SARA K-NIMEANZA KUIMBA KWA KUKOPA PESA



  
Sarak K

SARAH K ni muimbaji anayegusa watu wengi hasa kutokana na nyimbo anazoziimba, lakini ni wachache sana wanaofahamu historia ya muimbaji huyo.

Muimbaji huyo aliyezaliwa miaka 42 iliyopita, ameolewa na mchungaji japo kabla ya kuanza huduma ya uimbaji, alishafanya jitihada nyingi maishani ikiwemo kuuza mbogamboga ili mradi maisha yasonge.

Makala haya yanaangazia maisha na mapito magumu aliyoyapitia muimbaji huyo kabla ya kuinuliwa na Mungu.
Kabla ya kuanza huduma ya uimbaji, Sara ambaye jina lake kamili ni Sarah Kiriare alikuwa akikusanya fedha kidogokidogo ili apate kuingia studio, ambapo alikuja kufanikiwa na kutoa albamu kwa lugha yake ya asili.
Sarah K na mwanae katika pozi
Mbali ya changamoto mbalimbali alizowahi kupitia ikiwemo kukatishwa tamaa na baadhi ya rafiki zake tena wa karibu, ikiwemo kudai kwamba sauti yake haifanani na uimbaji na kwamba ni kama vile anaongea na si kuimba na pia wengine wakisema sauti yake ni ya kiume, jambo ambalo kwa kweli lilimhuzunisha sana, lakini yote hayo hayakumzuia kusonga mbele.

Pamoja na kudharauliwa na kuonekana hafai kwa baadhi ya waimbaji ambao kwa namna moja au nyingine amewafanya kujulikana mbele ya jamii, pia ni jambo ambalo Sarah anaguswa nalo moja kwa moja.

Sarah anasema kuwa suala la kudharauliwa lilikuwa likimliza na kuamua kumlilia Mungu hadi kufikia hapo alipo; ni matokeo ya kusema jambo linamlomsumbua kwa Mungu wake, mathalan msanii mmoja aliyewezeshwa kupitia Sarah, na kisha baada ya hapo maneno yakaanza, ikiwamo kudai kuwa Sarah si lolote wala si chochote kwa maana hajawika kama ambavyo muimbaji huyo aliyewezeshwa kutoka anavyowika.

Muimbaji huyo ameshawahi kuuza nyanya, magunia, kutembea kwa mguu kwa kukosa nauli, kuimba kwa kukopa pesa ya studio na albamu haitoki kutokana na kuwa na deni kubwa, kutembeza kanda mguu kwa mguu.

“Niseme tu nimeshapitia maisha magumu; nimeshauza nyanya, nimeuza sukuma, nimeuza mangurunya, nimetembea mguu yaani kwa miguu bila ya kupata hela ya kwenda na gari.
“Nimeanza kuimba kwa kukopa pesa; naomba pesa za studio; naenda halafu siuzi kwa hivyo nadaiwa hizo fedha sijui nizitoe wapi.

Nimeshalia, nimeshatembeza kanda zangu zikiwa mfukoni nikipeleka kwa wenye maduka yaani mambo yalikuwa magumu mpaka mahali Mungu akanifikisha nasema asante.”
Sarah K akiwa katika pozi na mwanae

Sarah K ameolewa na ana watoto watatu na anasema kuwa yeye ni Mkenya; anaeleza sababu za watu wengi kulia akiimba nyimbo zake: “Nimeshaona hivyo tena mara nyingi nikienda kwenye kanisa ambako ninakwenda kuhudumu, ninajikuta hata mimi mwenyewe nalia, kanisa pia hata watu wengi wanalia nadhani kwa sababu wanapata mguso ambao pengine kuna mambo walishapitia, pengine wamekata tamaa yaani ile basi kama vile wanaona Mungu amewasahau lakini niwaambie kuwa Mungu anatuambia tusishughulike sisi wenyewe tusije tukafichaficha au tukajifanya hatutaki kuyataja, tumwambie waziwazi ndivyo ninavyoomba yaani nikulisema linalonitatiza,” anasema.

