Je! WEWE ni MWANAFUNZI wa YESU?-sehemu ya 2






1b. Je! Mwanafunzi wa Yesu ni mtu wa namna gani?

Wanafunzi waliitwa:
“Simoni Petro alipoona hayo, alianguka magotini pa Yesu, akisema, Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana. Maana alishikwa na ushangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye, kwa sababu ya wingi wa samaki walioupata; na kadhalika Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, waliokuwa washirika wa Simoni. Yesu akamwambia Simoni, Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu. Hata walipokwisha kuviegesha pwani vyombo vyao, wakaacha vyote wakamfuata.” (Luka 5:8-11).

Mistari hii inatuambia wakati Petro na wenzake wakiwa kazini, wanavua samaki, Yesu akaenda pande hizo kuhubiri. Siku hiyo alitumia mtumbwi wa Petro kuhubiria. Baada ya hapo akamwambia Petro “shusha nyavu”. Hadithi hii imejirudia kwa wanafunzi wengine. Wote 12 “waliitwa kumfuata Yesu” japo kuna wengine “walimfuata Yesu kabla ya kuitwa”. Lakini nataka uone hapa, “Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu. Hata walipokwisha kuviegesha pwani vyombo vyao, wakaacha vyote wakamfuata”. Baada tu ya kupata samaki wengi sana, biashara kuchanua kwa ghafla, Yesu anamwambia Petro, “tangu sasa” sio kesho. Hebu fikiri wale samaki wengi waliovua ilikua je? Waliwaacha ufukweni na kumfuata Yesu! Baada ya kushangilia WINGI wa samaki na kufanikiwa kwa uvuvi wao, ghafla! Petro anagundua ni mwenye dhambi! Neno “usiogope” Yesu alilosema, lilimwondoa hofu na mashaka na kutangaza MSAMAHA, na kilichotokea “waliacha vyote UFUKWENI na kumfuta Yesu”. Hii inanionyesha kwamba kuna hatua ya KUTUBU (kuacha vyote) ili uwe mwanafunzi wa Yesu.

Kuna wengi pia walifeli kwenye hatua ya mwanzo tu ya “kuitwa”. Baadhi yao walikua wanataka kumfuata Yesu kwa sababu ya kupata faida fulani kwa jinsi ya mwilini, na Yesu akawanyesha kwamba hana kitu kwa jinsi ya mwilini, japo ni Mungu. Kumbuka, tunapaswa “kuutafuta KWANZA Ufalme wa Mungu na HAKI yake, na mengine tutazidishiwa”, ukigeuza hii sentensi, na kuanza kutafuta MENGINE kwanza, ndio Ufalme wa Mungu baadae, tarajia kukutana na jibu kama hili, “nao walipokuwa wakienda njiani, mtu mmoja alimwambia, Nitakufuata ko kote utakakokwenda. Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana pa kujilaza kichwa chake.” (Luka 7:57,58).

Wengine waliitwa kabisa, ila walikuwa na mambo yao ya KIPAUMBELE cha juu zaidi kuliko mambo ya Yesu, wakafeli pia. Kumbuka hawakukataa wito, ila walikua na AGENDA zao binafsi muhimu za kutimiza ndio wamfuate Yesu, ona hapa “akamwambia mwingine, Nifuate. Akasema, Bwana, nipe ruhusa kwanza niende nikamzike baba yangu. Akamwambia Waache wafu wawazike wafu wao; bali wewe enenda ukautangaze ufalme wa Mungu. Mtu mwingine pia akamwambia,” (Luka 7:59,60).

Sasa nataka uone pia kwamba kuna wengine walimfuata Yesu wao wenyewe, baadhi yao walifeli kama huyu hapa“Bwana, nitakufuata; lakini, nipe ruhusa kwanza nikawaage watu wa nyumbani mwangu. Yesu akamwambia, Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu.” (Luka 9:61-62). Kwa sababu ya NIA mbili ndani yao! Sifa moja wapo ya Mungu wetu ni wivu, huwezi kuamua kumfuata Yesu halafu huku nusu duniani na nusu kwa Yesu ukafanikiwa. Hii hali inaitwa “vuguvugu” na Yesu anasema “atawatapika” watu wa namna hii.

