Je! Kuna tofauti kati ya mteule na mwanafunzi?

Na mtumishi wa MUNGU, Frank Philip


Katika sehemu ya kwanza ya somo hili tumeona maana ya neno Mwanafunzi kwamba ni mtu anayetenda/fanya yale anayojifunza kwa Mwalimu wake. Haiishii tu kukiri/kushuhudia bali kutenda kwa sababu imeandikwa “imani bila matendo imekufa”. Tunaokolewa kwa imani, na huwezi kusema tu “umeokoka” kama hutendi sawa na maneno yako, itakuwa unajidanganya na kuwaharibu wakusikiao pia. Agizo la kuwafanya mataifa kuwa wanafunzi halikuishia kwenye kuamini, kubatizwa na kuokoka, ILA kujifunza KUSHIKA (kuyaishi) yote Yesu aliyoyaagiza.

Kumbuka, wanafunzi wa SIRI wa Yesu, kwa mfano Yusufu wa Arimathaya na Nikodemo walionyesha imani yao kwa Bwana kwa matendo. Hutawasikia mahali walipohubiri humu katika Injili. Wakati ule ambapo Petro anaogopa hadi kumkana Yesu hadharani, ndio wakati huo ambapo Nikodemo alijitahidi kumtetea Yesu mbele za Pilato HADHARANI ili asihukumiwe. Wakati wale Mitume 12 wamesambaratika kila mmoja na njia yake, ndio wakati Yusufu wa Arimathaya anapata ujasiri wa kwenda kwa Pilato kuomba mwili wa Bwana kwa mazishi. Kumbuka wale wanawake ambao walimsindikiza Bwana kutokea Galilaya hadi Yerusalemu kwa mguu (hapakuwa na magari). Walitembea na Bwana katika njia ya msalaba hadi Golgotha alikosulubiwa, huku wanalia na kupiga vifua vyao, hawakuogopa kwamba watapata shida, walienda tu hadi dakika ya mwisho Bwana anakata roho. Pamoja na maumivu makali ya mijeledi, njaa, na mateso mfululizo, Yesu anawatuliza wale wanawake, “msinililie mimi, bali jililieni ninyi na watoto wenu, mimi naenda kwa Baba, nimemaliza kazi yangu”.

Kama haitoshi, hawa wanawake hawakurudi nyumbani, wakamfuata Yusufu wa Arimathaya kwa nyuma, katika msafara wa mazishi. Lengo lao ilikuwa kujua wapi mwili wa Bwana umewekwa ili waje baaadae kuupaka manukato huko kaburini. Wakarudi nyumbani kuandaa manukato, bila kujali kwamba Yusufu alishaweka kilo 30 ya manukato mengine pamoja na manemane kwenye mwili wa Bwana. Hawa ni wanafunzi wa SIRI! Hawakusema neno zaidi ya matendo yao. Huku kwenye maandiko hakuna mahali tunaona INJILI yao kwa maneno ila kwa MATENDO yao! Matendo yao yalikuwa zaidi ya maneno yao mbele za watu. Hebu fikiri wale “inner circle” ya Yesu, Akina Petro, Yohana, Yakobo, nk. wako wapi? Matendo yako ni muhimu sana kuonyesha imani yako. Wapi umesimama kwa ujasiri kama hawa wanawake? Hawakuogopa mtu, walifanya kwa bidiii, iliwagharimu muda na pesa (manukato yalikuwa ni kitu cha thamani, ndio maana Yuda alitaka yauzwe ili wakasaidie masikini badala ya kumpaka Yesu). Na hawa wanawake ndio waliojua kwa mara ya kwanza kwamba Bwana wao amefufuka! Matendo yako, matendo yako, matendo yako. Kushuhudia ni sawa, je matendo? Hasa ukiwa mwenyewe, hakuna mtu anakujua kama umeokoka, huko mbali kabisa, unafanya nini? (Luka 23:50-56).

