihubiri Injili kwa mtu wa Mataifa aitwaye Kornelio.

Ishu ya vyakula ilileta mvutano sana, hata ikabidi mtume Paulo kuizungumzia katika barua zake ili kuweka hali sawa katikati ya wanafunzi, tena wale waliokuwa wa Mataifa kama sisi Watanzania. Barua hizo zilizobeba maonyo juu ya mvutano wa vyakula ni pamoja na ile ya Warumi na Wakolosai na ile iliyoenda kwa Timotheo. Hawa walikuwa watu wa Mataifa, na walikuwa wanasumbuliwa sana na Wanafunzi wa asili ya Kiyahudi waliokuwa na msimamo mkali kwa habari ya maaagizo ya Torati. Kuna ambao walikuwa wanalazimisha hata kutahiriwa, wakidai kuwa bila tohara ya mwili mtu anakuwa bado hajakamilika katika Wokovu, what a nonsense that was; Paul crushed this doctrine, kwakuwa aliujua kweli na habari ya wito wake na alijua kile ambacho Yeye aliyemtuma alikuwa amemuhakikishia kama alivyosema katika Warumi 14:14.

Ni kweli kabisa katika Agano la Kale kuna makatazo ya vyakula, kuwa usile hiki, usile kile, kuwa hiki ni najisi, na kile ni najisi hivyo usile. Andiko,lililo maarufu na inalotumika sana na wakristo wanaovuta juu ya vyakula ni lile la Walawi 11, ambalo naamini hata wanafunzi wale wa Yesu Kristo wa asili ya kiyahudi walikuwa wanalitumia sana ili kuwabananisha wanafunzi wengine wa asili ya mataifa. Kama ilivyo leo, watu wanatumia andiko hilo kwa habari ile ile. Ila ashukuriwe Mungu kwakuwa tunayo maandiko katika Agano Jipya yanayotuweka huru kabisa na habari hii ya vyakula. Tena unajua mimi namshangaa hata huyu mtume Petro, siku ile Bwana Yesu aliposema yale maneno katika Mathayo 15:10-17, yeye Petro alikuwa anawaza nini sijui hata akaendelea na ule msimamo juu ya unajisi wa vyakula, ila ashukuriwe Mungu aliyemfungua na ngome ile. Ngome zingine huwa zinahitaji hekima na maarifa ya Mungu kuziangusha, na hekima na maarifa hayo ndiyo yanahitajika leo na ninakuhakikishia kuwa yaja yapo njiani, na ngome zinakwenda kubomolewa kwa kiwango cha kustaajabisha na wengi waliofungwa na maagizo na mafundisho ya wanadamu yenye hila wanaenda kufunguliwa.

Maandiko yako wazi nayo yanasema hivi:

Mathayo 15:11, 17
"Sikilizeni sicho kiingiacho kinywani kimtiacho mtu unajisi bali kitokacho ndicho kimtiacho mtu unajisi....Hamjafahamu bado ya kuwa kila kiingiacho kinywani hupita tumboni kikatupwa chooni?"

Marko 7:15,18,19
"Hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo ndivyo vimtiavyo unajisi yule mtu...hamfahamu ya kwamba kila kitu kilicho nje ya mtu kikimwingia hakiwezi kumtia unajisi kwasababu hakimwingii moyoni ila tumboni tu, kisha chatoka kwenda chooni? Kwa kusema hivi alivitakasa vyakula vyote."

Matendo ya Mitume 10:11-15
"Akaona mbingu zimefunuka na chombo kikishuka kama nguo kubwa inatelemshwa kwa pembe zake nne hata nchi, ambayo ndani yake walikuwamo aina zote za wanyama wenye miguu minne na hao watambaao na ndege wa angani. Kisha sauti ikamjia kusema ondoka Petro uchinje ule, lakini Petro akasema, hasha Bwana, kwa maana sijakula kamwe kitu kilicho kichafu au najisi. Sauti ikamjia mara ya pili ikimwambia, vilivyotakaswa na Mungu usiviite wewe najisi."

Warumi 14:1-14
"Yeye ALIYE DHAIFU WA IMANI, mkaribisheni, WALAKINI MSIMHUKUMU MAWAZO YAKE. MTU MMOJA ANAYO IMANI, ANAKULA VYOTE, LAKINI YEYE DHAIFU HULA MBOGA. Yeye alaye asimdharau huyo asiyekula wala yeye asiyekula asimhukumu huyo alaye, kwa maana Mungu amemkubali.....KILA MTU NA ATHIBITIKE KATIKA AKILI ZAKE MWENYEWE....Basi ni hivyo kila mtu miongoni mwetu atatoa habari zake mwenyewe mbele za Mungu....NAJUA TENA NIMEHAKIKISHIWA SANA KATIKA BWANA YESU, YA KUWA HAKUNA KITU KILICHO NAJISI KWA ASILI YAKE, LAKINI KWAKE YEYE AKIONAYE KITU KUWA NAJISI, KWAKE HUYO KITU KILE NI NAJISI."

