Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste nchini (PCT), limedai kusikitishwa na
 kitendo cha Serikali kuwabagua katika uteuzi wa wajumbe wa Bunge 
Maalumu la Katiba. 
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa 
Baraza hilo, Askofu David Batenzi, alisema wao ni miongoni mwa taasisi 
kubwa za kidini iliyo wasilisha majina serikalini kama walivyoagizwa.
Alisema Serikali inapaswa kukomesha mara moja ubaguzi wa kidini nchini 
ambao kimsingi umekuwa ukigawa watu kwa makundi ukitawaliwa na siasa, 
udini na ukabila. 
Aliongeza kuwa, kama Serikali itaendelea kung'ang'ania msimamo wa kutaka
 wajumbe wa Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste wasihusike Bunge hilo, 
wataitisha Mkutano Mkuu ambao utajumuisha Maaskofu wote nchi nzima.
Wengine ambao watahusika na mkutano huo ni mitume na wachungaji wote ili
 kutafakari kwa pamoja hatima ya kutengwa na serikali ya Chama Cha 
Mapinduzi (CCM) na kuchukua hatua ili haki iweze kutendeka kwa vizazi 
vijavyo. 
"Katika kutafakari mwenendo wa uongozi wa Serikali tangu awamu ya kwanza
 hadi ya nne, tumeona kuna mfumo dume unaofanya ubaguzi wa makusudi kwa 
baadhi ya makundi ya kidini na kukumbatia makundi mengine ya kidini.
"Hali hii imesababisha makundi mengine kuporwa haki zao za msingi 
wanazotakiwa kupewa na Serikali...utafiti uliofanywa hivi karibuni, 
unaonesha hali ya udini, siasa na ukabila ambao unajitokeza sana katika 
nchi yetu," alisema.
Alisema ubaguzi huo hujitokeza hasa unapofika wakati wa kuamua masuala 
muhimu yenye manufaa kwa ajili ya nchi pamoja na vizazi vijavyo.
Askofu Batenzi alisema Kamati Kuu ya Utendaji ya PCT Taifa, katika kikao
 chake cha Desemba 5,2013, walichagua majina ya watu walioona wanafaa 
kuchaguliwa katika Bunge hilo, lakini hakuna hata mmoja aliyechaguliwa.
Aliongeza kuwa, si mara ya kwanza kwa Serikali kupuuza mapendekezo ya 
Wapentekoste bali imekuwa ikiwabagua kila yanapojitokeza masuala muhimu 
yanayohusu uwakilishi wa kidini katikaTaifa. 
"Kwa muda wa miongo miwili, Wapentekoste tumekuwa tukinyimwa haki na 
Serikali ikiwemo ya kushiriki katika mambo ya msingi ya kitaifa.
"Serikali haitushirikishi katika sherehe za kitaifa kama inavyofanyika 
kwa taasisi nyingine za kidini, maombi ya dua wakati Rais mteule 
anapoapishwa na kuwekewa masharti magumu ya vibali vya mikutano ya 
injili," alisema. 
Alisema pengine Serikali inaona Wapentekoste hawana sifa za kuchaguliwa 
katika Bunge hilo hivyo ikaamua kuteua majina ya wajumbe kutoka taasisi 
nyingine zikiwemo za Waislamu, Wakatoliki, Walutheri, wengine binafsi 
Tanzania Bara, Visiwani na kuwaacha wao.
"Baraza la Kiislamu wamepewa nafasi 10, Baraza la Maaskofu wa Kanisa 
Katoliki (TEC) wajumbe watatu, Walutheri (CCT) wajumbe watano na wawili 
binafsi lakini PCT hakuna hata mmoja.
Kwa Upande wake, Mjumbe wa Baraza la Utendaji ambaye pia ni Askofu wa 
Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zakaria Kakobe, alisema 
wamechoshwa kubaguliwa na Serikali hivyo watasimama kutetea haki yao.
                                     
Source:Majira

Comments