KUMSHUKURU MUNGU




Kumshukuru Mungu imekuwa utamaduni na taratibu za ibada za dini mbalimbali. Lakini je! Kumshukuru Mungu kuna maana gani? Au umuhimu wake ni nini? Nimetamani tujifunze hili jambo ambalo Daudi amesisitiza mara nyingi katika Zaburi akisema “nitamshukuru BWANA kwa ajili ya haki yake na nitaliimbia sifa jina la BWANA Aliye Juu Sana” (Zaburi: 7:17) Na pia Daudi anahimiza watu wengine wamshukuru Mungu kwa kusema “Mshukuruni BWANA, kwa kuwa ni mwema, upendo wake wadumu milele.” (Zaburi 118:1)

Kati ya mambo mengi muhimu nataka tuone haya machache kwa ufupi:

i). Huwezi kumshukuru Mungu kwa DHATI kama HUNA cha kushukuru

Kama kuna jambo gumu ni kushukuru kwa DHATI kwa ajili ya jambo ambalo hulijui. Kwa kweli utabaki kushukuru kwa sababu mtumishi wa Mungu amesema “mshukuruni Mungu” na wewe ghafla unaanza “asante Yesu, asante Yesu, asante Yesu”, lakini hayo maneno yanatoka hapo kinywani tu na wala sio Moyoni kwa sababu ndani ya MOYO wako HUONI kitu Mungu amefanya na ukijaribu kuvuta hisia haziji basi unaanza tu kushukuru kama kasuku. Ukiangalia hapo pembeni unaona mwenzako anashukuru huku machozi yanamtoka, japo wote wawili mnatamka maneno yale yale “asante Yesu, asante Yesu”. Sasa kuna tofauti ya “asante Yesu” ya kwako na ya mwenzako. Na tofauti haiko katika maneno yenu ila MIOYO yenu. Kumbuka kulia sio ishara ya SHUKURANI ya dhati japo inawezakuwa pia.

Daudi anasema “Msifuni BWANA. Mshukuruni BWANA, kwa kuwa ni mwema, upendo wake wadumu milele. Ni nani awezaye kusimulia matendo makuu ya BWANA au kutangaza kikamilifu sifa zake?” (Zaburi 106:1,2) “Mshukuruni BWANA, kwa kuwa Yeye ni mwema, upendo wake hudumu milele. Waliokombolewa wa BWANA na waseme hivi, wale aliowaokoa kutoka katika mkono wa adui, wale aliowakusanya kutoka nchi mbalimbali, kutoka mashariki na magharibi, kutoka kaskazini na kusini.” (Zaburi 107:1-3).

Kama UMEONA wema wa Mungu, Upendo wa Mungu, na Matendo ambayo Mungu amekutendea, ukienda mbele zake kwa kumshukuru, utagundua HUNA maneno ya kusimulia huo ukuu wake, ndio maana watu wengi sana wakianza kumshukuru Mungu kwa DHATI huanza kulia tu. Hebu chukua muda kutafakari mambo MENGI ambayo Mungu amekutendea na nenda mbele zake kwa DHATI kabisa KUSHUKURU tu, sio kuomba, zama katika Moyo wako kushukuru huku ukibeba hayo mambo mbele za Mungu na Roho Mtakatifu atakusaidia kuona kitu Daudi anasema hapa.

ii). Ukubwa wa SHUKURANI zako unategemea UKUU wa Mungu unaouona

“BWANA ni nguvu yangu na ngao yangu, moyo wangu umemtumaini yeye, nami nimesaidiwa. Moyo wangu unaruka kwa furaha nami nitamshukuru kwa wimbo.” (Zaburi 28:7) Daudi alipita VIPINDI ambavyo aligundua, “kwa kweli hapa sio nguvu zangu ila ni nguvu za Mungu”, alipotizama hayo mambo, anasema “moyo wangu unaruka kwa furaha, nami nitamshukuru Mungu kwa wimbo”. Sasa mafanikio yetu yamekuwa KIKWAZO cha kumshukuru Mungu kwa DHATI kwa sababu mara nyingi tumeona jinsi ambavyo tumefanikiwa kwa JITIHADA zetu au kwa misaada ya watu FULANI. Kila ukitafakari HATUA za maisha yako moyoni unasema “kwanza familia yetu tuna akili sana, wote tunefaulu tu, ndio maana hata sasa nimefaulu”, au “kwa kweli namshukuru sana fulani, kama asingenilipia ada ungekuta sijasoma”, au “nafahamiana na fulani, naye anacheo kikubwa, ndio maana niliweza kuvuka mahali fulani”, au “kwa kweli nimefanya kazi kwa bidii sana, vyeti vyangu ni vizuri sana, hii nafasi ya uongozi katika ofisi ni halali yangu”, au “ndugu hapa mjini ni kufahamiana, usipomfahamu mtu utapata shida”, nk. Katika MAMBO yote hayo HUKUMWONA Mungu ila NGUVU zako, JITIHADA zako, nk. na ukiambiwa “mshukuru Mungu”, huku ndani unakuwa mkavu sana kwa sababu huoni ni kwa namna gani Mungu amekupitisha hadi hapo ulipo, bali watu na pesa zao, au jutihada zako.

