Askofu Zachary Kakobe akifundisha somo la ufufuo na uzima

moja ya huduma za Askofu Kakobe, hapa akiwaombea wachungaji katika semina mjini Lubumbashi .


L
eo, katika Siku yetu ya Kuichambua Biblia, tunaendelea kujifunza Kitabu cha YOHANA katika Biblia zetu na kutafakari YOHANA 11:17-46.  Kichwa cha Somo letu la leo, ni “UFUFUO NA UZIMA“, hata hivyo, kuna mengi zaidi ya kujifunza katika mistari hii.  Tutayagawa mafundisho tunayoyapata katika mistari hii katika vipengele tisa:-

(1)      KUTOKUCHELEWA KWA MUNGU (MST. 17-18);
(2)      MAHUDHURIO YA WATU WENGI KATIKA MSIBA (MST. 19);
(3)      UFUFUO NA UZIMA (MST. 20-25);
(4)      AISHIYE NA KUNIAMINI, HATAKUFA KABISA HATA MILELE (MST. 26-
27);
(5)      YESU AKALIA MACHOZI (MST. 28-37);
(6)      LIONDOENI JIWE (MST. 38-40);
(7)      NGUVU YA SHUKRANI (MST. 41);
(8)      LAZARO, NJOO HUKU NJE (MST. 42-44);
(9)      KUMWAMINI YESU BAADA YA KUONA ALIYOYAFANYA (MST. 45-46).

(1)      KUTOKUCHELEWA KWA MUNGU (MST. 17-18)
Yesu Kristo, alifika Bethania kwa Lazaro, na kumkuta amekwisha kuwamo kaburini yapata siku nne.  Ilionekana kana kwamba amekwisha kuchelewa na haiwezekani tena kwa Lazaro kuwa mzima.  Hata Martha na Mariamu, wakasema “Kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa“ (MST. 21, 32), kwa kumaanisha kwamba kwa sasa amekwisha chelewa.  Ni muhimu kufahamu kwamba kuchelewa, ni kwetu wandamu tu.  Tukichelewa usafiri wa basi au ndege, tayari tunakuwa katika tatizo kubwa n.k.  Kwake Yesu, sivyo, Yesu hachelewi kamwe.  Yesu alimponya mtu kiwete aliyekuwa katika hali hiyo kwa miaka 38 (YOHANA 5:2-9).  Alimponya pia mwanamke aliyetokwa damu kwa miaka 12 (MARKO 5:25-34).  Alimponya mwanamke aliyekuwa na pepo wa udhaifu muda wa miaka 18 akiwa amepindana (LUKA 13:11-13).  Alimponya mtu kipofu aliyekuwa katika hali hiyo, TANGU KUZALIWA (YOHANA 9:1-11).  Hata kama tatizo letu limechukua muda mrefu kiasi gani, na kuonekana kana kwamba mambo yamekwisha kuharibika, ni muhimu kukumbuka kwamba Mungu wetu hachelewi.  Anaweza kuingilia kati popote pale na kutujibu kwa utukufu wake.  Wakati wake wa kufanya miujiza, huwa mzuri zaidi kuliko wakati wetu.  Inatupasa kuwa na subira kama Ayubu, na kuungojea wakati wa Mungu wetu asiyechelewa (YAKOBO 5:11).

(2)      MAHUDHURIO YA WATU WENGI KATIKA MSIBA (MST. 19)
Watu wengi katika Wayahudi, walikuwa wamekuja kwa Martha na Mariamu, ili kuwafariji katika msiba huo.  Huu pia, ndiyo wajibu wa kila ajiitaye Mkristo.  Inatupasa kuhudhuria kwa wingi wetu katika misiba ya ndugu zetu katika Kristo na kutoa faraja zote.  Mungu mwenyewe, alimzika Musa (KUMBUKUMBU 34:5-6).  Ikiwa Mungu alichukua kwa uzito mkubwa mazishi ya Musa, sisi nasi tunajifunza kama Wakristo kuchukulia kwa uzito mkubwa mazishi ya ndugu zetu katika Bwana.  Vivyo hivyo Yohana Mbatizaji alizikwa kwa uzito mkubwa na ndugu katika Bwana (MATHAYO 14:6-12).  Mahudhurio yetu katika msiba wa ndugu yetu katika Bwana, hayana budi kuwa ya watu wengi ili tuonyeshe upendo wetu wa Kikristo.  Siyo hilo tu, tunajifunza hapa kwamba Yesu naye, alihudhuria katika msiba huu.  Ndivyo ilivyo hata leo, Yesu huhudhuria katika msiba wa kila mtu aliyeokoka.  Ndiyo maana hutupa faraja ya kipekee.
(3)      UFUFUO NA UZIMA (MST. 20-25)
Yesu anajitaja hapa kwamba, “Mimi ndimi huo ufufuo na uzima (MST. 25).  Yesu ni UZIMA (YOHANA 14:6), hata hivyo, Yeye ni zaidi ya Uzima, Yeye ni Ufufuo na Uzima.  Kwa kuwa Yeye ni Uzima, hutuponya katika magonjwa yetu.  Kwa kuwa Yeye ni Ufufuo, ana uwezo pia wa kufufua viungo vyetu vilivyokufa kabisa.  Yesu kama Uzima, anaweza kuziponya Ndoa, kazi au biashara zetu zinazolegalega.  Hata hivyo, Yesu kama Ufufuo, ana uwezo wa kuzifufua ndoa, kazi au biashara zetu zilizokufa kabisa.  Anaweza pia kufufua maisha yetu ya maombi, na kumtumikia Mungu, yaliyokufa.

