MATUMIZI MABAYA YA SADAKA NA MADHARA YAKE KWA MTUMISH

 Na Daimon Nathan

Katika miaka ya maisha niliyoishii kumekuwa na ongezeko la manung’uniko ya waumini juu ya kile ambacho kinaonekana kuwa ni matumizi mabaya ya sadaka yanayodhaniwa kufanywa na watumishi wa madhabahuni. Jambo hili limekuwa likiongezeka kwa kadiri muda unavyokwenda kiasi ambacho utoaji wa waumini umeathiriwa na hisia hizi. Watumishi wamekuwa wakituhumiwa na waumini kwamba ni wapenda anasa na wanatumia sadaka za waumini kujinufaisha na kushibisha tamaa za miili yao zisizo na uhusiano na kazi ya Mungu.
Ni kweli kwamba Mungu ameruhusu makuhani watunzwe kwa vitu vinavyotolewa sadaka, lakini pia Mungu ana utaratibu alioweka kuhusu nini wapate na kitolewe vipi. Mtumishi haruhusiwi kumlazimisha mtu kutoa kitu kama sehemu ya sadaka yake kwa Mungu kisha yeye akakichukua akaenda kukitumia kukidhi tamaa za mwili wake. Natamani leo tujifunze juu ya namna Mungu alivyoshughulika na jambo hili ambalo liliwahi kutokea nyakati za agano la kale ili tupate kujua jinsi ambavyo jambo hili ni la hatari kwa watumishi wa Mungu.
Ieleweke kwamba hali ya manung’uniko ya aina hii si ngeni kwa Mungu, ilisha wahi kutokea siku za nyuma, na kwamba namna Mungu alivyoshughulikia jambo hili siku za agano la kale ndivyo atakavyoshughulikia sasa na wakati wote kwa kuwa Yeye habadiliki. Ni mwamuzi mwenye haki asiye na double standard, alivyoshughulikia jambo hilo siku za nyuma ndivyo atakavyolishughulikia sasa na milele.
Katika kitabu cha samweli wa kwanza 2:12-17 tunaona habari ya makuhani waliokuwa wana wa Eli, Kuhani waliokuwa wakitambulika kwa majina ya Hofni na Finehasi na jinsi walivyokuwa wakiishi na kutenda kama makuhani wa Mungu. Unaposoma habari hii utaona mambo kadhaa ya uovu waliokuwa wakiyafanya makuhani hawa ambayo pamoja na mambo mengine yalihusisha matumizi mabaya ya sadaka kama ifuatavyo
• Kutokumjali Mungu waliyekuwa wamewekwa kumtumikia wala kuziheshimu taratibu alizoweka kwa maisha yao (1sam 2:12) kudharau sadaka zilizokuwa zikitolewa kwa Mungu (1sam 2:17, 29)
• Kutwaa sadaka kwa nguvu na kuzitumia kwa matakwa yao kutoka mikononi mwa watu zikiwa zinaandaliwa kwa kumtolea Bwana ili kushibisha tamaa za iili yao na matumbo yao (1Sam 2:13-14)
• Kuvunja utaratibu uliowekwa na Mungu wa utoaji wa sadaka za kuteketezwa kwa kutwaa kwa nguvu nyama mbichi kabla ya mafuta kuteketezwa kwa moto, hii ikiwa ni kinyume na maagizo ya Mungu juu ya sadaka za amani kwa makuhani (Law 3:1-5)
• Uasherati na kulala na wanawake waliokuwa wakitumika mlangoni pa hema ya kukutania (kwa lugha ya sasa kanisa) (1Sam 2:22b)
• Kutokumsikiliza baba yao aliyekuwa kiongozi wao wa kimwili na kiroho pale alipowakanya kuachana na tabia hiyo (1Sam 2:23-25)
Biblia inasema kwa sababu ya matendo ya uovu ya vijana hawa dhambi yao ilikuwa kubwa machoni pa Bwana kwa maana matendo yao yaliwafanya watu wadharau sadaka ya Bwana na wengine wakarudi nyuma na kuacha kumtolea Mungu. (1sam 2:17) jambo hili liliamsha wivu wa Mungu na hasira ya Mungu juu ya Eli na uzao wake. Eli aliadhibiwa kama kiongozi kwa kuwa hakuchukua hatua za kutosha kuwarekebisha wanae, hakuwalea jinsi ilivyompasa hata wakamdharau Mungu na sheria zake.