Wakati Bwana anawaaga wanafunzi wake aliwaambia “Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.” (Yohana 14:1-3). Lengo la Yesu ilikuwa sio kuwaacha tu wanafunzi, bali kuja kuwachukua ili akae nao Milele. Ila, kwa sasa, akawaacha ili wafanye “mataifa kuwa wanafunzi” pia wakati huo yeye akiandaa MAKAO. Hili ndio lengo KUU la Yesu kwa wanafunzi wake. Sio kuhubiri tu, kutoa pepo tu, kufanya kazi ya huduma tu, kufanikiwa na mali nyingi tu, nk. Lengo ni wanafunzi kurithi UZIMA wa milele pamoja naye.

Angalia hapa “ndipo wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako. Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme. Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru. Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.” (Luka 10:17-20). Katika kundi kubwa la wanafunzi wa Yesu, aliwapa hawa 70 nafasi ya kufanya mazoezi (practical training). Akawatuma huko wakafanye huduma, lengo ni kuwaonyesha ile mamlaka inavyotenda kazi ili siku moja waendelee na kazi wenyewe. Yesu alijua iko siku, na sio mbali atarudi kwa Baba, kwa hiyo aliwafundisha hawa wanafunzi kufanya kama ambavyo yeye angefanya. Sasa, wanafunzi walipoona pepo wanawatii wakadhani wamefikia LENGO la darasa lao, Yesu akasema, hapo bado, kufanikiwa kihuduma, miujiza, nk. hapo bado, LENGO kuu ni “kuishi pamoja na mimi milele Mbinguni”. “Msifurahi mapepo kuwatii, bali majina yenu yameandikwa Mbinguni”.

Angalia tena hapa, “Naye alikuwa akipita katika miji na vijiji, akifundisha, katika safari yake kwenda Yerusalemu. Mtu mmoja akamwuliza, Je! Bwana, watu wanaookolewa ni wachache? Akawaambia, Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze. Wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango, nanyi mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, Ee Bwana, tufungulie; yeye atajibu na kuwaambia, Siwajui mtokako; ndipo mtakapoanza kusema, Tulikula na kunywa mbele yako, nawe ulifundisha katika njia zetu. Naye atasema, Nawaambia, Siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu. Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno, mtakapomwona Ibrahimu na Isaka na Yakobo na manabii wote katika ufalme wa Mungu, nanyi wenyewe mmetupwa nje.” (Luka 13:22-28). Ukiangalia hii mistari utagundua hawa ni watu waliokuwa WAKIAMBATANA na Yesu. Wanajaribu kumbusha Yesu “nawe ulifundisha katika njia zetu”, yaani hawa walikuwa WANAFUNZI pia! na walikuwa wakihudhuria darasa, walikuwa na Yesu katika maisha yao ya kila siku, wanamkumbusha Yesu “tulikula na kunywa mbele zako”. Bwana anawaambia “ondokeni kwangu ninyi mlio wafanyaji wa UDHALIMU”! Tafsiri nyingine inasema “ondokeni kwangu ninyi mtendao maovu”. Hawa jamaa walikuwa kati ya wanafunzi wa Yesu, ila MATENDO yao yalikuwa ya kidhalimu! Pamoja na kujifunza habari za Yesu, kutembea na kula pamoja Naye, yamkini hata kushuhudia habari za Yesu, ila walifukuzwa kwa sababu walikuwa “wafanyaji wa udhalimu/uovu”.

