KAMA utakuwa sahihi, huwezi
kuwataja waimbaji wa nyimbo za Injili nchini na Afrika Mashariki bila
kuyataja baadhi ya majina kutokana na mvuto na ubora wa kazi zao sokoni.
Miongoni mwao ni Rose Mhando, Bahati Bukuku, Upendo Nkone, Upendo
Kilahiro, Christina Shusho, Siana Ulomi, Martha Mwaipaja, Jane Miso,
Jennifer Mgendi na chipukizi, Edison Mwasabwite.
Kwa mvuto wa kazi zao, kila duka linalouza kazi za muziki wa Injili ni
vigumu kupita saa mbili kabla mmoja wao hajauza kazi yake.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa muziki wa Injili, baadhi ya wasanii wa Bongo
Fleva, taarabu na muziki wa dansi, hali ni tofauti kwani soko kwa
upande huo limekuwa gumu.
Nyimbo za Injili zinaonekana kuanza kuufunika muziki mwingine kiasi cha
kupigwa katika kumbi mbalimbali za starehe kwa hoja kuwa muziki wake
unachezeka, una mvuto, hivyo kupendwa na wengi.
Rose Muhando
Huyu ndiye kiboko yao, wanamuziki wa Bongo Fleva wanamfahamu kwa jinsi
anavyowapiga bao katika uuzaji wa kazi zake, si tu katika CD na video,
Rose pia ni kinara wa mauzo katika miito ya simu.
Diamond ambaye anasifika kwa kuuza miito ya simu, akikutana na Rose
anakaa chini kwani mapema mwaka huu alimwacha mbali kwa kuingiza sh
milioni 29 ndani ya miezi mitatu, huku Diamond akiingiza sh milioni 21.
Albamu zake za ‘Mteule Uwe Macho’, ‘Kitimutimu’, ‘Jipange Sawasawa’ na
‘Utamu wa Yesu’ bado zinaendelea kufanya vizuri pamoja na kuwa wasanii
wengine wanaingiza albamu mpya kila kukicha.
Bahati Bukuku
Huyu anatajwa kushikilia nafasi ya pili ya mauzo ya CD na video katika
maduka mbalimbali ya kazi za sanaa.
Pamoja na kutotoa kazi mpya mara kwa mara, albamu yake moja ilimfanya
kuwa mwimbaji namba mbili katika mauzo na matamasha nchini.
Katika tamasha lolote la Injili, haliwezi kukamilika bila kupigwa nyimbo
zake ama kualikwa, albamu zake za ‘Nyakati za Mwisho’, ‘Nimesamehewa
Dhambi’, na mpya aliyoizindua Septemba, 2013 iitwayo ‘Dunia Haina
huruma’ zimemfanya kuendelea kuwika katika soko la muziki huo.
Bukuku ni mwanamuziki mwenye mafanikio mengi ambapo kwa sasa amejikita
pia katika ujasiriamali, maisha yake asilimia 70 yapo katika kulima na
kuwekeza.
Mwimbaji huyo anamiliki nyumba nne alizojenga mwenyewe, mbili zikiwa
Tabata Migombani, moja Bunju na nyingine Mbezi Beach.
Pia anamiliki mashamba manne huko Kitunda, Bunju, Kibaha na Mbeya,
mashamba hayo yana takriban ekari mbili hadi tano.
Aidha, ana makarashi mawili ya kusaga dhahabu mkoani Geita na anamalizia
kujenga hoteli yenye vyumba 38 mkoani Geita, Hoteli hii itaitwa ‘Double
B Hotel’.
Upendo Kilahiro
Mwanadada huyu licha ya kutokuwa na albamu kwa sasa, bado ameendelea
kutamba katika muziki wa Injili kutokana na sauti yake kuwa tamu na
nyororo.
Kwa Kilahiro, muziki wa Injili unamlipa kwani ameweza kuanzisha chuo cha
ushonaji kiitwacho, New Day Africa Foundation, ambacho wanafunzi wake
wanasoma bure kwa muda wanaochukua ujuzi chuoni hapo.
Kilahiro anayetamba na nyimbo za ‘Unajibu Maombi’ na ‘Usinipite’, ni
msanii namba tatu kwa mauzo ya nyimbo za Injili hapa nchini.
Sifa nyingine ya mwanadada huyu ni kwamba, akiwa katika harakati zake za
uimbaji, watu wengi hasa raia wa Afrika Kusini akiwemo mwanamama Rebeka
Malope, aliwahi kumuomba abadili uraia wa Tanzania na kuchukua uraia wa
nchi hiyo ili aweze kufanya kazi zake kwa uhuru zaidi akiwa nchini
humo, lakini Upendo alikataa.
