SOMO : KURUDISHA KIBALI KILICHOIBIWA NA MCHUNGAJI GWAJIMA

Na. Mchungaji Kiongozi Josephat Gwajima ,Ufufuo na Uzima,Tanganyika parkers Kawe


Matendo 19:20
“Na wengi wa wale walioamini wakaja wakaungama, wakidhihirisha matendo yao. 19 Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu. 20 Hivyo ndivyo neno la Bwana lilivyozidi na kushinda kwa nguvu. “ Mungu anapotaka kumariki mtu, majira ya Baraka yanapofika hata iweje lazma atapokea. Mungu ni Mungu wa nyakati na majira.

Galatia 4:4-6
‘Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria,…’ unaweza kulaumu kuwa umeombewa mara nyingi na hukupokea, wakati mwingine ni kwa sababu saa yako inakuwa haijafika. Wakati ukifika utapokea tu.
Mhubiri 3:1
‘Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. 2 Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; Wakati wa kupanda, na wakati wa kung'oa yaliyopandwa; …’

Mungu anatubariki wakati ukifika, Wachawi wapo, neno wachawi limeandikwa mara nyingi sana kwenye biblia. Katika Matendo 19:19Paulo anasema ‘Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu. ..’
Kuna wakati unaweza kuomba sana lakini kimya, sio kwamba Mungu hasikii ila wakati wako unakuwa bado kwa mfano mimi wakati nachunga kanisa Musoma, nilikuwa nimejipanga kufunga mara 2, 3 kwa wiki kwa ajili ya mambo flani lakini pamoja na kuwa serious kwa maombi na kufunga bado mambo niliyotaka yatokee hayakutokea kwa wakati ule niliotegemea! Ilifika wakati hadi nikawa kama nakata tamaa hivi! kumbe wakati ulikuwa haujafika. Hayo maombi hayapotei hivihivi ila yanakuwa akiba kwa ajili ya wakati husika. Na wakati ukifika unapokea bila hata kufanya vita sana.
Zamani watu kabla ya kwenda kwa wafalme walikuwa wanamwomba Mungu kibali. Wakati wako wa kuinuliwa ukifika, Mungu huwa anatumia watu kukuinua‘ God always raise people through people’.

Wachawi sasa huwa wana uwezo wa kuona kuwa huyu mtu anakoelekea anaelekea kupata mtaji, kuolewa, kupata kazi. Shetani ana uwezo wa kujua nyakati, kumbuka Yesu wakati akipita aliyaamuru mapepo yamtoke mtu, yale mapepo yalipaza sauti na kuomba wasiangamizwe mana wakati wao bado.
Ufunuo 12:12 ‘ Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.’
Hivyo shetani anajua kalenda, anajua wakati. Shetani anajua majira yako ya kuinuliwa, anajua dada fulani ifikapo February,2014 atakutana na bwana xx ambaye atamuinua kwa kumpa mtaji n.k, shetani na waganga wanachofanya ili kuzuia ni kukuondolea kibali mbele ya huyo mtu. Huyo mtu hata kama ana nia kiasi gani ya kukusaidia, atakapokuona tu anajisikia kama kuahirisha au anaanza kuona kama hufai kuaminiwa hivi. Au wakati mwingine anakufunika, mtu aliyetumwa kukuinua, kukuchumbia asikuone.

