Muhando kuachia ‘Kung’uta Yesu’


MALKIA wa nyimbo za Injili nchini, Rose Muhando, mwishoni mwa mwezi huu anatarajiwa kuachia albamu mpya itakayojulikana kwa jina la ‘Kung’uta Yesu’.
Nyimbo tano katika albamu hiyo amezirekodi nchini Afrika Kusini chini ya Kampuni ya Sony na kueleza kuwa albamu hiyo itakuwa na nyimbo nane, tatu akizirekodi hapa nchini.
Akizungumza kupitia blog yake, Muhando alisema kuwa albamu hiyo amewashirikisha waimbaji maarufu wa Afrika Kusini, Solomon Keke na William Sejake walioimba kwa Kizulu na Kiswahili.
“Sina mengi juu ya upendo mnaoonyesha katika kuniunga mkono kwa kazi zangu, nafanya kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Sasa nimekuja na nyimbo zingine, ukiwepo wimbo unaoitwa ‘Kung’uta na Yesu.’ Ninaomba sana mniunge mkono watumishi wa Mungu,” aliandika.
Muhando alisema kuwa watu wakae mkao mzuri kupata ladha mbili tofauti kwa muimbaji Solomon Keke aliyeimba Kiswahili pamoja na Kizulu.
Alisema yapo mambo mengi aliyojifunza kupitia wanamuziki wa Afrika Kusini kutokana na wao kupiga hatua kubwa katika uimbaji ukiwemo uimbaji wao wa kutumia mtindo wa ‘live band’  ambao anasema ameuchukulia  kama changamoto katika maisha yake.
Aidha, alisema yuko katika kujipanga kufanya video za nyimbo mbili katika alibamu hiyo atakazozifanya nchini humo chini ya Kampuni ya Sony.
Pia alisema amejipanga kufanya filamu ya maisha yake aliyopitia toka alipoanza muziki mpaka alipofikia sasa na kusema kuwa filamu hiyo itasimamiwa na Sony na atawashirikisha baadhi ya waigizaji kutoka hapa nchini.
“Ni shauku yangu kubwa kufanya filamu hiyo, kwakuwa ni moja ya ndoto zangu siku moja nifanye filamu itakayobadilisha maisha ya mtu mmoja aliyekata tamaa kutokana na umaskini anaopitia,” alisema.
Alisema kuwa ataachia nyimbo moja mpya itakayoambatana na video ya wimbo huo, ikiwa ni albamu ya tano tangu aanze kuimba.
Albamu hiyo ina nyimbo nane ambazo ni ‘Majira ya jioni’, ‘Kwa Yesu kuna mambo’, ‘Yesu Jiwe’, ‘Yerusalem’, ‘Hallelujah Hosana’, ‘Sondezigue’, ‘Shine na Papa’ pamoja na ‘Wololo’.
Wimbo ‘Sondezigue’ ameufanya na Solomon Keke, ‘Hallelujah Hosana’ amefanya na William Sejake.Wimbo ‘Wololo’ ukiwa na maana ya unisafishe Baba na ‘Sondezigue’ ni nivute uweponi mwako.

                                 Chanzo.Tanzania daima


Bali wote waliompokea(YESU KRISTO) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; -Yohana 1:12

Comments