Kutokana na msimamo wake huo, Malope alimuomba Upendo kuwa msemaji wake
katika ukanda wa Afrika Mashariki, kazi anayoifanya mpaka sasa.
Upendo Nkone
Ana albamu za ‘Mungu Baba’, ‘Hapa Nilipo’, ‘Zipo Faida’ na mpya
aliyoitoa mwaka jana iitwayo ‘Nimebaki na Yesu’, zinafanya vizuri huku
albamu zote zikiendelea kununuliwa kwa wingi.
Kila anapoachia wimbo mpya, huendelea kuzifanya zile za zamani ziwe
nzuri zaidi.
Mbali ya kuuza kazi zake, pia ni mwanamuziki anayeongoza kwa kufanya
matamasha ndani na nje ya Bongo.
Mara kwa mara hufanya ziara nchini Kenya ambako anakubalika na
kuheshimika, lakini pia ni fundi wa kushona nguo, ambapo anamiliki ofisi
aliyoajiri watu kwa kazi hiyo.
Christina Shusho
Huyu anazo sababu zaidi ya 100 za kuwa mwanamuziki anayeuza katika
muziki wa Injili.
Sababu kubwa ya kwanza ikitajwa kuwa ni sura yake inapokaa kwenye ‘kava’
inampa mteja hamu ya kutoa pesa yake kununua CD.
Sababu ya pili ni sauti yake na namna anavyotengeneza video zake, tungo
zake zinazogusa maisha ya kawaida na kiroho zimekuwa kivutio kikubwa.
Mwimbaji huyo anamiliki kipindi cha runinga, lakini Shusho pia kwa mwaka
jana alishinda tuzo ya mwimbaji wa mwaka 2013 kwa nchi za Afrika
Mashariki katika tuzo za Africa Gospel Music Awards.
Masanja Mkandamizaji
Anafahamika kwa jina la ‘Masanja Mkandamizaji’ huku jina lake halisi
likiwa ni Emmanuel Mgaya, yeye ameweza kushika kasi baada ya kuokoka na
kujiita mchungaji mtarajiwa.
Masanja Mkandamizaji anatamba na albamu yake ya ‘Hakuna Jipya’, ambayo
ndani yake kuna mfumo wa uchekeshaji. CD za msanii huyo zimefanya vizuri
sana sokoni.
Waliochipukia
Martha Mwaipaja na Siana Olomi nao wanaingia kwenye kundi hilo, lakini
wanapishana kidogo kutokana na sababu mbalimbali zilizotolewa na
wafanyabiashara wa kazi hizi.
Waimbaji hao ni kama wanachipukia kwenye soko la kazi hizi, lakini
wamekuwa wakichuana na wakongwe kina Flora Mbasha na Jennifer Mgendi,
ambao wamekuwa katika muziki huo kwa muda mrefu.
Edson Mwasabwite
Anaingia akiwa mpya kabisa tena chipukizi kwa kupanda juu baada ya
albamu yake ya ‘Ni kwa Neema tu na rehema’ ikiendelea kuwabamba
mashabiki wa nyimbo za Injili.
Albamu ya Mwasabwite imefanya vizuri sokoni na itaendelea kufanya vizuri
kwa mwaka huu kutokana na wimbo wake uliobeba albamu.
Waliochemsha
Wafanyabiashara wa kazi hizi wanasema, Jennifer Mgendi na Flora Mbasha
waliwahi kuwa vinara wa mauzo, lakini walipoanza kujichanganya na
biashara nyingine, iliwapunguzia mashabiki ambao walianza kununua kazi
za waimbaji wengine.
Flora Mbasha
Japo mwimbaji huyu amefanya matamasha ya kimataifa nchini Marekani na
kwingineko pamoja na kumiliki studio, likichomuangusha ni kujihusisha na
kampeni mbalimbali zikiwamo za vyama vya siasa.
Jennifer Mgendi
Msanii huyu kujiingiza katika uigizaji wa filamu, zinatajwa kuwa ni
sababu zilizomrudisha nyuma.
Boni Mwaitege
Huyu amepotea katika soko baada ya kukaa kimya tangu alipotoa albamu ya
‘Mama ni Mama.’ Ukimya wake unaelezwa kuwa umesasabisha hata uuzaji wa
nyimbo zake kuwa doro.
Hawa ndio wasanii wa muziki wa Injili wanaoongoza sokoni.
CHANZO: GAZETI LA TANZANIA DAIMA
Bali wote waliompokea(YESU KRISTO) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; -Yohana 1:12
Comments