NENO LA UFAHAMU KWA MWANAFUNZI WA KWELI WA YESU KRISTO.

Na Sam Balele


Nataka niweke ufahamu mmoja wazi hapa ili wale watakaoupokea wafaidike nao, na yule ambaye ataona ni upuuzi basi atauweka pembeni na hasara itakuwa ni kwake wala si kwangu mimi. Ni hivi kuna watu wa aina mbili linapokuja suala la Maswali na Majibu, na hapa naongelea kwa yale yanayohusu mambo ya Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, na Imani katika Kristo Yesu.

(1)Kuna mtu atauliza swali akiwa na nia ya kujifunza kitu kwa vile ni kweli anataka kujifunza, na mtu wa aina hii huwa anakuwa amepata neema kwa Mungu, ni Mungu mwenyewe anakuwa ameufungua moyo wake ili kumpa ufahamu na ufahamu huo ukiingia ndani ya moyo wake basi uweze kumponya, kama ilivyokuwa kwa yule mwanamke Lydia pale ziwani, kama ilivyokuwa kwa Nikodemo, kama ilivyokuwa kwa Kornelio na wengineo. Hawa walikuwa na maswali nafsini mwao, na majibu yalipotoka yaliwafungua. Kule kuwa kwao na maswali hakukuwa kwa hila, la hasha bali kulikuwa kwa kweli na kwa uhitaji hasa, kwa nia hasa ya kutaka kupata ufahamu. Kulikuwa na kiu ya kuifahamu Kweli, na walipoisikia Kweli, ile Kweli ikawaweka huru. Na kweli yatokana na Mungu pekee akiwatumia watumishi wake ambao ni wanadamu.

(2)Kuna mtu atauliza swali akiwa na hila moyoni mwake, na aina hii ya watu hata Bwana Yesu alikumbana nayo sana, na mara nyingi hakuwa anawajibu moja kwa moja, kulikuwa na hekima ya kiungu ndani yake akiongozwa na Roho Mtakatifu katika kuwajibu watu wa aina hii. Maswali yao yalikuwa si kwa ajili ya kuhitaji ufahamu bali kumtega na kuzusha malumbano ya kimaandiko ama kihistoria ama namna yoyote ile. Watu wa namna hii, wakati anapouliza swali tayari anakuwa amejihifadhi katika ngome yake ya fikra, si kwamba anakuwa amejiandaa moyo wake kukusikiliza, la hasha, anakuwa amejiandaa kwa kitu kingine kabisa. Hivyo anakuuliza huku amejiandaa kupangua jibu utakalompa, na wakati mwingine anakuwa anajua kabisa utampa jibu gani, hivyo anakuwa anataka kukuingiza katika mabishano na malumbano yasiyo na faida yoyote kwako na Ufalme wa Mungu katika Kristo Yesu.

Sasa si kila mtu ni wa kumjibu swali analouliza, labda kama na wewe uwe ni mtu usiyejua nafasi yako katika Kanisa la Kristo, si kila mtu ni wa kumjibu, tena Biblia inasema "mjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake", tena inaelekeza juu ya kutunza kinywa na maneno tusemayo, sasa katika social networks it translates katika kutunza VIDOLE, Oh haleluya. Si lazima ujibu swali lolote linalokuja mbele yako. Na ikiwa unajibu basi mjibu kwa jinsi ya kumuachia alama huyo aliyeuliza, Mungu huwa anawafuatilia hawa watu wa aina hii. Ikiwa ni mwana wa amani basi amani itampata tu na ikiwa si mwana basi atakula ghadhabu ya Mungu katika majira yake. Manake kuna vyombo vya rehema na vyombo vya ghadhabu. Ndomana Bwana alisema kwa wale Thenashara 70 wakati anawatuma wawili wawili kuwa, mkiingia katika nyumba na salamu yenu ya amani ikakosa reception iacheni hiyo nyumba go to the next house, hakuwaambia walazimishe na kutengeneza ligi ya mabishano, majibizano na malumbano. Usitengeneze vita ya maneno ambayo Roho Mtakatifu hajakupa kibali.
Msikilize Roho Mtakatifu sikuzote, hili ni suala la kujifunza kumsikiliza.

Ikiwa unaongozwa na Roho Mtakatifu daima utakuwa na jibu sahihi kwa kila swali unaloulizwa. Daima hautojikuta katika majibizano yasiyo na faida na mtu mwenye hila. Bwana Yesu hakuwahi kujibizana na wenye hila mioyoni mwao. Majibu yake yalikuwa mafupi na yenye hekima ya kiungu, na ndivyo impasavyo mwanafunzi wa Yesu Kristo kuwa kama alivyokuwa Bwana wake. Si lazima umjibu mtu swali lake la kipumbavu lisilo na nia ya kuhitaji msaada wa kumtoa kifungoni.

WEWE MLENGWA WA HILI NENO, NAKUOMBEA KWA MUNGU AKUPE KUELEWA HILI NENO.


 

 Bali wote waliompokea(YESU KRISTO) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; -Yohana 1:12

Comments