Wanafunzi wa siri:
Kuna kundi jingine la wanafunzi wa Yesu walioitwa “wanafunzi wa siri”. Hawa walikuwepo ila walimwendea Yesu kwa siri, na Yesu aliwajua (recognize) pia. Kwa mfano Nikodomo (Yohana 3). Huyu bwana alikua mmoja wa wale Mafarisayo na Wakuu wa dini, kazi yake ilikua MWALIMU wa mambo ya dini/sheria. Yesu akamfundisha habari za kuzaliwa kwa mara ya pili na habari za Roho Mtakatifu. Kwa lugha ya sasa tungesema “akaokoka” (akaanza hatua ya kwanza ya kuwa mwanafunzi wa Yesu). Nikodemo alionyesha kuwa MFUASI wa Yesu ndio maana wakati wa Yesu kuhukumiwa kabla ya kusulubiwa Nikodemo alijitahidi kwa namna fulani kumtetea Yesu ili kumnusuru na adhabu (Yohana 7:50,51). Lakini pia tunamwona Yusufu wa Arimathaya, pia alikua mwanafunzi wa Yesu. Wakati hali imekua mbaya, Bwana amepigwa na kuuwawa, akina Petro na wenzake wametokomea, hawa wanafunzi wa SIRI, Yusufu wa Arimathaya na Nikodemo ndio walifanya MAZISHI ya Bwana. Nikodemu akaleta manemane (uudi) na manukato, zaidi ya kilo 30 (ratili 100), akaweka kwenye mwili wa Bawana, wakauviringisha sanda (ya kitani), na kuuweka kwenye kaburi JIPYA. Hebu fikiri, hawa wanafunzi wa siri walimpendaje Bwana wao? Kilo 30 za mchanganyiko manukato na manemane, kitani na kaburi jipya! (Yohana 19:38-42).

Kujikana:
“makutano mengi walipokuwa wakifuatana naye, aligeuka, akawaambia, Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu” (Luka 14: 25-28).

Kila mtu anajua Yesu hasemi habari za KUWACHUKIA watu hapa, ila anaonyesha hali ya JUU sana ya KUACHA yote, yaani TOBA ya kweli, na kumtanguliza Yesu katika kila jambo, na kumfanya kuwa BWANA katika maisha yao. Toba maana yake ni KUGEUKA, kuungama (kutaja kwa jina) KOSA ulilofanya na kuomba msamaha na KUACHA kufanya hicho ulichotubia. Yesu kuwa Bwana maana yake ni KUMSIKILIZA/KUMTII yeye kwanza kabla ya NAFSI yako na wengine wowote maishani mwako. Kama kuna kitu salama ni KUMWAMINI Yesu anapokuongoza. Hakuna siku atakupoteza. SIFA mojawapo ya muhimu ya mwanafunzi ni KUMWISHIA na KUMTANGULIZA Bwana, ndio maana akatoa mfano mgumu hapa ili watu waelewe vizuri, yaani “Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu”. Kuna mazingira ambayo ni magumu kidogo. Kwa mfano akina Shedrack, Meshack na Abednego, walifika mahali wakasema “hatuli vyakula vya mfalme, tunataka mtama na maji tu, tusije tukajinajisi kwa vyakula vya mfalme tukamkosea Mungu wetu”. Kwa ajili ya Kristo, kuna mambo mengi tu imekupasa “kujichukia” ili umpendeze Yeye.

Wanafunzi 12:
Kulikua na namba kubwa ya wanafunzi wa Yesu ambao majina yao hayapo humu kwenye Biblia. Katika hili kundi kubwa la WANAFUNZI (walioitwa na kumfuata), alichagua 12 kati yao, na jina lao akawaita MITUME. Hebu soma hapa. “Ikawa siku zile aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu. Hata kulipokuwa mchana aliwaita wanafunzi wake; akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita Mitume; Simoni, aliyemwita jina la pili Petro, na Andrea nduguye, na Yakobo na Yohana, na Filipo na Bartolomayo, na Mathayo na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Simoni aitwaye Zelote, na Yuda wa Yakobo, na Yuda Iskariote, ndiye aliyekuwa msaliti.” (Luka 6:12-16).