Hebu fikiri Daudi anasema “nijapopita katika bonde la uvuli wa mauti” na sasa amepita yuko ng’ambo. Hebu fikiri kiwango cha SHUKURANI atakacho kimimina kwa Mungu wake? Sasa kumbuka wakati anapita katika hayo MAGUMU kiasi cha kuona “mauti”, ndani ya moyo wake anapata FARAJA kwa sababu anaona “ulinzi wa gongo na uongozi wa fimbo yake”, anapata furaja japo ADUI wamemzunguka, hadi pale “mezani pake”, anaposema “sasa ngoja nile”, adui zake wapo hapo pia! Na hawamtakii mema, wanataka kumwamngamiza. Mungu anampigania katika hizo HATUA zote na sasa yuko nga’ambo! Hebu fikiri kiwango cha shukurani kwa Mungu ambazo Daudi atamimina? Sasa mara nyingi sana tumefunika macho na masikio yetu, tumejitahidi kwa njia zetu za uovu au akili zetu na tumefanikiwa hapa na pale na hatukumwona Mungu, tunajiona sisi na watu wengine tu. Sasa nisikilize vizuri, hata kama hukumwona Mungu akikupigania jua hapo ulipo sio wewe mwenyewe na hukufanikiwa kwa nguvu zako. Mwombe Mungu akupe kuona MKONO wake ulivyokupigania ili uweze kuwa na SHUKURANI za dhati mbele zake.

Daudi anasema “Nayainua macho yangu nitazame vilima, msaada wangu utatoka wapi? Msaada wangu hutoka kwa BWANA, Muumba wa mbingu na dunia.” (Zaburi 121:1). Ukiyatizama maneno haya ya Daudi utapata picha ya mtu aliyoko mahali kusiko na watu, peke yake na ametingwa. Sasa usifikiri Daudi alikuwa peke yake kwa jinsi ya mwilini. Lakini Moyo wake ulikuwa umemwelekea Bwana kwa kiwango kwamba anaona MSAADA wake WOTE unatoka kwa Bwana. “akiinua macho anaona milima tu”, sasa hebu fikiri amepanda hiyo milima na yuko “kileleni”, halafu anasogea mbele za Mungu kwa shukurani? Nataka uone tofauti ya shukurani na shukurani ili ujifunze KUMSHUKURU Mungu kwa dhati.

iii). Kuna uhusiano wa KUMPENDA Mungu na kiwango cha SHUKURANI umpazo

Watu wengi sana HUENDA mbele za Mungu kwa MAOMBI kwa bidii sana wakiwa na SHIDA, UHITAJI, VITA, nk. Wakati wakiwa katika KUOMBA na KUFUNGA, huwa wanakuwa WATAKATIFU sana. Wanajitahidi kusoma Neno na kukaa karibu na Mungu. Wakifanikiwa KUPATA walichokuwa wanaomba, wanamshukuru Mungu na kuweka SILAHA chini. Sasa wanashangilia ushindi na kumsahau Mungu wao na wengine kwa KUPITIA hizo NAFASI, VYEO na MALI walizokuwa wanamlilia Mungu, sasa wanamtenda Mungu dhambi. Hakuna tena shukuruni ndani ya mioyo yao sasa ni KIBURI na kuwatizama wengine kama HAWANA imani!

Kwa upande wa pili, kuna watu wengine pia HUENDA mbele za MUNGU kuomba juu ya mahitaji mbali mbali, vita, cheo, pesa, nk. WANAPOFANIKIWA huuona UKUU wa Mungu na KUMSHUKURU Mungu kwa DHATI kabisa. Yale mambo ambayo Mungu amewafanyia yanawavuta KARIBU zaidi na Mungu. Hayo mambo yanawafanya wanazidisha UPENDO wake kwa Mungu na wanazidi KUMTUMAINI na kutangaza UKUU wa Mungu.