Sarah K aliyeanza huduma ya uimbaji mwaka 1991 ambapo alitumia lugha yake ya asili na kufanikiwa kutoa albamu tatu kwa lugha yake.

“Nina albamu kama tatu hivi za kilugha halafu mwaka wa 2000 ndio nilitoa albamu ya kwanza iliyokuwa inaitwa Wamtumainio Bwana na Mwimbieni Bwana nyimbo kama hizo. Halafu mwaka 2003 ndio nikatoa albamu ya Milele Daima na ndani yake ndio kuna wimbo ‘Nasema Asante’.
“Hivyo ukijumlisha zote za Kiswahili na Kiingereza ni Wamtumainio, Milele Daima, Adonai, Testimony na nyingine; na sasa nina Liseme na nimetoa albumu nyingine mpya ya sita ambayo ni mpya.

“Hiyo ina siku kadhaa sasa kwa hivyo za Kiswahili ni sita na za kilugha kama tatu hivi,” anasema.
Muimbaji huyo anasali katika kanisa la Anglikana ambapo mume wake ni mchungaji na anasema: “Ombi langu ni kwamba namwamini Mungu nitaendelea katika huduma yangu ya uimbaji hata kama nitakuwa na miaka 80 hata kama nitakuwa na miaka 90.

“Nitaendelea kumwimbia Mungu na kuwa mnyenyekevu na mtiifu mbele zake sio mbele za watu tu.
“Katika utunzi wangu ninamhusisha Mungu zaidi ya mimi mwenyewe ninavyojiona “Siwezi kusema ooh kwa sababu nina albumu tisa au 10; yaani nina ujuzi kabisa wa utunzi kwa hivyo simhitaji Roho Mtakatifu na simhitaji Mungu-siwezi kumsahau Mungu.


“Ninawajenga watu mioyo yao; nitakuwa nawainua watu mioyo yao ambao ni wadhaifu kwenye maeneo ambayo Roho Mtakatifu ananipa watasikia wameinuka na kuwa na matarajio kwamba Mungu yupo na ataendelea kuwatendea makuu-ni mengi tu wacha niachie hapo kwanza.”
Muimbaji huyo anawataka wasanii wachanga wasife moyo na wafuatilie ndoto zao na maono yao kwa sababu kuna mambo mengi ambayo yanaweza kupotosha uimbaji wao.
“Mambo mengi huja kwa mtindo kwamba umefika kumbe bado hujafika; nitakutolea mifano miwili: hili linaweza kuzungumziwa kwa urefu sana katika uimbaji, inaweza ikaja ukiwa mchanga halafu Mungu akakupa kibali sana mbele ya watu kwa wimbo wako kupendwa na ukauzwa sana.
“Sasa hapo kikwazo kimoja kinaweza kukufanya ukarudi nyuma; ni zile hela utakazozipata kutoka kwenye uimbaji ule zinaweza kukutikisa ukarudi nyuma ukakosa kufuatilia yale maono yako uliyokuwa nayo au ahadi ulizoweka mbele za Mungu.

“Unajua kuna ahadi zile uliweka wakati uko chini kabisa ukamwambia Mungu, ‘Utakaponivusha, utakaponibariki nitafanya mambo kadhaa’; kwa hivyo unajikuta umesahau.
“La pili ni ile umaarufu wakati wimbo wako ume-‘hit’ ukajulikana sana kuna ule umaarufu unaoupata kila mtu anakuita Sarah K, Sarah K kila mtu anaongea juu yako redio zote zinakutaja; kwa hiyo hiyo umaarufu ukishaingia ndani yako na ukaukubali kwamba wewe ni maarufu ndipo kiburi kitaanza kujiinua.
“Ni vema kuendelea kuwa mnyenyekevu tu daima na umshukuru Mungu.


sarahthubi@yahoo.com
www.sarahkiarie.com 
 

Comments