Maamuzi na hukumu ya Mungu juu ya dhambi hii imeandikwa katika 1Samweli 2:30-36;
• Aliufuta uzao wa eli wasiwe makuhani tena nyumbani mwa Mungu kwa kuwaua wanawe wote wawili. (1sam2:34)
• Siku za uhai za watu wote wa jamaa ya eli zilipunguzwa, hakuna aliyeweza kuishi na kufikia uzee milele yote. Yaani jamaa ya eli wote walihukumiwa kufa mapema kabla ya uzee wao. (1sam2:33)
• Watu wote ambao hawakutengwa na madhabahu ya Bwana katika jamaa ya eli walihukumiwa kuwa watu wenye kuhuzunisha. Wenye kusababisha huzuni katika jamaa yao. . (1sam2:33)
• Watu wa jamaa yote ya eli walihukumiwa umaskini na kwamba wangeishi kwa kuomba toka kwa kuhani mwaminifu wa Bwana aliyeinuliwa (1Sam 2:36)
• Anguko lao lilikuwa kuu sana kwa namna ambayo lilileta mshangao katika maskio ya wote walio lisikia (1sam 3:11)
• Uovu wao ulihukumiwa kuto kusafika kwa dhabihu wala kwa sadaka hata milele. Yaani dhambi yao ilihukumiwa kuto kusamehewa kwa kuwa matendo yao yaliwafanya watu kumdharau Mungu na maagizo yao.
Biblia inaweka wazi kwamba Mungu wetu ni Mungu mwenye wivu, Sadaka ni jambo lililoagizwa na Mungu mwenyewe, ni jambo linaloendana na kuthibitisha mfano wa Mungu uliopo ndaniya wanadamu kwa kuwa utoaji ulianzishwa na Mungu mwenyewe aliyemtoa mwana wake wa pekee kwa upendo kwa ajili ya ukombozi wa wanadamu.
Tendo la matumizi mabaya ya sadaka na uvunjaji wa utaratibu wa Mungu wa utoaji dadaka ni Dhambi kuu ambayo inamgusa Mungu moja kwa Moja. Imeandikwa katika 1Samweli 2:25 “mtu mmoja akimkosa mwenzake, Mungu atamhukumu; lakini mtu akimkosa Bwana, ni nani atakayemtetea?”
Dhambi ya matumizi mabaya ya sadaka ni dhambi ambayo mtu anakuwa amemkosea Mungu moja kwa Moja kwa kuwa inawafitinisha watu wa Mungu na Mungu wao, inaifanya sadaka ya mtu isiwe na kibali mbele za Mungu, inaharibu Imani za watu na kuwarudisha nyuma. Namna ile ile ambayo Mungu alishughulika na dhambi ya wana wa Eli ndivyo atakavyoshughulika na dhambi hii katika maisha yetu ya sasa. Biblia katika Zaburi 7 : 11 inaweka wazi kwamba - Mungu ni mwamuzi mwenye haki, Naam, Mungu aghadhibikaye kila siku. Mungu hana Double standard, Ikiwa dhambi ya wana wa eli ilihukumiwa kutokusamehewa milele, wala hakuna sadaka wala dhabihu ambayo ingeweza kuusafisha uovu ule, ni dhahiri kwamba Mungu hata sasa hukumu ya Mungu juu ya dhambi hii huwa ni kali kwa sababu ni jambi linalomgusa moja kwa moja.
Mungu akusaidie wewe uliye mtumishi wa Mungu kujiepusha na vitu vilivyowekwa wakfu kwa Bwana. Mungu akupe kuwa mwaminifu katika uwakili uliopewa wa sadaka za watu wa Mungu wanazoleta kwa Mungu wao na ufanikiwe kuziweka katika mambo yanayomrudishia Mungu utukufu.

BARIKIWA
 


Bali wote waliompokea(YESU KRISTO) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; -Yohana 1:12

Comments