Miaka 7 iliyopita nilikaribishwa kwenda kuhubiri pale Japan, mimi nilishazoea kuhubiri watu wengi, nilipokaribishwa kuhubiri, pale walipokuwepo watu 13 tu. Nikavunjika moyo lakini nikahubiri, baada ya kumaliza kuna jamaa mmoja kutoka Tokyo akaniambia amependa ninavyofundisha atanialika Tokyo mwaka unaofuata, ulipofika muda huo akanialika nilipoenda nilishangaa kukuta watu wengi wamejaa, zaidi ya 4,000, na kutokea hapo nikaanza kuhubiri mikoa yote ya Japan na watu wanakuwa wanajaa, na kwa kutokea hapo nikawa naenda kila mwaka Japan, hadi Helcopter ikatokea. Ila yote yalianza na mtu mmoja tu. Hivyo ikawa utukufu juu ya utukufu, hatua juu ya hatua, nguvu juu ya nguvu. Na kwa upande wa Ulaya ikawa hivyohivyo, nilianzia Uingereza, wakatokea watu wakasema lazma niende na Norway, kufika Norway wakatokea waliosema niende na Sweeden, Poland n.k mara nikajikuta nimehubiri katika nchi nyingi katika bara la Ulaya. Yote hayo yalisababishwa na kibali. Shetani anajua kalenda yako, anajua nyota yako imeng’aa na kuna mtu sehemu fulani anakusubiri.
Hawezi kukubali kirahisi.

Mfano wa kweli Yesu alizaliwa katika familia maskini, familia ya fundi seremala, lakini ni mwana wa Mungu! Mungu hufanya kazi kupitia watu wanyonge/hali nyonge. Yesu wakati akizaliwa, mamajusi kutoka mashariki ya mbali walisafiri miezi na miezi kwenda kwa fundi seremala kisa kibali kimeonekana. Yaani kibali cha Yesu ndio kilisababisha vitu vizuri vimfuate, dhahabu, manemane n.k Mkikutana watu wawili wenye sifa sawa,mmoja mwenye kibali na mwingine hana kibali, Yule mwenye kibali ndiye atakaye pasua.
Kisa cha kweli Siku moja nilishangaa sana, wakati tunasafiri kwenye ndege, kuna mtu akazidiwa sana ndani ya ndege, wahudumu wakauliza kama kuna daktari aje amsaidie. Ikawa kimya! Baadae mhudumu akaja moja kwa moja kwangu na kuniambia ‘Dr. naomba ukamsaidie mgonjwa’ nikashangaa sana, kaona nini kwangu maana mimi si daktari. Basi nikakubali nikamsogelea yule mgonjwa, nikakuta anahemea juu, nikamshika kifuani nakatamka kimoyomoyo ‘ewe pepo la presha mwache huyu kwa jina la Yesu’ yule mgonjwa akapumua kwa nguvu na kuamka akiwa mzima kabisa na kunishukuru. Uongozi kwenye ndege ukanishukuru kwa kunipa dola 100, unaona kibali ndio kilimfanya haya mhudumu wa ndege aje kwangu na kupitia nilichofanya nikapata dola mia.
Na wewe Mungu asababishe jambo utakalolitolea ufumbuzi na kupitia hilo uinuliwe katika jina la Yesu’ Kuna watu wanaweza kuchukua sura za watu na viungo vya watu na kuanza kutumia kwa shughuli zao za kichawi. Leo natoa tangazo liende kote, iwe bungeni, wizarani na popote, yeyote unayetumia ubongo wa mtu, kazi ya mtu, sura ya mtu au chochote RUDISHAAAAA!!!!

Shetani hajawahi kuumba chochote, isipokuwa anachukua vya watu na kuvitumia kwa shughuli zake. Shetani anaweza kuchukua sura ya mtu ya kibali na kuwabandika watu wake kwa madhumuni fulani mfano kushinda mashindano ya urembo, n.k. Kuna watu wamejivika sura za watu wengi, hivyo ananawiri tu, na wale walioibiwa wanabaki wamenyong’onyea tu. Ila huu ni wakati wa Bwana lazima vyote vilivyoibwa virudi katika jina la Yesu. Ulikuwa unakubalika kwa watu ila leo hukubaliki tena, ni kwamba kuna mtu wa karibu ndugu, rafiki n.k anakuwa amechukua kibali chako kwa faida zake. Kila unachowaza kufanya unakuta kimeshafanywa.

