Je! WEWE ni MWANAFUNZI wa YESU?(sehemu ya 1)



Mara nyingi sana watu wamefikiri kila ANAYESEMA ameokoka moja kwa moja anakua ni mwanafunzi wa Yesu. Kumbuka, watu wengi sana walimfuata Yesu, na wengi sana walimwamini, ila alikua na wanafunzi 12, sehemu nyingine tunaambiwa 70, ila pia katika wale wanafunzi 12, kuna wakati alijitenga na wanafunzi 3 wakati akifanya mambo fulani, na pia kuna mahali tunaambiwa kulikua na wanafunzi wa siri. Kuna sehemu nyingine tunasoma uhusiano tofauti na baadhi ya wanafunzi kwa mfano, “yule mwanafunzi Yesu aliyempenda”. Nikifuatilia mistari hii nagundua hatuwezi kujua idadi halisi ya wanafunzi wa Yesu aliokuanao wakati ule na UHUSIANO/UKARIBU aliokua nao na wanafunzi wake tofauti. Swali hili kwamba kila Mkristo/aliyeokoka ni mwanafunzi wa Yesu limenifanya nitamani kujifunza zaidi juu ya maswali yafuatayo: Je! Mwanafunzi wa Yesu ni mtu wa namna gani? Je! Kuna tofauti kati ya mteule na mwanafunzi? Je! Ni lazima mwanafunzi awe mtumishi pia? Je! Kuna kuhitimu katika (kama kumaliza shule) hali ya uanafunzi kwa Yesu? Je! Kuna uhusiano gani wa kumtumikia Mungu na hatua ya uanafunzi wako? Je! Kuna uhusiano gani kati ya kua mwanafunzi na utakatifu/ukamilifu?

1. Je! Mwanafunzi wa Yesu ni mtu wa namna gani?

Maana halisi ya MWANAFUNZI ni mtu anayejifunza CHINI ya MWALIMU. Palipo na mwanafunzi kuna mwalimu/mkufunzi/kiongozi ambaye huyu mwanafunzi anajifunza KUFANYA kama MWALIMU wake afanyavyo. Angalia tena hapa kwa makini, “mwanafunzi anajifunza KUFANYA kama mwalimu wake”. Haimsaidii sana mwanafunzi KUJUA mwalimu anataka nini na HAFANYI vitu ambavyo mwalimu ameagiza kufanya. Mwanafunzi wa namna hii JAPO anaelewa na anajua alichofundishwa hata kukikiri, ATAFELI kwa sababu HAKUFANYA yale ayajuayo kwa sababu kipimo hakipo katika KUSEMA, ila KUFANYA kwa kiwango cha KUFANANA na mwalimu.

Kama KUSUDI la mwanafunzi ni kufanya kama mwalimu (Yesu), basi si budi ujue kwamba kuna GHARAMA ya kua mwanafunzi wa Yesu. Kwa sababu Yesu ALIMTII sana Mungu kwa gharama kubwa, naam, hata mauti ya msalaba, jua kwamba, KUMTII Mungu katika mambo YOTE kuna GHARAMA. Angalia hapa, “makutano mengi walipokuwa wakifuatana naye, aligeuka, akawaambia, Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia?” (Luka 14:25-28). Nataka uone jambo moja hapa, kama Yesu alikua na wanafunzi wake 12 tayari, hawa aliokua anawaambia kwamba “wasipokua tayari kubeba msalaba na kumfuata hawawezi kua wanafunzi wake” ni akina nani? Inamaana kuna kundi kubwa zaidi la wanafunzi kuliko hawa 12! Au alikua akisema juu wa wale ambao baadae wangeamua kuwa wanafunzi wake kama mimi na wewe, na akawa anatoa jinsi imempasa mwanafunzi kuwa.

Kusudi la somo hili ni kutaka kukusaidia uweze kujitathmini na ujue kama wewe ni mwanafunzi wa Yesu na uchukue hatua. Haikusaidii sana kubeba majina ya dini au madhehebu fulani huku ukijiona BORA kuliko wengine. Kumbuka hayo madhehebu yako hayakuwepo wakati wa akina Petro, ila WANAFUNZI wa Yesu walikuwepo. Kama unadhani dhehebu lako, au “ile” sala ya toba uliyoongozwa ndio umemaliza kazi na sasa umefuzu kua mwanafunzi wa Yesu, jiulize tena vizuri na kuchukua hatua zipasazo.

Frank Philip.
NB: Majibu ya maswali mengine yatafuata hapo punde.


 

 Bali wote waliompokea(YESU KRISTO) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; -Yohana 1:12

Comments