(4)      AISHIYE NA KUNIAMINI HATAKUFA KABISA HATA MILELE (MST. 26-27)
Kufa hapa, kunazungumzia mauti ya milele au ghadhabu ya Mungu, moto wa milele (YOHANA 3:36).  Yeye aliyeokoka, hukumu hiyo ya adhabu huwa mbali naye (WARUMI 8:1-2).

(5)      YESU AKALIA MACHOZI (MST. 26-37)
Yesu hulia na waliao, na kufurahi pamoja na wafurahio, kama anavyotuagiza kufanya (WARUMI 12:15).  Anatupenda upeo.  Huzuni yetu, ni huzuni yake na furaha yetu, ni furaha yake.  Hivyo hatupaswi kuwa na mashaka juu ya kuhusika kwake na matatizo yetu.

(6)      LIONDOENI JIWE (MST. 38-40)
Kuna sehemu yetu ya kufanya katika ukamilishaji wa kila muujiza tunaouhitaji.  Ikiwa hatuliondoi jiwe, ni vigumu kumwona Lazaro akifufuka.  Hatuna budi kuangalia kwamba kuna jiwe gani la kuondoa, katika kupata miujiza yetu.  Ikiwa tunaomba mfanikio ya kifedha, jiwe la kuondoa, ni kuhakikisha tunatoa fungu la kumi la mapato yetu YOTE hata kama ni madogo.  Ikiwa tunataka kazi, jiwe la kuondoa, ni kuhakikisha tunahusika kikamilifu kutafuta kazi na kuondoa uvivu.  Ikiwa tunahitaji mtoto, tuhakikishe tunakutana waume na wake zetu katika siku za mwezi zilizo na rutuba ya uzazi na tuondoe kila namna ya chuki na ugomvi siku hizo, maana hayo yatatufanya tusikutane siku za rutuba na kukutana siku zisizo na rutuba.

(7)      NGUVU YA SHUKRANI (MST. 41)
“Baba NAKUSHUKURU“, ni maneno ya Yesu yanayotufundisha kushukuru.  Tukiondoa shukrani katika maisha yetu ya maombi, tunabakiwa na sifuri.  Shukrani zina nguvu ya ufufuo.  Tunapaswa kuunga maombi na shukrani wakati wote, ikiwa tunataka kuona nguvu ya Ufufuo ya Yesu ikitenda kazi (1 WATHESALONIKE 5:17-18; WAKOLOSAI 3:15).  Je, ni kweli kwamba Mungu hajatutendea lolote lililo jema?  Mbona tunaomba tu bila kushukuru?  Tuanze na shukrani kwanza kabla ya maombi yetu kila inapowezekana.  Tumshukuru hata kwa hewa tunayoivuta bila malipo.

(8)      LAZARO, NJOO HUKU NJE (MST. 42-44)
Watu WOTE waliomo makaburini, wataisikia sauti ya Yesu wakati wa Ufufuo (YOHANA 5:28-29).  Hapa Yesu alisema “LAZARO NJOO HUKU NJE“.  Kama angesema “NJONI HUKU NJE“, wote waliokufa tangu wakati wa Adamu, wangekuja!  Ni kwa sababu hii alitaja jina la huyu Lazaro anayehusiana na Martha na Mariamu.

(9)      KUMWAMINI YESU BAADA YA KUONA ALIYOYAFANYA (MST. 45-46)
Wengine huwa tayari kuokoka, KABLA ya kuona miujiza; lakini wengine huwa tayari kuokoka, BAADA ya kuona miujiza kama hapa.  Katika kushuhudia kwetu, hatupaswi kumwekea Mungu mipaka na kusisitiza kumwombea mtu matatizo yake pale tu anapokuwa tayari kuokoka kwanza.  Asipokuwa tayari kuokolewa, tumwombee tu.  Mapepo yake yakitoka au akipata muujiza wowote, ni rahisi kuvutwa kwa Yesu na kuokolewa pia kama watu hawa.  Akiokoka kabla ya maombezi, ni vema zaidi, hata hivyo tusiweke hiyo kuwa KANUNI.
…………………………………………………………………………………………………………………………………..
Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 
Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Neno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe     tembelea sehemu zifuatazo katika inernet  
Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org
Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries
Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe



Comments