Kila mtu ni mzuri, ila kila mtu ana kibali chake katika eneo fulani. Yaani hilo eneo Mungu anakuwa amekupa ‘divine acceptance’. Sasa kinapochukuliwa mambo yananza kwenda vibaya. Wakati wa uchaguzi ni kitu gani kinafanya watu wamshabikie sana huyu na sio huyu ni kibali. Kuna kukubalika kulichotengenezwa kwa utendaji wa mtu, ushirikina. Na kibali cha asili ambacho mtu anakuwa nacho, kila akitokea sehemu watu wanamfurahia. Na kuondoka kwake hicho kibali ni rahisi, ni mtu tu anaenda kwa mganga anachukua chako, halafu anakubambika mashetani ya kuondoa kibali unashangaa sana mambo yanaanza kwenda vibaya, watu hawakufurahii tena.

Hebu nikupe siri ya ajabu- wachawi wanapenda ukubali tatizo. Mfano kama uso una shida uone uso huu ni wa kwangu ila una matatizo….. Ukitaka kumkomesha mchawi kataa hiyo hali! Sema nakataa, uso huu si wangu, chukueni uso wenu. Utakapokubali unakuwa wako kweli. Unapokataa na kuurudisha ulipotoka kweli unarudi. Unaweza kushangaa zamani ulikuwa ukifanya biashara mambo yanaenda vizuri lakini siku hizi mambo hayaendi watu hata hawataki kufanya biashara na wewe kwa sababu kile kibali kinakuwa kishachukuliwa, hivyo kile kilichokuwa kinamvuta kwako kinakuwa kimeondolewa, unaweza kudhani una matatizo kumbe wala ni kibali kimechukuliwa.

Korintho 6:16
‘..Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja. 17 Lakini yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye..’

Kuna mtu kibali chako kimeondolewa kwa sababu ya kuwa na mke/mume wa kiroho. Unaota unakutana kimwili na mtu, hii si ndoto bali ni bayana. Huyo aliyekujia ni mume/ mke wa kiroho ‘spiritual husband/wife’. Anaweza kuwa jini, joka, mzimu. hivyo katika ulimwengu wa roho wewe na huyo mnakuwa ni mwili mmoja kwa maana mmefungishwa ndoa katika ulimwengu wa roho. Hiki ni kisababishi kikubwa cha kukosa kibali. Watu wote walio kwenye ndoa halafu wana waume/wake wa kiroho ndio wenye matatizo ya kindoa. Haya majini yanakuja yenyewe. Yanazuia kila maendeleo katika maisha yako, ni mawakala wa kumfanya mtu akose kibali. Haya yana nguvu sana kwa sababu kuna agano la ndoa. Agano la ndoa Inakuwaje wanakuja kwa mtu;
1. Kuokota vitu mfano. pete ya dhahabu nzuri, utakapovaa hiyo ndio tayari ndoa. Baadae itakuja kupotea au kuibiwa, lakini ndio unakuwa ushaolewa hivyo,
2. Kukutana kimwili na asiye mtu- majini yanauwezo wa kuvaa mwili na kuwa kama watu. Majini ni malaika (wachafu), kumbuka wale wageni aliowapokea Ibrahimu walikuwa kama watu kabisa lakini walikuwa malaika.
3. Uhusiano wa kimapenzi na mtu mwenye majini Ili kuvunja mkataba wa ndoa za kichawi/kishetani lazma utamke. Siku moja nikiwa Japan nikihubiri, kuna binti mmoja anaitwa Masami, maombi yalipopamba moto alianza kuruka na kuparamia miti, tulivyomkamata akaanza kusema kuwa yeye ni mtumishi wa shetani. Anachofanya ni kuwa na mahusiano na watu wakubwa, akilala nao anaachilia vitu vya ajabu ndani yao na huo wanaume wanaenda kuviachilia kwa wake zao au kwa yeyote atakayelala nao, ndo matokeo yake kuzaliwa watoto walemavu au waliokufa. ‘Ninavunja maagano ya ndoa za kishetani/kichawi kwa jina la Yesu, nadhoofisha utawala wa majoka katika maisha yangu katika jina la Yesu.....’
Ufufuo na Uzima,Tanganyika parkers Kawe

IMEANDALIWA NA INFORMATION MINISTRY. UFUFUO NA UZIMA
 

Comments