Nataka uone jambo hapa katika Luka 13: 22-28, “Je! Bwana, watu wanaookolewa ni wachache? Akawaambia, Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze.” Hapa tunaona kuna swala la KUJITAHIDI. Na ukiangalia hawa wanaojitahidi, WAMETAKA kuingia kwenye huu mlango mwembamba, kwa lugha nyingine WAMEUONA mlango ila wameshindwa kuingia. Sasa hii ni sifa ya mwanafunzi ambaye AMEJIFUNZA vizuri darasani, ameelewa na anajua kusema kwa uhodari sana alichojifunza, ila “ni mfanyaji wa udhalimu”! Maneno yake na matendo haviendani! Mlango unambana, kashindwa kupita. Huyu haingii kwenye Ufalme wa Mungu kule ambako Bwana alienda kuandaa makao. Natamani uone hili jambo kwa namna ya ndani kabisa, utizame nafsi yako na kujitathmini vizuri, utizame mlango sawasawa na ujipime kama unaingia au la, kisha uchukue hatua. Swala la kuingia Mbinguni sio lelemama! Hakuna kinyonge kinaingia huko, na Ufalme wa Mungu unatekwa na wenye nguvu, funga viuno sasa na ujipange vizuri.

Pamoja na kwamba Yesu anasema “jitahidini kuingia mlango ulio mwembamba” pia ukisoma mistari hii utagundua kwamba kuna NEEMA iokoayo. Hii neema ina uwezo wa kuwapitisha watu “mlangoni” japo HAWASTAHILI! Kwa lugha nyingine jitihada kwa jinsi ya matendo tu bado sio kitu, kuna sehemu ya Neema. “Basi enendeni hata njia panda za barabara, na wote mwaonao waiteni arusini. Watumwa wale wakatoka wakaenda njia kuu, wakakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema; arusi ikajaa wageni. Lakini alipoingia yule mfalme ili kuwatazama wageni wake, akaona mle mtu mmoja asiyevaa vazi la arusi. Akamwambia, Rafiki, uliingiaje humu nawe huna vazi la arusi? Naye akatekewa. Mfalme akawaambia watumishi, Mfungeni mikono na miguu, mchukueni mkamtupe katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache.” (Mathayo 22:9-14) Angalia vizuri hapa, pamoja na kwamba hawa jamaa hawakuwa wazuri sana kwa matendo yao, yaani “wakakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema”, SIFA iliyowastahilisha ilikuwa VAZI la ARUSI. Wokovu ni vazi. Sasa hii tunaita Neema kwa sababu wale walioalikwa arusini hawakuwa tayari. Hawa wengine waliokusanywa huko barabarani wameingia arusini kwa sababu walipoitwa walikuja (utayari wao), ila LAZIMA wawe na VAZI! [wokovu ni bure, na ni mara moja (obtained), ila kuwa mwanafunzi ni mchakato (attained)].

Sasa tuone tofauti kati ya mwanafunzi na mteule. Mwanafunzi ni mtu yeyote anayejifunza habari za Yesu, kutenda na kuishi maisha ya imani kama Yesu anavyotaka. Mteule ni kundi dogo kati ya hawa wanafunzi ambalo litaurithi uzima wa milele. Ninaita kundi dogo kwa sababu “waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache”. Ni kweli kabisa sifa ya mwanafunzi ni lazima aokoke, yaani amkubali Yesu kama Bwana na Mwokozi wa maisha yake. Hiyo ni hatua ya kwanza tu, ila tunaambiwa “atakayevumilia hadi mwisho ndiye atakaye okoka”. Kwa lugha nyingine, mwanafunzi atakayevumilia hadi mwisho ndiye mteule. Kama hujajua, ngoja nikupashe habari. Hii njia imesonga na ni nyembaba, kuna misukosuko na vurugu nyingi. Inakupasa kuwa “kondoo” ili ukae katika zizi japo una Simba wa Yuda ndani yako. Unahitaji kuvumilia ndugu, jua mateso na majaribu huja kukomaza imani yako na sio kukuangusha. Vumilia tu, Bwana anaona. Ukivumilia mpaka mwisho, UTAOKOKA. Kipimo cha WOKOVU ni MWISHO sio MWANZO.

Neema na izidi kwenu mnapojifunza na kumtafuta sana huyu Mwana wa Mungu aonekane kwenu.

Frank Philip.


 Bali wote waliompokea(YESU KRISTO) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; -Yohana 1:12

Comments