Tabia ya uungu ya wana wa MUNGU duniani

Na Sam Balele


Tabia ya Mungu ni kusamehe na kusahau, tena kwa ajili yake mwenyewe si kwa ajili ya yule aliyemkosea. Tabia ya mwanadamu na namna ya ulimwengu huu ni kusamehe pasipo kusahau tena kwa ajili ya yule aliyekosea. Hapa ndipo watoto wa Mungu wanapochengana na watoto wa ulimwengu huu [watoto wa Ibilisi] 1 Yohana 3:10. Tabia yako ni ipi? Maana kama alivyo Baba ndivyo alivyo mtoto.

Tabia ya Mungu; tabia ya uungu imepasa kuwemo ndani ya wana wa Mungu, kama ilivyoandikwa katika 2 Petro 1:3,4
3 Kwa kuwa uwezo wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa [utakatifu], kwa kumjua Yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. 4 Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno; za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa WASHIRIKA WA TABIA YA UUNGU, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa."

Hapa nafarijika sana nikisoma hii 1 Yohana 2:1-3
1 Tazameni ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; NA NDIVYO TULIVYO. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui kwa kuwa haukumtambua Yeye [Yesu Kristo]. 2 Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo. 3 Na kila mwenye matumaini haya hujitakasa, kama Yeye alivyo Mtakatifu.

Mwanadamu anapopata Neema ya kufanywa mwana wa Mungu kwa Imani katika Yesu Kristo kama ilivyoandikwa katika Yohana 1:12-13,, ule utu wa kale unakufa ndani yake, ambapo utu wa kale tabia yake ni ya ulimwengu huu, unaotawaliwa na nguvu ya dhambi na mauti. Mwanadamu huyu anapokea utu mpya ndani yake kwa kuzaliwa mara ya pili yaani kuokoka, kupita kutoka mautini na kuingia uzimani; ambapo utu huu unakuwa umekirimiwa vitu vyote vipasavyo uzima na utakatifu. Ndipo Biblia inasema mwanadamu anakuwa kiumbe kipya 2 Wakorintho 5:17.

Kiumbe kipya kinakuwa kimepewa kuwa mshirika wa tabia ya Uungu, na katika hili kuna KUSAMEHE NA KUSAHAU, tena KUSAMEHE KWA AJILI YAKE YEYE MWENYEWE ALIYEKOSEWA SI KWA AJILI YA ALIYEKOSEA. Tabia hii ya MUNGU inaonekana katika Isaya 43:25, imeandikwa hivi;
25 Mimi, naam, Mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe wala sitazikumbuka dhambi zako"

Imempasa mwanadamu kuhitaji kufananishwa na mfano [image] ya Mwana wa Mungu, Bwana na Mwokozi Yesu Kristo. Ni Yeye pekee alidhihirisha Tabia ya Uungu ambayo kwa Neema ya Mungu imetiwa ndani ya wana wa Mungu na yapaswa kuwa dhahiri katika tabia na mwenendo wa maisha yao hapa duniani. Ikiwa wajijua wewe ni mwana wa Mungu lishike na lielewe hili haraka. Hili ndilo Kusudi la Mungu tangia awali hata sasa na milele. Warumi 8:28,29

Kwahiyo mwanadamu, jikague moyo wako na njia yako. Mungu hayuko mbali nawe. YUKO KARIBU SANA. Ufalme wa Mungu hauko mbali nawe; mlango wa ufalme wa Mungu bado uko wazi, haujafungwa. Fanya uamuzi sahihi leo.

Isaya 55: 6-7; Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana, mwiteni, maadamu yu karibu
Mtu mbaya na aache njia yake, na mtu asiye haki aache mawazo yake
Na amrudie BWANA, naye atamrehemu' Na arejee kwa Mungu wetu,
naye atamsamehe kabisa.

Fanya uamuzi sahihi, ili uiokoe roho yako na mauti, na nafsi yako ipate kufunguliwa na mwili wako upate kuponywa na uharibifu.

MUNGU awabariki 
By  Na Sam Balele

 

 Bali wote waliompokea(YESU KRISTO) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; -Yohana 1:12

Comments