UTUKUFU WA MUNGU UNAPATIKANA MAHALI YESU ALIPO ( Sehemu ya Tatu)

Na Daimon Nathan


TUNAWEZAJE KUWA KARIBU NA YESU ILI TUBADILISHWE NA KUPOKEA UTUKUFU ALIOTUPA?
Katika kujibu swali hili naomba nianze kwa kusema kwamba; Inawezekana kabisa mtu akawa ameokoka, yaani amemkiri Yesu kama Bwana na Mwokozi wa maisha yake, na kufanyika mtoto wa Mungu, lakini akakosa ule mng’ao wa utukufu wa Mungu katika maisha yake, yaani akakosa kudhihirisha attributes/sifa zinazoonesha uwepo wa Mungu katika maisha yake.
Ni muhimu kusisitiza kwamba udhihirisho wa sifa zinazoashiria uwepo wa Mungu katika maisha ya mtu ni matokeo ya ukaribu alio nao mhusika na Yesu kristo mwana wa Mungu unaomwezesha kuakisi utukufu alio nao Yesu katika maisha yake. Kuokoka ni hatua ya kwanza kabisa inayomfungulia mtu mlango wa kufanyika mtoto wa Mungu, hata hivyo akisha kuingia katika Pendo la Mungu mtu huyu ana safari ndefu ya kubadilishwa na kukamilishwa hata afikie cheo cha kimo cha utimilifu wa kristo Yesu. Kubadilishwa huku kunawezeshwa na bidii aliyonayo mhusika katika kutafuta kumjua Mungu na kutembea na Mungu.
Naomba ieleweke wazi kabisa kwamba Kamwe haiwezekani kutembea na Mungu sawasawa pasipo kujua vipaumbele vya Mungu. Imeandikwa katika Amosi 3:3; “Je! Watu wawili waweza kutembea pamoja, wasipokuwa wamepatana? Kamwe haiwezekani kutembea na Mungu pasipo kujua na kukubaliana na vipaumbele vyake. Kutembea na Mungu na kuwa karibu na Yesu ni jambo linaloanza na kutafuta kujua vipaumbele vya Mungu na mapenzi yake kwa maisha ya mtu binafsi.
Kipaumbele cha kwanza cha Mungu ni maslahi ya Ufalme wake, imeandikwa katika Mathayo 6 : 33 “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa” Yapo mambo mengi sana tunayosumbuka nayo katika maisha yetu ya kila siku, lakini kuanzia saa tunapookoka, kipaumbele cha kwanza katika maisha yetu inapaswa kuwa ni maslahi ya ufalme wa Mungu, yaani Maisha yetu kudhihirisha haki amani na furaha katika roho mtakatifu (Warumi 14 : 17) ambazo ndizo nguzo za ufalme wa Mungu.
Biblia inaweka wazi kabisa mwelekeo wa utendaji wa Bwana Yesu na ni wapi tunaweza kukutana na Yesu kristo, na kuwa karibu naye. Siri hii imefichwa katika utume mkuu tuliopewa na Bwana Yesu kama ilivyoandikwa katika injili ya mathayo 28: 19-20 “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”
Katika maneno haya ya Bwana Yesu Mungu ametufunulia mchakato wa hatua tatu unaosimamiwa na Yesu Kristo katika mradi wa kuukuza ufalme wa Mungu. Hatua hizo tatu ni kama ifuatavyo;
• KUWAFANYA MATAIFA YOTE KUWA WANAFUNZI WA YESU; hii ni hatua ya kwanza kabisa katika mradi wa kuukuza ufalme wa Mungu. Hatua hii inahusisha kazi ya kuhubiri habari njema ya wokovu. Iko namna nyingi sana ya kuhubiri, hata matendo yetu yanatosha kumhubiri kristo. Ni hatua ambayo inahusisha kuwajulisha watu habari njema ya wokovu, habari za ile neema ya Mungu na upendo wa Mungu uliomtoa kristo Yesu kwa ukombozi wa ulimwengu. Si kila mtu anaweza kuwa mwinjilisti wa madhabahuni, lakini kila mtu anaweza kwa neno au kwa tendo kuwashuhudia watu habari njema za wokovu, na Yesu kristo ndiye msimamizi mkuu wa kazi hii. Ukitaka kuwa karibu na Yesu, fanya sehemu yako katika kutekeleza kazi hii sawa na karama uliyopewa na Bwana, huko utamwona yesu na kuwa karibu naye sawa na ahadi yake kuwa nasi siku zote hata ukamilifu wa dahari.