Ukitaka kuona kulikua na wanafunzi wengi zaidi ya 12 hebu jaribu kuona hapa tena, “Akashuka pamoja nao, akasimama mahali tambarare, pamoja na wanafunzi wake wengi, na makutano makubwa ya watu waliotoka Uyahudi wote na Yerusalemu, na pwani ya Tiro na Sidoni; waliokuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao” (Luka 6:17). Sasa jua neno hili, katika MAKUTANO kulikua na mitume 12, wanafunzi wengine, na umati wa watu. Sio kila aliyemfuata Yesu alikua mwanafunzi wake, na sio kila mwanafunzi wake alikua mtume.

Sifa ya muhimu ya mwanafunzi:
Kuna tofauti ya KUITWA (kuongozwa sala ya toba) na kuwa mwanafunzi wa Yesu. Kuitwa na KUITIKA ni hatua ya kwanza tu, ila unapokaa ndani ya YESU, ukajifunza na kuanza kuzaa MATUNDA, unachukua hatua za kua mwanafunzi. Sasa kumbuka wengi sana walimfuata, hiyo sio tabu, jiulize je! Unazaa matunda? Yesu akasema, “Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.” (Mathayo 15:7,8). Ukiangalia sentensi ya mwisho ni “wakati ujao” yaani “BAADA ya kukaa ndani yangu, kuzaa sana, MTAKUA wanafunzi wangu”. Haianzi kua MWANAFUNZI tu baada ya sala ya toba. Nataka nikupe sababu moja kati ya nyingi, tunaokolewa kwa IMANI, na imani huja kwa KUSIKIA (kutii) Neno la Kristo. Haishii kwenye KUITWA, mwanafunzi hufanya kama MWALIMU wake, unapoanza kuchukua HATUA, kufanya kwa VITENDO tunasema IMANI yake ni HAI kwa maana imani bila matendo imekufa. Sasa, anapoanza kutenda sawa na maagizo ya Yesu, kinachotokea ni kuzaa MATUNDA mema. Unapodumu katika hayo (kuzaa sana) unakua mwanafunzi wake. Hakuna mwanafunzi asiyefanya mambo anayoagizwa na mwalimu wake akawa mwanafunzi! Haiwezekani mtu akae ndani ya Yesu, amsikilize (atii) Anavyomwongoza halafu asizae matunda, ndio maana Yesu anasema “kila tawi lisilo zaa hukatwa na kutupwa” kwa maana sababu moja wapo ya kutokuzaa ni KUTOKUSIKIA Bwana anapokuongoza kufanya mambo fulani.

Utume mkuu:
“Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” (Mathayo 28:19,20). Lengo la Yesu haikua kuita makutano na kuishia kumfuata kama ilivyo leo watu wengi wanafarijika na makanisa/kumbi kujaa bila kujali kama hao watu ni wanafunzi au la. Lengo kuu ilikua KUWAFANYA (process) watu kuwa wanafunzi. Huu ni mchakato ambao unahusisha kufundisha “KUSHIKA” maagizo ya Bwana, kwa lugha nyungine KUISHI kama Kristo. Sasa jiulize, Je! Unaishi maisha yanayofanana ya Yesu? Najua jibu ni HAPANA, au NDIO, au HUNA UHAKIKA, ila Je! Uko katika mchakato wa kumwishi Kristo? Kwa maana haiwezekani unasema wewe ni mwanafunzi wa Yesu wakati “hujaacha yote”! nikimaanisha kuacha dhambi na kufuata njia zako mwenyewe (kukaa nje ya mapenzi ya Mungu). Najua hapa kuna changamoto na mwaswali mengi, ila unachukua hatua za “kujionyesha umekubalika”? Mtume Paulo alitumia hilo neno “kujionyesha umekubalika mtumishi asiye na waa”. Hasa unapokua peke yako, je! Unatunza ushuhuda wa Kristo?

Frank Philip.



 Bali wote waliompokea(YESU KRISTO) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; -Yohana 1:12

Comments