NJIA YA KUPATA MAMBO YOTE NI KUTAFUTA JAMBO MOJA!

 Na mtumishi wa MUNGU,Frank Philip.


“ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao” (2Nyak:7:14).

Angalia lengo la MSINGI la kuomba/maombi, “kuutafuta USO wa Mungu”, angalia jambo Mungu anataka kwako “kuacha njia zako mbaya”. Sasa hakuna mahali hapa unaona “ukiomba kwa bidii uponyaji wa nchi yako, Mungu ataiponya”! Ila ukiutafuta USO wa Mungu, na kuacha njia zako mbaya, ghafla! Mungu anaanza kushughulika na nchi (mambo yanayokuhusu), jambo moja baada ya jingine yanapanguka tu. Hata adui zako wataanza kuwa na hofu juu yako kwa sababu watauona Mkono wa Mungu akitenda kazi juu yako na mioyo yao inayeyuka mbele zako, “njia za mtu zikimpendaza Mungu....Hata adui zake humpatanisha naye”. Umewahi kujiuliza wakati Musa anarudi kutoka mlimani, sura imebadilika, watu wanapata shida hata kumwangalia kwa sababu ya ule utukufu? Hebu fikiri kwamba Musa alienda kuomba kwa ajili ya shida moja moja za hawa watu wote na shida zake pia? No! Musa alienda kuutafuta USO wa Mungu, alipouona, ilikua ni majibu ya mambo mengi kwa pamoja.

Wakati tunaagizwa kwamba “utafuteni kwanza UFALME wa Mungu na HAKI yake na hayo MENGINE mtazidishiwa.” Sio kwamba Mungu haoni MATATIZO ya msingi kabisa yanayokukabili katika maisha yako. Mungu anajua kwamba unashida zaidi ya elfu! Katika kukusaidia anakuambia, “achana na kutafuta majibu ya shida zako, nitafute KWANZA mimi Mungu, na HAKI yangu na hayo mengine utazidishiwa”. Angalia hapa tena, “hayo mengine”, inamaanisha mambo yako MENGI yanayokukabili au unayohitaji utazidishiwa.

Ukiona kila siku unamwibukia Mungu na list ya matatizo tu, mahitaji ya mwilini tu, pesa tu, mali tu, mchumba tu, nk. Jua umeanza kupita njia ya mwinuko. Hatusemi kwamba hutafika, ila hiyo njia ni ya mwinuko. LAKINI, kama utautafuta uso wa Mungu kwa bidii, na kuacha njia zako mbaya, jua katika ulimwengu wa roho umeanza kutembea njia ya mteremko, kwa maana Mungu ataanza kujibu mambo yako Mengi zaidi kuliko uombavyo na utamwona dhahiri katika njia zako. Mkumbuke Suleiman, alipokusudia jambo moja, “kufanya kazi ya Mungu na kumpendeza”, halafu Mungu akachunguza ndani ya moyo wa Suleiman na hakuona “ubinafsi”, akasema kwakuwa hukutaka “mambo yako binafsi”, mali, adui zako washindwe, nk. Basi nakupa “hayo yote”! Jifunze hii tabia ya Mungu. Suleiman, akajikuta ghafla tu yuko kwenye jia ya mteremko…anakua tajiri tu, anafanikiwa tu, nk. kwa sababu “alimtafuta KWANZA Mungu na HAKI yake”, hayo mengine akazidishiwa, japo hakuyaweka kwenye list ya maombi yake!

Angalia hapa, Yesu anasema, “kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao? Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani haba? msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.” (Mathayo 6:25-34).

Tatizo liko katika KUSUMBUKA, MASHAKA na HAOFU ya maisha! Na Yesu anaona hii ni dalili ya “imani haba”, tena anawafananisha watu wa namna hii kama “mataifa”, watu wasio mjua Mungu, kwa sababu hao husumbuka, huangaika, huwa na hofu ya maisha, nk. Kama kuna jambo linalompendeza Mungu ni imani yako kwake. Ndio maana tunaambiwa “haiwezekani kumpendeza Mungu pasipo imani”, na “yeyote amwendaye lazima aamini kwamba Yupo”. Sasa unaweza ukadhani ni utani lakini ukiangalia maisha ya watu wengi kwa makini utadhani hawajui kama Mungu yupo, japo wanamwomba kila siku na wanaenda kanisani. Na kwa kukosa imani wanajikuta kila siku maisha yao ni ya kupanda mlima tu. Hebu jifunze kwenda mbele za Mungu kumshukuru, kumsifu, kumwabudu, kuutafuta tu uso wake, na kuomba rehema na utakaso, zidi sana hapo na kudumu katika kumshukuru na kumtukuza huku ukijua “haja zako ZOTE ziko wazi mbele zake”. Utaniambia tofauti utakayoona hapo tukikutana. Siku zote kumbuka, sio mapenzi yetu yatimizwe bali ni mapenzi ya Baba, na tukiondoa kila ubinafsi na tamaa ndani yetu, Mungu anajibu kwa kipimo cha kujaa kusukwasukwa na kufurika. Yesu aliye ahidi kwamba “tukiomba neno lolote kwa jina lake atajibu” sio muongo.

Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi tangu sasa na hata milele, amen.

Frank Philip.



Comments