• KUWABATIZA KWA JINA LA MUNGU BABA NA MWANA, NA ROHO MTAKATIFU; Hii ni hatua ya pili katika kuukuza ufalme wa Mungu, ni hatua inayohusisha kuwawezesha watu kuuvua utu wa kale na kuuvaa utu mpya ulioumbwa katika haki ipatikanayo kwa Imani na utakatifu wa kweli. Hii ni hatua inayohusisha kuuzika utu wa kale na kuvaa utu mpya, inahusisha kufanywa upya nia za watu ili wapate kuwa na nia ile ile iliyokuwamo ndani ya kristo Yesu, waache kutafuta mambo yao badala yake watafute kutenda mapenzi ya Mungu. Ni hatua inayohusisha ukombozi wa roho na mwili wa mwanadamu ili awekwe huru na apate kuudhihirisha utukufu wa Mungu katika maisha yake. Zipo karama za Roho mtakatifu ambazo zimeachiliwa kwa watu wa Mungu ili kuikamilisha kazi hii. Ukitaka kuwa karibu na Yesu, basi elewa kwamba msimamizi mkuu wa kazi hii ni Yesu kristo Mwana wa Mungu, hivyo ingia katika kazi hii sawasawa na wito ulio ndani yako pamoja na karama uliyopewa na Roho mtakatifu, utamwona Yesu akikuwesesha kuikamilisha.
• KUWAFUNDISHA KUYASHIKA YOTE NILIYOWAAMURU; Hii ni hatua ya tatu katika kuukuza na kuueneza ufalme wa Mungu. Ni hatua inayohusisha kuwasaidia watu wapate kujua mapenzi ya Mungu na hivyo wapate kutembea sawasawa na mapenzi ya Mungu kwa maisha yao. Ni hatua inayohusisha kuuondoa ujinga na kuvunja zile ngome za kifikra na kuumba akili mpya ndani ya watu iliyohuishwa na elimu ya Mungu. Ni hatua inayohushika na kuumba Imani ndani ya watu kwa kuwafundisha neno la Mungu. Ni hatua inayo wezesha watu kutambua tofauti kati ya amri za Mungu, maagizo ya Mungu, Maelekezo ya Mungu na Hukumu za Mungu. Ni hatua inayohusisha kuwasaidia watu kuelewa kanuni za Mungu, mfumo wake wa utendaji kazi na namna yake ya kutenda kazi ili watu hawa wapate kuwa raia wema wa ufalme wa Mungu na watenda kazi pamoja na kristo. Ukitaka kuwa karibu na Mungu, chunguza sehemu yako katika hili, na omba Mungu akuongoze katika kuifanya kazi hii sawasawa na karama iliyomo ndani yako. Kazi hii inasimamiwa na Yesu kristo mwenyewe na hakika utamwona akikusaidia katika kuikamilisha kwa utukufu wa jina lake takatifu.
Napenda uelewe kwamba kuwa karibu na Yesu ni jambo linalowezekana ikiwa utaamua kuingia katika mradi wa kuueneza na kuukuza ufalme wa Mungu sawasawa na nafasi na karama uliyopewa na Bwana. Bwana Yesu kwa kinywa chake amesema huko ndiko atakakopatikana “SIKU ZOTE” hata ukamilifu wa dahari. Baraka za Mungu karama zake pamoja na nguvu za Mungu ni maalum kwa ajili ya kazi hii ya kuukuza ufalme wa Mungu

 By Daimon Nathan
 
Bali wote waliompokea(YESU KRISTO) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; -Yohana 1:12