Katika haya makundi mawili ya watu, kiasi cha SHUKURANI zao kwa Mungu kinaathiriwa na UPENDO wao kwa Mungu. Na kinachoonyesha kwamba kundi la kwanza hawampendi Mungu ni matendo yao. Yesu anasema “mkinipenda mtazishika amri zangu”, na pia tunasoma, “tukipenda ulimwengu na mambo yake [uzinzi, tamaa mbaya, nk.], kumpenda Mungu hakumo ndani yetu”. Sasa unajua huwezi kumshukuru kwa dhati mtu usiye mpenda! Na ukimshukuru, utamshukuru kwa muda huo tu mfupi akiwa hapo na akikupa kisogo unasahau habari yake. ILA mtu unayempenda, ULE upendo unawaka kila saa ndani, na unakumbuka yale mambo mazuri aliyokutendea, moyoni kunajaa shukurani kila mara, kwa sababu ya UPENDO!

iv). Sio mambo YANAYOKUFURAHISHA tu yanastahili shukurani

Tunahimizwa na kuambiwa “shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu.” (1Wathesalonike 5:18). Kama kuna wakati mgumu unapoenda mbele za Mungu au unaona kabisa hapa NIMEPIGWA, au nimeshindwa, halafu unaambiwa eti, “shukuru tu maana hayo ni mapenzi ya Mungu!” Ndipo utagundua kwamba hata kushukuru nako kunahitaji IMANI! Hebu tuangalie mfano wa Ayubu kidogo. “Ndipo mkewe akamwambia, Je! Wewe hata sasa washikamana na utimilifu wako? Umkufuru Mungu, ukafe. Lakini yeye akamwambia, Wewe wanena kama mmoja wa hao wanawake wapumbavu anenavyo. Je! Tupate mema mkononi mwa Mungu, nasi tusipate na mabaya? Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi kwa midomo yake.” (Ayubu 2:9,10). Kama kuna mahali ambapo unahitaji IMANI ni pale mambo yanapoenda vibaya halafu “usimtende Mungu dhambi kwa kinywa chako” bali umshukuru. Na Ibilisi anajua hii siri, anapoona umefika mahali pa kuanguka, anakuja kama mke wa Ayubu, kukuzomea na kukuonyesha “ona sasa umeshindwa hapo na unasema umeokoka?”. Ayubu akaona ni UPUMBAVU tu kumshukuru Mungu wakati ukipata mema ila mabaya yakija haushukuru! Akasema “Bwana alitoa na sasa ametwaa, Jina lake lihimidiwe.” Kumbuka siku zote, shukurani utoayo kwa DHATI katika kipindi kama hiki cha mapito magumu ina THAMANI kubwa mbele za Mungu kuliko ile shukurani ya kushangilia USHINDI.

v). Kumshukuru Mungu kwa DHATI kunategemea IMANI yako kwa Mungu

Imani ni kuwa na “HAKIKA ya mambo ya jayo na ni BAYANA ya mambo yasiyoonekana”. Huwa nasikia mara nyingi watumishi wengi wa Mungu wanasisitiza kukiri UPONYAJI au MAJIBU ya maombi yako, na hata KUSHUKURU kwamba Bwana ametenda. Nilichogundua ni kwamba kama huna IMANI ya kwamba UMEPOKEA huwezi kushukuru kwa DHATI. Kumbuka ni vigumu kutafsiri IMANI, ila anayeamini anajua kwamba anaamini au la! Sasa ukifika mahali una MASHAKA ndani yako, kwamba “hayo uliyoomba yamekuwa yako”, ni vyema kushukuru ila nakushauri UENDELEE kuomba hadi utakapo sikia KIBALI cha ndani, ule uthibitisho wa ndani kwama TAYARI imekuwa, sasa hapo endelea kushukuru kwa maana katika hatua hiyo unaweza kumshukuru Mungu kwa DHATI. Sasa sikukatazi kumshukuru Mungu katika HALI zote, ni vyema kabisa kufanya hivyo, ila kuna namna unaenda mbele za Mungu na unasikia “kufunguka huku ndani”, hiyo ni hatua nzuri sana ya kumimina shukurani. Pili, imekupasa kujua KUSHUKURU hakumpindishi Mungu kufanya kitu ambacho hajakusudia kufanya. Kuna idadi kubwa sana ya watu hawasimami katika nafasi zao na kutimiza wajibu wao ila wako busy KUSHUKURU kwa miujiza na ahadi zisizo wahusu wakidhani zitakuwa zao. Uwe na hekima, usipoteze muda. Tafuta uso wa Mungu na tembea katika kusudi lake nawe utafanikiwa na UTAMSHUKURU Bwana Mungu wako aliyekuvusha.

Mungu atusaidie kuona hii siri katika kumshukuru katika mambo yote na tusikose SHUKURANI za DHATI mbele zake kila siku. AMEN.

Frank Philip.


 
 Bali wote waliompokea(YESU KRISTO) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; -Yohana 1:12

Comments