Wakolosai 2:16,17
"Basi mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji.....mambo hayo ni kivuli cha yajayo bali mwili ni wa Kristo. BASI IKIWA MLIKUFA PAMOJA NA KRISTO MKAYAACHA YALE MAFUNDISHO YA AWALI YA ULIMWENGU, KWANINI KUJITIA CHINI YA AMRI, KAMA WENYE KUISHI DUNIANI. MSISHIKE, MSIONJE, MSIGUSE (mambo yote hayo huharibika wakati wa kutumiwa), hali mkifuata maagizo na mafundisho ya wanadamu? Mambo hayo yanaonekana kana kwamba yana hekima katika namna ya ibada mliyojitungia wenyewe, na katika kunyenyekea na KUUTAWALA MWILI KWA UKALI, lakini hayafai kitu kwa kuzizuia tamaa za mwili."

1 Timotheo 4:1-4
"Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani.....wakiwazuia watu wasioe na kuwaamuru wajiepushe na vyakula ambavyo Mungu aliviumba VIPOKEWE KWA SHUKRANI NA WALIO NA IMANI WENYE KUIJUA HIYO KWELI. Kwa maana kila kiumbe cha Mungu ni kizuri, wala hakuna cha kukataliwa kama kikipokewa kwa shukrani, kwa kuwa kimetakaswa kwa neno la Mungu na kwa kuomba."

Sasa hayo ni maandiko kutoka katika Agano Jipya lililowekwa kwa damu ya Yesu Kristo. Maandiko haya yanaweka msimamo juu ya vyakula mbali na Walawi 11. Agano la Kale ni kivuli cha Agano Jipya, yote yaliyosemwa ama kufanywa katika Agano la kale yalikuja kutimilizwa katika Agano Jipya. Yalitimilizwa na kugongomelewa msalabani, yalitimilizwa kabla na katika kazi ya Yesu Kristo pale msalabani. Hakuna habari ya siku, hakuna habari ya mwandamo wa mwezi, hakuna habari ya sabbaths, tena hakuna habari ya vyakula wala habari ya vinywaji kwakuwa Bwana Yesu alitupa kula mwili wake na kuinywa damu yake katika jioni ile ya Pasaka alipoketi chakulani na wenzetu wale na kula nao na kunywa nao. Akamega mkate pamoja nao, na kula nao na kuinywa divai pamoja nao, huku akiacha agizo kufanya vile kwa pamoja kwa ukumbusho wake. Hadithi zote zinazotajwa katika Wakolosai 2:16 zilikomea msalabani nazo zilikuwa ni kivuli tu. Sasa hatuko chini ya amri wala hatujitii chini ya amri kwa habari ya vyakula au vinywaji au siku au mwandamo wa mwezi au sabbaths

Lakini ikiwa mtu anaamua kujitia chini ya amri kama mwenye kuishi duniani, sasa hapa hekima ya Mungu na itambulikane, maana yake watoto wa Mungu ni tofauti na watoto wa Ibilisi walio watoto wa ulimwengu huu, watoto wa Mungu ni wapitaji, ni wasafiri, ndiyo maana Paulo akauliza "kwa nini kujitia chini ya amri kama wenye kuishi duniani?". Watoto wa Mungu imewapasa kuenenda kwa Roho tangia siku ile Bwana Yesu alipoitimiliza Torati na Manabii pale msalabani, sasa ni nini kujitia chini ya maagizo ambayo yalikuwa ni kivuli cha mambo yajayo? Ikiwa umejiondoa katika kuzishika sabbaths, kwa nini hujiondoi katika kushika vyakula? Kwa nini kunakuwa na double standard katika mambo ya Mungu?

Je Mungu anajipinga mwenyewe ama ni sisi wanadamu ndo tunaopotoshana kwa kusikiliza roho zidanganyazo na mafundisho ya mashetani kama alivyonena mtume Paulo katika 1 Timotheo 4:1,2

Yeye aliye na hekima na apambanue, na athibitike katika akili zake mwenyewe.
Bwana Yesu Kristo ni Kichwa cha Kanisa, viungo vyote imewapasa kukishika Kichwa - Wakolosai 2:18,19

MUNGU akubariki sana.
By  Sam Balele
 
Bali wote waliompokea(YESU KRISTO) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; -Yohana 1:12

Comments

Unknown said…
WE MTUMISHI WA MUNGU NAONA UNATUMIA TAFSIRI SISISI YA MAANDIKO. KUHALALISHWA KWA CHAKULA NI TOFAUTI KABISA NA KUOHALALISHA VIUMBE. NAONA UMEAMUA KUTAFSIRI MAANDIKO ILI UKIDHI HAJA YA TAMAA YAKO BADALA YA KUJITOA KUTAFUTA UKWELI WA MAANDIKO HAYO.