Maaskofu, wachungaji na waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, wacharuka na kuvamia Kituo cha Polisi cha Karagwe

Maaskofu, wachungaji na waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, wamecharuka na kuvamia Kituo cha Polisi cha Karagwe wakipinga Mchungaji wao, Jackson Kanyiginya, kunyimwa dhamana katika mazingira tata na kuswekwa rumande. 
Mchungaji huyo ambaye jana alipandishwa kizimbani kwa kosa la kumpiga mfanyabiashara, Joseph Gareba, alinyimwa dhamana baada ya Mwendesha Mashitaka, Meja Juma Litafa, kuzikataa barua za wadhamini hadi azifanyie uhakiki. 

Akizungumza kutoka Karagwe, Askofu mstaafu wa KKKT Dayosisi ya Karagwe, Bagonza, alisema mchungaji Jackson alikuwa kwenye mkutano na viongozi wote wa kanisa hilo kwa ajili ya kufanya mafungo. 


Alisema akiwa katika kituo cha mafungo, alipata wito wa polisi wa kumtaka afike mahakamani juzi kwa ajili ya kujibu kesi iliyofunguliwa kwa siri ya kumpiga Gareba. 


Alisema baada ya kufika polisi, Mchungaji Jackson jana hiyo hiyo alipandishwa kizimbani na kukana shitaka la kumpiga Gareba kisha kupewa dhamana. 


“Baada ya kufikishwa mahakamani, mchungaji alisomewa mashitaka ya kumpiga Gareba, alikana na kupewa dhamana. 


“Wadhamini wawili ambao ni maofisa watendaji wa vijiji na kata, walijitokeza na barua zao lakini mwendesha mashitaka alizikataa barua hizo eti hadi azifanyie uhakiki ili kujiridhisha, hivyo akaagiza mchungaji aende selo katika Gereza la Kayanga la Karagwe hadi Februari 26,” alisema Askofu Bagonza. 


Kwa mujibu wa askofu huyo, viongozi wa kanisa hilo waliokuwa kwenye mafungo walikatisha mafungo yao na kuwaita baadhi ya viongozi na waumini wao na kukusanyika katika Kituo cha Polisi cha Karagwe kudai Mchungaji Jackson aachiwe kwa dhamana, kwa kuwa masharti ya dhamana yake yalijitosheleza. 


“Leo tumekatisha mkutano wa mafungo, tumekuja hapa polisi tangu saa moja kujua hatima ya mchungaji wetu. Tupo na maaskofu wengine Paulo Mkuta na Nelson Kazoba, tumeandaa tamko tumemkabidhi Kamanda wa Polisi wa Mkoa na hivi sasa mchungaji ameachiwa kwa dhamana tunaingia kanisani kusali,” alisema. 



Akizungumzia chanzo cha mzozo huo, Askofu Bangonza alisema mfanyabiashara Gareba alikuwa na kesi ya ardhi na kanisa tangu miaka ya 1980 na mahakama iliagiza ardhi hiyo isiguswe hadi kesi itakapomalizika. 


Alisema mwaka jana mfanyabiashara huyo aliingia kwenye eneo hilo na kuanza kukata miti, lakini waumini walipoona hali hiyo walimjulisha Mchungaji Jackson. 


“Mchungaji alichokifanya, alikwenda polisi, akachukua askari wakaenda kumkamata Gareba na kumuweka ndani, lakini baadaye alitoka na kesi yake ya kuvunja amri ya mahakama ilifutwa katika mazingira ya kutatanisha,” alisimulia. 


Kwa mujibu wa Askofu Bagonza, baada ya tukio hilo, mfanyabiashara huyo alikwenda kufungua kesi ya kupigwa kwa siri bila kanisa kujua hadi juzi Mchungaji Jackson alipoitwa polisi na kufikishwa mahakamani. 


Askofu huyo alivilaumu vyombo vya dola kwamba tukio la kukamatwa na kutupwa rumande kwa mchungaji wao lina harufu ya rushwa. 


“Rushwa imetufikisha mahala pabaya. Wapo vijana walioajiriwa kwenye mahakama zetu wanasema wanapokea rushwa kwa sababu wanataka kurejesha mikopo waliyopewa na serikali wakati wakisoma. 


“Leo kanisa limeandamana kwa sababu mtu wetu kaguswa, jiulize wapo wangapi wanaonewa?” alihoji askofu huyo.
 

                                                credits: Tanzania Daima
 
 
 
 
Bali wote waliompokea(YESU KRISTO) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; -Yohana 1:12

Comments